HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 2, 2022

TMA YATAJA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU NA MAFANIKIO YAKE KWA MWAKA 2022/2023

 

Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri Dkt. Hamza Kabelwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma leo Novemba 2, 2022 wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu na mafananikio ya Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini kwa mwaka wa fedha 2022/2023

MAMLAKA ya hali ya Hewa nchini, inesema katika utelekezaji wa majukumu yake katika mwaka wa fedha 2021/22 wamepata mafanikio mbali mbali ikiwemo kuongezeka kwa asilimia 53 ya Mapato kwa kuwafikia wadau wengi na kuwaeleza juu ya umuhimu wa kutumia huduma za hali ya hewa na pia kuchangia huduma hiyo.

Pia Mamlaka iliendelea na utekelezaji wa mradi wa Rada, Vifaa na miundombinu ya hali ya hewa ambapo hatua mbalimbali zilifikiwa.

Hatua hizo ni pamoja na kukamilika kwa asilimia 90 ya utengenezaji wa mtambo wa rada mbili za Mbeya na Kigoma ambapo malipo asilimia 90 yamefanyika huku mafunzo kwa wahandisi na waendesha mitambo kuhusu kuzihudumia na kuzitumia Rada hizo yakiwa yalishafanyika kiwandani nchini Marekani.

Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri Dkt. Hamza Kabelwa ameyasema hayo Jijini Dodoma, leo Novemba 2, 2022 wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu na mafananikio ya Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini.

Dkt. Kabelwa amesema miundombinu ya Rada za Mbeya na Kigoma imekamilika huku tengenezaji wa Rada mbili za mwisho zitakazofungwa KIA na Dodoma umefikia asilimia 45.

Ametaja utekelezaji mwingine ni kufungwa kwa Mitambo miwili ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe inayohamishika na “measuring cylinders” zipatazo 100; Seti tano za vifaa vya kutambua matukio ya radi; Vifaa 15 vya kupima mgandamizo wa hali ya hewa; vifaa 25 vya kupima kiasi cha joto na unyevunyevu; mitambo minne ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe; vifaa vya kupima mvua vinavyojiendesha vyenyewe.

Aidha Mamlaka imepokea kompyuta maalum “Cluster Computer” na pia imefunga mfumo mpya wa uangazi wa hali ya hewa ya anga ya juu katika kituo cha kupima hali ya hewa ya anga ya juu kilichopo JNIA.

Amesema, Mamlaka pia imeingia mkataba wa ununuzi wa vifaa na mitambo mbalimbali ya yali ya hewa ya kutoa huduma za hali ya hewa kwa ajili ya usafiri wa anga na kupima hali ya hewa mahususi kwa sekta ya kilimo. Aidha,

Ameendelea kutaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja kutekeleza jukumu la kutoa utabiri wa hali ya hewa wa kila siku, siku tano, siku kumi, msimu na tahadhari ambapo usahihi wa utabiri katika kipindi husika ulikuwa asilimia 93.8 ukiwa juu ya asilimia 70 ya kiwango cha usahihi kinachokubalika kimataifa;

"Huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga imeendelea kutolewa kwa kuzingatia mfumo wa kudhibiti ubora wa huduma (ISO 9000:2015) ambapo jumla ya ndege 40,323 zimehudumiwa katika mwaka 2021/22 ukilinganisha na ndege 35,111 zilizohudumiwa katika mwaka 2020/21 ikiwa ni ongezeko la asilimia 13" amesema Dkt. Kabelwa.

Ameongeza kuwa Mamlaka imeendelea na utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa watumiaji wa Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu kupitia ofisi zake zilizopo kwenye Bandari za Bahari ya Hindi na Ziwa Victoria, Nyasa na Tanganyika na kwamba huduma hizo zimechangia kuongezeka kwa usalama na ufanisi wa shughuli za kiuchumi zinazofanyika kwenye maji.

"Mamlaka imeendelea kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake iliyopewa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani ya kuwa Kituo cha kutoa mwongozo wa utoaji wa utabiri wa hali ya hewa kwa nchi za ukanda wa Ziwa Victoria (Regional Specialized Meteorological Centre) kwa nchi zilizopo Afrika Mashariki n kusaidia ufuatiliaji wa ubora na upatikanaji wa data za hali ya hewa kwa vituo vya hali ya hewa vilivyo katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, na Sudan ya Kusini kupitia kituo cha Kanda kilichopo Tanzania". Amesema Dkt. Kabelwa

Mamlaka ilipata hati safi ya ukaguzi wa hesabu katika ukaguzi wa mwaka 2020/21 uliofanywa na wakaguzi kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Uboreshaji kwenye mifumo ya kihasibu ulifanyika ambapo Mamlaka ilihamia katika Mfumo wa Uhasibu Serikalini (MUSE). Aidha, katika ukaguzi uliofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Mamlaka ilipata alama ya asilimia 88 ambayo inaonyesha kuwa Mamlaka inazingatia matakwa ya Sheria katika utekelezaji wa shughuli za manunuzi

Amesema, TMA imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kupunguza gharama za uendeshaji wa Taasisi ambapo imeweka mkazo katika kutumia TEHAMA kwa ajili ya uendeshaji na utoaji wa huduma na kuboreshewa maslahi ya ya wafanyakazi kupitia kupandishwa vyeo, kubadilishwa Kada na kuhuishwa kwa miundo ya kada kwa watumishi wa Mamlaka kufuatia Mabadiliko ya Miundo ya Maendeleo ya watumishi (Schemes of Services).

Aidha,TMA imeendelea na utekelezaji wa mpango wa mafunzo kwa watumishi ambapo jumla ya wafanyakazi 50 walikuwa masomoni katika ngazi za (PhD, MSc, BSc and Diplomas) ndani na nje ya nchi, kati yao 3 PhD; 11 MSc.; 34 BSc.; 1 BA; na 2 ngazi ya shahada huku pia ikitekeleza azma ya Serikali kwa kuhamishia Ofisi za Makao Makuu Dodoma.

"Kukamilika kwa ukarabati wa majengo ya Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa (National Meteorological Training Centre - NMTC) kilichopo mkoani Kigoma na ukarabati wa vituo vya hali ya hewa ambapo vituo nane vilivyopo katika mikoa ya Singida, Songwe, Dodoma, Tabora, Mpanda, Mahenge, Songea na Shinyanga vilikarabatiwa".

Aidha TMA imesema , katika utekelezaji wa mwaka wa fedha wa 2022/23, imepanga mikakati itakayosaidia katika utoaji wa huduma za Hali ya Hewa Nchini ikiwemo Kupanua wigo wa utoaji wa elimu kwa wananchi na wadau wengine juu ya umuhimu wa hali ya hewa.

Mikakati mingine ni kuimarisha uangazi wa hali ya hewa katika Bahari na Maziwa Makuu, kufanya ufuatiliaji kwa wakandarasi wanaotengeneza Rada na vifaa vya hali ya hewa kuongeza vyanzo vya mapato kwa lengo la kuboresha huduma za hali ya hewa Kuhakikisha wadau wote wenye vifaa vya hali ya hewa nchini wanavifunga vifaa hivyo kwa kuzingatia Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na. 2 ya mwaka 2019 na kanuni zake na kuendelea kuboresha miundombinu ya Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa huandaa miradi mbalimbali yenye lengo la kupata rasilimali kutoka kwa washirika wa maendeleo ndani na nje ya nchi ili kuboresha huduma za hali ya hewa nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad