HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 2, 2022

KIJANA WA MIAKA 20 AJIFANYA RAIS SAMIA FACEBOOK AHUKUMIWA

 

Kijana Nickson Mfoi (20) akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kuamuruliwa  kulipa faini ya sh. Milioni kumi ama kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani baada ya kukiri kosa la kujifanya yeye ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwenye mtandao wa Facebook.

Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
MAHAKAMA Hakimu Mkazi Kisutu imemuamuru kijana Nickson Mfoi (20) kulipa faini ya sh. Milioni kumi ama kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani baada ya kukiri kosa la kujifanya yeye ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwenye mtandao wa Facebook.

Shtaka jingine ni kuwa mshtakiwa alikutwa akimiliki na kutumia laini ya simu iliyo katika umiliki wa mtu mwingine bila kutoa taarifa kwa mtoa huduma.

Mfoi amekiri makosa yake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate baada ya kuomba kukumbushiwa mashtaka yake mahakamani hapo.

Kabla ya kusomewa adhabu yake baada ya kutiwa hatiani, upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa serikali, Ashura Mzava umeiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na kwa wengine ambao wamekuwa wakiendelea vitendo vya matumizi mabaya ya mitandao kwa kutumia majina ya viongozi na hata kuwakashfu.

Kwa upande wake mshtakiwa ameiomba mahakama imuonee huruma kwani wakati anatenda kosa hilo hakujua kama madhara yake ni makubwa.

Hakimu Kabate amesema, amepitia hoja za pande zote mbili na kuongeza kuwa...,Ukimzungumzia Rais ni wazi kuwa umeizungumzia Tanzania nzima, personation iliyoko katika shtaka hili siyo ya kawaida na jina ulilolitumia siyo la kawaida hivyo lazima udhibiwe.' Amesema Kabate.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Kabate amesema katika shtaka la kwanza la kujifanya yeye ni Rais Samia Suluhu Hassan mshtakiwa anapaswa kulipa faini ya Sh. Milioni tano au kwenda jela mwaka mmoja huku pia katika shtaka la pili anapaswa kulipa Sh.milioni tano ama kutumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani.

Hata hivyo mahakama imesema adhabu zote hizo zitakwenda pamoja ambapo mshtakiwa anapaswa kulipa sh. Milioni kumi na kama atashindwa basi atakaa gerezani mwaka mmoja tu.

Katika hoja za awali inadaiwa mshtakiwa alitumia akaunti ya Facebook yenye jina la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwa kujiwasilisha kuwa yeye ni Rais Samia Suluhu Hassan

Pia, mshitakiwa huyo alikiri kwamba kati ya Septemba, 2021 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa nia ya kulaghai umma alijiwasilisha kama Rais Samia Suluhu Hassan kupitia akaunti yake Facebook.

Pia alikutwa akitumia laini ya simu ambayo awali ilikuwa inamilikiwa na Getness Jackson kwa madai kwamba alipewa na mtu anayesajili laini.

"Ni kweli hii akaunti ya Facebook nilikuwa naitumia mimi, niliuziwa lakini yaliyokuwa yakiendelea humo mimi siyajui na ni kweli nilikuwa natumia simu ambayo haijasajiliwa kwa kidole changu," alidai Mfoi

Mshtakiwa Mfoi pia amekiri kwamba Septemba, 2021 alikamatwa na askari katika hoteli ya Malaika mkoani Mwanza na alipopekuliwa alikutwa ana miliki simu moja na laini iliyosajiliwa kwa jina la Jackson bila kutoa taarifa kwa mtoa huduma, ambapo alikamatwa na Agosti 4,2021 aliletwa mahakamani kwa ajili ya kujibu mashitaka yake.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad