HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, January 11, 2022

TAMBIKO LA WAYAO

 

Mti aina ya Msolo

Adeladius Makwega, Dodoma.
WAYAO hata kabla ya kuingia kwa Uisilamu na Ukristu katika eneo lao wanaloishi waliaamini katika uwepo wa Mungu (Ambuje Nnungu). Ikiaminika kuwa Ambuje Nnungu ni mwenye nguvu zaidi ya binadamu. Wakiamini pia hata mtu akifariki anapata uwezo mwingine na roho yake inakuwa na nguvu fulani na kuwa kama mzimu (Achimasoka).

Wayao wanaamini kuwa Achimasoka wapo jirani na binadamu kuliko huko alipo Ambuje Nnungu ambaye ni Mungu. Kila ukoo ukiaminika kuwa una Achimasoka wao ambao huwa na kazi ya kuyasikiliza maombi na wakati mwingine kuyakataa maombi hayo.

Kabila hili linaamini kuwa japokuwa Ambuje Mnunge na Achimasoka wanasikiliza maombi yao lakini maombi haya yapo yanayokwenda moja kwa moja kwa Ambuje Mnunge na yale yanayokwenda kwa Achimasoka.

Uzingatiaji huo wa kupeleka maombi Wayao wanaamini kuwa ni jambo la msingi mno na kitendo cha kuyapeleka maombi pahala ambapo si sahihi kinaweza kusababisha mwombaji kukataliwa kabisa maombi yake tangu wakati huo.

Swali ambalo linakuja hapo Je Maombi yepi yanapelekwa kwa Ambuje Nnunge na yale ya Achimasoka?

Katika jamii kunapotokea njaa, magonjwa makubwa ama uhaba wa mvua basi maombi haya hupelekwa moja kwa moja kwa Ambuje Nnunge na siyo kwa Achimasoka. Lakini kama tatizo hilo linakumba jamii ya wachache katika kabila hilo basi maombi hayo yanapelekwa mbele ya Achimasoka, ambapo awali nilikujulisha kuwa kila ukoo unakuwa na Achimasoka wake.

Maombi kwa Achimasoka huwa yanaitwa Mbepesi. Wayao wenyewe wanagawa Mbepesi katika makundi makubwa mawili: Mbepesi ja Pansolo na Mbepesi ja Kumakabuli.

Mbepesi ja Pansolo ni aina ya kale ya Mbepesi ambayo inaaminika kuwa sasa ni nadra mno, lakini hufanyika panapotokea balaa na wakuu wa ukoo uketi pamoja na kujadiliana juu ya shida hiyo alafu na watapanga miadi ya kufanyika kwa Mbepesi. Siku ikiwadia wakubwa hao wa ukoo wakiwa kati ya wanne na watano watachukua vyakula kama unga wa mahindi, mtama na chumvi. Watafunga safari hadi katika Mti wa Nsolo/Mti wa Msolo/Mti wa Solo hapo chini yake wataweka vyakula hivyo.

Wakifika katika mti wa Nsolo watafanya usafi wa eneo hilo vizuri na watafanya matambiko yao na kukiacha chakula chini ya mti huo, huku wakitazama mashariki. Hapo yatatajwa majina ya Achimasoka wao mmoja baada ya mwingine, pamoja na kutajwa orodha ya shida zinazowakabili.

“Chonde Achimasoka Kunndiko,

Tukumenda ntupilikanile Mbepesi yetu,

Mwalole Achvana venu yakuti pa kulanga,

Munape ensausyo Iwati yeleyi chonde,

Chonde Che (hapa watataja majina ya Achimasoka wao mmoja baada ya mwingine)

Uweji achi (hapa yatatajwa majina ya wazee wa ukoo waliopo hai wakati huo)

Tukumenda mwatyochesy (hapa zitatajwa orodha ya shida zao/maombi yao ya siku hiyo)

Ipisya yao Ikwapatayo.”

Kwa tafsiri ya moja kwa moja tunaweza kusema kuwa, tafadhali sana wazee wetu, popote mlipo tunawaomba sana, siye wana wenu maombi haya, mtutazame watoto wenu sasa tupo katika shida. Tunaomba mtuondolee tabu hizi. Tafadhali sana wazee wetu (watatajwa majina yao). Tuliopo hapa mbele yenu ni (watatajwa majina yao). Tunawaomba maombi yetu ambayo ni(yatatajwa maombi yao kwa siku hiyo). Mtusamehe na dhambi zetu.

Maombi haya yanafanyika wakati wa asubuhi sana au wakati wa jioni na wakiamini kuwa hao wazee wao watakuja na kuchukua chakula hicho kilichoachwa chini ya mti wa Nsolo.

Nilipokuwa nakamilisha andiko la utafiti huu nilipokutana na Mti wa Nsolo nilimkumbuka ndugu yangu mmoja niliyesoma nae Chuo cha Ualimu Kasulu Kigoma kati ya mwaka 2001-2003 Afande Nsolo Hamisi ambaye nadhani bado ni Afisa wa Jeshi letu la Polisi Tanzania. Jina lake hilo la ukoo Nsolo (Msolo) nilidokezwa kuwa labda walikuwa wakiishi jirani na mti huo, au babu yake alikuwa akiutunza mti huo au shamba lao lilikuwa jirani na mti huo lakini pia waliniambia kuwa inawezekana mmoja wa ndugu wa familia yao aliwahi kupata changamoto na mti huo kwa kuwa ni mti wa matambiko.

Nilijaribu kumtafuta Afande Nsolo, sikumpata angalau nimsalimie na anipe jibu juu ya ukoo wao kuitwa Nsolo/Msolo na pia azungumze na ndugu zake hawa, nadhani alikuwa bize na kazi ya kuwalinda raia na mali zao.

Mwanakwetu kwa sasa Wayao hawafanyi Mbepesi ja Nsolo kwa sababu mbalimbali. Bali sasa hufanywa aina ya pili ya Mbepesi inayofahamika kama Mbepesi ja Kumakabuli.

Mbepesi ja Kumakabuli hufanywa sawa sawa na hii ya Mbepesi ja Pansolo kwa kutumia maneno yale yale lakini wao mandari inabadilika badala ya chini ya Mti wa Nsolo sasa ni makabulini. Hufunga safari hadi makabulini hufanyia usafi alafu maneno hayo hayo hutamkwa.

Swali ambalo lakujiuliza leo je kwanini Wayao wanaacha tambiko la chini ya Mti wa Nsolo (Mbepesi ja Pansolo) na badala yake sasa tambiko linalofanyika sana ni lile la Mbepesi ja Kumakabuli? Jawabu ya jambo hilo inawezekana ni uhaba wa Mti wa Nsolo kwani haupatikani kila pahala. Ni mti mkubwa, ambao unatumia miaka kadhaa kukua. Kwa sasa miti mikubwa ni michache sana lakini makabuli yanapatika kila pahala binadamu tunapoishi kwa kuwa tunazaliwa, tunakufa na kuzikana.

Msomaji wangu katika matini hii umeweza kuona pale awali palipo na neno Nsolo niliweka Msolo hiyo ni kutokana na matamshi mengi ya watu kusini wa Tanzania kuwa na athari hiyo ya N na M usiwe na mashaka msomaji wangu.

Kwa leo mwanakwetu naweka kalamu chini hapo, nakuahidi kuwa nitaendelea kumtafuta Afande Nsolo Hamisi ili anipe jibu ya maswali yangu juu ya jina la ukoo wao. Nakutakia siku njema.


0717649257

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad