HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, January 11, 2022

WAZIRI NAPE AWASILI KATIKA OFISI YAKE MTUMBA, APOKELEWA NA MENEJIMENTI NA WATUMISHI WA WIZARA

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye akisaini kitabu katika Ofisi yake katika Wizara hiyo iliyopo Mji wa Serikali Mtumba mara baada ya kuwasili ofisini hapo baada ya kuapishwa Ikulu ya Chamwino Dodoma.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye (wa tatu kushoto mstari wa mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na Menejimenti na watumishi wa Wizara hiyo mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Wizara hiyo iliyopo Mji wa Serikali Mtumba. Wa pili kushoto ni Naibu wake Mhe. Mhandisi Kundo Mathew na kushoto kwake ni Katibu Mkuu Dkt. Jim Yonazi akifuatiwa na Naibu Katibu Mkuu Bw. Mohammed Khamisi.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye akizungumza na Menejimenti na watumishi wa Wizara hiyo mara baada ya kuwasili katika Ofisi yake katika Wizara hiyo iliyopo Mji wa Serikali Mtumba. Kulia ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mhandisi Kundo Mathew na kushoto ni Katibu Mkuu Dkt. Jim Yonazi
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew akizungumza mara baada ya mapokezi ya Waziri wake katika ofisi ya Wizara hiyo iliyopo katika mji wa Serikali Mtumba. Kushoto ni Waziri wake Mhe. Nape Nnauye
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi akizungumza wakati wa mapokezi ya Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Nape Nnauye (kulia) mara baada ya kuapishwa Ikulu ya Chamwino Dodoma kwa Waziri huyo, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Mohammed Khamis.

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew akisaini kitabu ofisini kwa Waziri wake Mhe. Nape Nnauye mara baada ya kuwasili Wizarani hapo


WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye amewasili katika Ofisi za Wizara hiyo zilizopo katika Mji wa Serikali Mtumba na kupokelewa na Menejimenti na watumishi wa Wizara hiyo wakiongozwa Naibu Waziri wake Mhandisi Kundo Mathew na Katibu Mkuu Dkt. Jim Yonazi mara baada ya kuapishwa Ikulu ya Chamwino leo tarehe 10.01.2022 baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe. Samia Suluhu Hassan  kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na watendaji wakuu Wizara katika ngazi ya Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu.


Mhe. Nape amezungumza na watumishi wa Wizara hiyo na kuwataka kufanya kazi kwa bidii, weledi na utulivu ili kuwezesha Sekta mbalimbali kupitia huduma za mawasiliano na TEHAMA pasipo urasimu na hatimaye nchi izidi kusonga mbele na Wizara yake iwe ni Wizara ya mfano katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi.


Ameongeza kuwa Mhe. Rais Samia amewapeleka katika Wizara hiyo kwa ajili ya kufanya kazi kwa kushirikiana na wataalamu wa Wizara hiyo kwa matokeo chanya na yeye yupo tayari kulinda haki za watumishi wa Wizara hiyo huku akiwasisitiza kufanya kazi kwa bidii na kutimiza wajibu


“Safari niliyopita imenifundisha kutambua haki za watu na kuwa mnyenyekevu, nitasifiwa nimefanya vizuri kama nyie mtafanya vizuri, na itakuwa hivyo kama mazingira yenu ya kazi yakiwa mazuri na kutimiza wajibu wenu kwa kiwango kinachohitajika”, Amezungumza Mhe. Nape


Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa viongozi waliopita walifanya kazi kubwa na kuifikisha Wizara mahali ilipo sasa na ana imani kubwa Wizara hiyo itaendelea kusonga mbele katika kuboresha, kuwezesha na kusimamia Sekta ya Habari, Mawasiliano na TEHAMA chini ya uongozi wa Waziri wake Mhe. Nape Nnauye, Katibu Mkuu Dkt. Jim Yonazi na Naibu Katibu Mkuu Mohammed Khamis.


Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa siku ya leo mara baada ya uapisho Viongozi wa Wizara hiyo wamekutana na Menejimenti na baadhi ya watumishi kwa lengo la kusalimiana na kufahamiana huku kikao rasmi cha Waziri huyo na watumishi wa Wizara kitaandaliwa na kufanyika kwa kadri itavyoonekana inafaa


Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mohammed Khamis amesema kuwa anamshukuru sana Mhe. Rais kwa kumteua na kumpatia fursa ya kuitumikia nchi yake kwa taaluma aliyosomea na kuahidi kuitendea haki.


Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imefanyiwa mabadiliko ya uongozi katika ngazi ya Waziri ambapo Mhe. Nape Nnauye ameteuliwa na kuapishwa kuongoza Wizara hiyo, Katibu Mkuu Dkt. Jim Yonazi ambaye awali alihudumu katika cheo cha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Naibu Katibu Mkuu Mohammed Khamis aliyeteuliwa na kuapishwa kuongoza Wizara hiyo huku Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhandisi Kundo Mathew ameteuliwa tena kuendelea katika nafasi hiyo.


Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad