HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 17 April 2019

NGOs ZATAKIWA KUJIKITA KATIKA MIRADI YENYE TIJA NA MASHIKO

Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini  bado hayajaonesha uwiano wa fedha zinazotumia na matokeo tarajiwa ya miradi mbalimbali zinazotekeleza kwani zimejielekeza zaidi katika kujenga uwezo na kutumia muda mwingi katika vikao badala ya miradi yenye tija.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema hayo katika hotuba yake wakati akifungua Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali leo Jijini Dodoma na kuyataka Mashirika hayo kuangalia miradi inayoleta matkeo chanya badala ya kutumia fedha nyingi katika kujengeana uwezo.

‘’Unakuta Mashirika mengine yanatoa matangazo ya kila dakika katika vyombo vya habari mfano kuhusu Afya ya Mama na Mtoto wakati unbakuta maeneo fulani ya Nchi wakina mama hawana vituo vya Afya, tumieni fedha izo kujenga vituo vya Afya badala ya kufanya vikao na miradi ya kujengeana uwezo’’ Alisema Waziri Mwalimu.

Aidha Waziri Mwalimu amezitaka NGOs kuzingatia misingi ya uwajibikaji na uwazi kama ilivyoanishwa katika Sheria ya NGOs pamoja na Kanuni zake lakini pia ameyataka Mashirika hayo kuhakikisha yanazi ngatia vipaumbele vya Serikali ili kutoa huduma muhimu katika  Maeneo yenye mahitaji.

Aidha Waziri Mwalimu ameitaka Bodi mpya ya Uratibu wa  NGOs itambue kuwa maamuzi watakayoyafanya kuwa ni  maamuzi ya Serikali na kuhakikisha pia wanatenda haki na kuzishughulikia NGOs zinazofanya kazi kinyume na Sheria ya NGOs na Kanuni zake lakini pia kukutana na wawakilishi wa NGOs na kujadiliana nao kuhusu masuala yao.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu ameitaka Bodi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutambua kuwa wanakazi kubwa ya kufanya kwa kuwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanatofautiana kiutendaji na mengine yanajihusisha katika mambo yasiyofaa kwa mujibu wa Sheria.

‘’NGOs nyingine zina fedha nyingi, nyingine zinajihusisha na utafiti, utoaji fedha lakini pia zipo ambazo zinajihusisha na vitendo vya ovyo kwahiyo mnakazi kubwa ya kufanya kwa kuwa mmeaminiwa na Taifa kupewa dhamana ya kusimamia NGOs hapa Nchini.’’Aliongeza Dkt. Jingu.

Dkt Jingu ameongeza kuwa Sekta ya NGOs ni Sekta kubwa na pana na muhimu kwa Taifa kwa kuwa inahusisha Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa na Mashirika haya ni takribani 8,310 na yanafanya kazi mbalimbali ikiwemo kufanya kampeni za kuleta mabadiliko.

Wakati huohuo  Mwakilishi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Kitaifa Bw. Ngunga Tepani amesema kwa sasa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanapatia changamoto nyingi sana zikiwemo za kisera na kiutekelezaji na hivyo kuiomba Bodi mpya kutoa huduma kwa mashirika hayo kwa kuyasimamia vema ili yaweza kuwa Sekta inayokua badala Sekta inayoanguka.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amezindua Bodi ya Nne ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kufuatia hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kumteua Dkt. Richard Faustine Sambaiga kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo na kuteuliwa kwa wajumbe wa Bodi.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akijadiliana jambo na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. John Jingu wakati wa uzinduzi wa Bodi Mpya ya Uratibu wa NGOs.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu Watoto akitoa hotuba yake wakati wa uzinduzi wa Bodi Mpya ya Uratibu wa NGOs.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. John Jingu akitoa hotuba yake wakati wa uzinduzi wa Bodi Mpya ya Uratibu wa NGOs.
  Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Neema Mwanga akitoa hotuba yake wakati wa uzinduzi wa Bodi Mpya ya Uratibu wa NGOs.
 Baadhi ya Wajumbe wa Bodi mpya ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na wadau wa NGOs wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa Bodi Mpya ya Uratibu wa NGOs.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wapya wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali mara baada ya uzinduzi wa Bodi hiyo. Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad