HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 17 April 2019

WAKUU WA IDARA WANAOFANYA KAZI KWA MAZOEA WAHAMISHWE VITUO VYA KAZI -RC MAKONDA


*Awataka madiwani Manispaa ya Ilala kuendana na kasi katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati

* Utendaji kazi wa RC Makonda katika sekta ya elimu wamvutia balozi wa nchi za kiarabu nchini atoa Milioni 20 kusaidia watoto wa kike katika sekta ya elimu

Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote jijini humo kuwahamisha kazi wakuu wote wa idara  wanaofanya kazi kwa mazoea hali inayopelekea kusuasua kwa kasi maendeleo inayoenda sasa.

Akizungumza katika kikao cha dharura cha baraza la madiwani  wa Manispaa ya Ilala  Makonda amesema kuwa baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wakikwamisha maendeleo, huku akieleza kuwa wakuu wa idara zote waliokwama kwenye idara zao watolewe Dar es Salaam na  kupelekwe Mikoani hadi kufikia mwezi June mwaka huu.

Amesema kuwa baadhi yao wamekuwa wakikwamisha shughuli za kimaendeleo pamoja na kutotoa ushirikiano kwa wakurugenzi wao na hata ubadilishwaji wa vituo vya kazi kwa wakuu wa idara hao umekuwa ni kutoka halmashauri moja kwenda nyingine hivyo ni vyema wakapelekwa katika Mikoa mingine ili kuboresha utendaji wao.

Kuhusiana na mradi wa ujenzi wa soko la kisutu Makonda amesema kuwa haoni sababu ya mradi huo kukwama huku fedha zikichezewa na kutumika kiholela na amefurahi baada ya  kuona leo   mradi huo umeanza kutekelezwa na hiyo ni baada ya kutoa maagizo ya siku tatu kwa Mkuu wa Wilaya na watendaji wake kushughulikia suala hilo.

Pia amesema kuwa kusuasua kwa mifereji na mto msimbazi hakufurahishi kwa kuwa watu wanapoteza maisha kunakosababishwa na mafuriko, amesema kuwa licha ya kuwepo kwa fedha lakini mradi huo bado hauridhishi na amewaagiza watendaji kufanya kazi usiku na mchana kwa kuwa Serikali tayari imetoa fedha ili kuboresha huduma kwa wananchi.

Vilevile amewataka madiwani hao kusimamia miradi ya kimkakati ipasavyo na kujenga tabia ya kuokoa fedha za wapiga kura.

Akitoa taarifa ya manispaa hiyo Naibu Meya wa Ilala OMari Kumbilamoto amesema kuwa makusanyo ya mapato yamefikia asilimia 70 huku akieleza kuwa zaidi ya bilioni moja zitatolewa kesho kwa makundi mbalimbali wakiwemo wajane, walemavu na wanawake.

Amesema kuwa takribani watoto 21 elfu wamerudi shule huku  madarasa mengi zaidi yakizidi kujengwa ili kutatua changamoto ya elimu na amemshukuru Rais Dkt. John Magufuli na Mkuu wa Mkoa Paul Makonda kwa kuendelea kuonesha ushirikiano katika kuleta maendeleo.

Wakati huo huo RC Makonda amepokea hundi ya shilingi milioni 20 kutoka kwa balozi wa  nchi za kiarabu nchini Balozi Khalifa Abdullahman al- Marzouqi  ambaye ametoa fedha hizo katika kuunga mkono juhudi za RC Makonda za kuwasomesha watoto wa kike  100 waliofaulu masomo ya sayansi na wanaoishi kwenye mazingira magumu kila mwaka.

Balozi Khalifa amesema kuwa utendaji kazi wa Makonda unavutia hasa kwa kuwagusa watu wenye mahitaji muhimu na amehaidi kuendelea kusaidia zaidi kwa siku za baadaye sambamba na kuboresha zaidi mahusiano ya nchi hizo mbili. Pia balozi huyo atafadhili ujenzi wa uwanja wa michezo (basketball) kwa ajili ya wanafunzi.
 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akizungumza na madiwani wa manispaa ya Ilala kwenye kikao cha dharura ambapo amewataka kuwa mstari wa mbele katika kusimamia miradi ya kimkakati jijini humo, leo jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda (kushoto) akiteta jambo na Balozi nchi za kiarabu nchini Khalifa Abdullahman al-marzouqi (kulia) mara baada ya balozi huyo kukabidhi hundi ya shilingi milioni 20 zitakazowasaidia watoto wa kike katika sekta ya elimu, leo jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad