Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi. Lekujan Manase pamoja na Wakurugenzi kutoka Idara ya Huduma za Ufundi na Umeme iliyo katika Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Dkt. William Nshama pamoja na Mhandisi Lazaro Vazuri wametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa kivuko kipya cha Pangani, pamoja na ukarabati wa kivuko cha magogoni katika eneo la bandari ya Dar es Salaam.
Wakikagua Mradi wa Ujenzi wa Kivuko kipya cha Pangani Mhandisi Lekujan Manase alisema; “Kivuko hiki kipo katika hatua za mwisho za ujenzi wake na leo tumekuja hapa kukagua mitambo ya kuendeshea kivuko (propulsion units) pamoja na engines zilizofungwa katika kivuko hiki ili kukamilisha ujenzi wake na hatimae kianze kufanya kazi”.
Mkandarasi Mkuu kutoka Songoro Marine Transport LTD (ambao ndio wajenzi wa kivuko hicho), alisema ujenzi wa kivuko hicho unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi huu wa saba na kwamba kivuko hicho kina uwezo wa kubeba magari sita na abiria 100 kwa pamoja, sawa na tani 50.
Nae Mhandisi Dkt. William Nshama alieleza kuwa ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa kivuko hicho unaofanywa kwa kiwango cha kimataifa na kuwa kivuko cha Pangani kinatarajiwa kutoa huduma kati ya Pangani na Bweni Mkoani Tanga baada ya ujenzi wake kukamilika.
Katika hatua nyingine Mtendaji Mkuu TEMESA na ujumbe wake wamekagua ukarabati wa kivuko cha Magogoni, ambao uko katika hatua za mwisho za ukarabati wake, kwani kwa sasa tayari mitambo ya kuendeshea kivuko pamoja na “engines” zinafungwa pamoja na kumalizia matengenezo ya milango yaani “ramps”. Ukarabati wa kivuko cha magogoni unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu wa saba. Kivuko cha Magogoni kinatoa huduma kati ya Magogoni na Kigamboni, Dar es Salaam.
Wakikagua mtambo wa kuendeshea kivuko (propulsion unit), kutoka Kushoto ni Mhandisi Lekujan Manase (Mtendaji Mkuu TEMESA), Major Songoro ( Mkurugenzi kutoka Songoro Marine Transport Ltd), Vitus Bujimu (Mwakilishi Kutoka Songoro Marine Transport Ltd), Mhandisi Lazaro Vazuri ( Mkurugenzi Msaidizi, Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Idara ya Huduma za Ufundi na Umeme), Mhandisi Japhet Maselle ( Mkurugenzi wa Huduma za Vivuko kutoka, TEMESA) pamoja na Mhandisi Dkt. William Nshama (Mkurugenzi,Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Idara ya Huduma za Ufundi na Umeme).
Kivuko kipya cha pangani katika hatua za kukamilishwa kwa ujenzi wake, unaofanyika katika eneo la bandari ya Dar es salaam.
Kivuko cha Magogoni katika hatua za kukamilishwa ukarabati wake. Kivuko hiki kinatoa huduma kati ya Magogoni na Kigamboni, Mkoani Dar es Salaam.
Sehemu ya juu ya Mlango wa kivuko cha Magogoni.
Sehemu ya chini ya mlango wa Kivuko cha Magogoni inayokuwa kwenye maji wakati wa uendeshaji wa kivuko. Kutoka kulia ni Major Songoro ( Mkurugenzi kutoka kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd inayokarabati kivuko hicho) akimuelezea jambo Mhandisi Dkt. William Nshama (Mkurugenzi Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Idara ya Huduma za Ufundi na Umeme) alie chuchumaa ni Mhandisi Japhet Maselle (Mkurugenzi wa Huduma za Vivuko kutoka TEMESA).
No comments:
Post a Comment