HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, January 26, 2016

Benki ya walimu yatahadharisha umma juu ya uzushi unaosambazwa mitandaoni

Uongozi wa Benki ya Walimu Tanzania (MCB) umekanusha vikali taarifa iliyotolewa katika mtandao wa ZOOM Tanzania na mitandao mingine ya kijamii ikidai kuwa benki hiyo iko katika mchakato wa kujaza nafasi 120 za ajira.

Taarifa hiyo iliyoanza kutolewa Ijumaa tarehe 22, 2016 inadai kuwa MCB imetafuta wataalamu washauri katika sekta ya benki wanaojulikana kama Quality Service Consultants kusimamia swala zima la ajira hizo na mafunzo katika muda wa miezi sita.

Imesema kuwa baada ya hapo, wale watakaofaulu wataajiriwa na benki hiyo na kuendelea na mafunzo kwa vitendo chini ya uangalizi wa wataalamu.

Pia taarifa hiyo iliyotolewa na mtu aliyejiita Christopher Mwakingwe ilidai kuwa benki hiyo inatafuta wazoefu na wenye bidii ambao wako tayari kufanyakazi katika mazingira shindani na kwenye matawi ya benki hiyo yanayoanzishwa nchini pote.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Afisa Mkuu Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Ronald Manongi alisema taarifa hiyo ni ya uongo na yenye lengo la kupotosha umma.

“Benki haijawahi kutoa tangazo kama hilo wala kutafuta mtaalam mshauri kufanya kazi hiyo kwa niaba yetu,” alisema Bw. Manongi.

Alitoa tahadhari kwa wananchi kutoomba kazi hizo kwani hazipo.

“Tunaitaka kampuni hiyo kukanusha taarifa hiyo kupitia mitandao waliyotumia ndani ya siku tatu kuanzia leo na kueleza chanzo cha taarifa hizo au wachukuliwe hatua za kisheria na benki,” alisema Bw. Manongi.

Benki hiyo pia imeitaka Quality Service Consultants kueleza ni mara ngapi wameshatoa taarifa kama hiyo siku za nyuma na watu wengine wanaoshirikiana nao kuchapisha taarifa za uongo zenye nia ya kupotosha umma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad