HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, October 3, 2023

PUMA ENERGY TANZANIA, AMEND WAZINDUA KAMPENI YA KUWA SALAMA BARABARANI


*Naibu Waziri Mambo ya Ndani atoa takwimu vifo vya ajali barabarani

Na Mwandishi Wetu

PUMA Energy Tanzania kwa kushirikiana na Amend Tanzania wamezindua kampeni ya kuleta mabadiliko ya usalama barabarani kwa lengo la kuboresha usalama wa watoto na vijana wawapo barabarani na kuwapeusha na majeraha na vifo vinavyotokana na ajali za barabarani.

 Akizungumza leo Oktoba 3,2023 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo iliyopewa jina la ‘Be Road Safe Africa’,Kamishna wa Jeshi la Polisi na Mkurugenzi Msaidizi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Idara ya Wakimbizi Nsato Mirajina aliyemwakilisha Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Jumanne Sajini aliyekuwa mgeni rasmi, amesema majeraha ya ajali za barabarani ndio chanzo kikuu cha vifo vya watoto na vijana kote ulimwenguni.

Huku akifafanua  Afrika ikiwa na viwango vya juu vya vifo vya barabarani na kwa mujibu wa takwimu za kikosi cha usalama barabarani cha Jeshi la Polisi nchini Tanzania  vifo 1,545 vinavyohusiana na barabara na majeruhi 2,278 vilivyoripotiwa kutokana na ajali 1,720 za barabarani kwa mwaka 2022 pekee. Watoto wanaotembea kwa miguu wakiwa hatarini zaidi.

Akieleza zaidi  kampeni hiyo amesema itafanyika katika shule tano za msingi  jijini Dar es Salaam katika maeneo yanayotajwa kuwa na mazingira hatarishi kwa ajali za barabarani zimechaguliwa kushiriki kampeni hiyo.Shule hizo ni Shule ya Msingi Kibugumo, Kifuru, Msewe, Kibasila na Shule ya Msingi Mtambani.

“Napenda kutoa pongezi za dhati kwa Puma Energy Tanzania kwa kuzindua kampeni hii na kwa juhudi zao katika kuborsha usalama wa watoto wa Tanzania barabarani.Aidha napenda kuhamasisha jamii nzima kushiriki katika kampeni za namna hii .

Ni wajibu wetu sote kuhakikisha watoto wetu wanapata elimu na mazingira salama wanaposafiri kwenda shule.

“Watoto ni hazina yetu, na tunawajibika kuhakikisha wanapata maisha bora na salama.Shughuli ya kampeni zitakazotekelezwa na Amend Tanzania zitawapa watoto wa shule za msingi maarifa na ujuzi muhimu wa usalama barabarani na kuwawezesha kufanya maamuzi salama barabarani.

“Shughuli hizo ni pamoja  na mashindano  ya kuchora na Mahakama ya Watoto ambayo huwawezesha watoto kuwawajibisha watu wazima kwa kuendesha gari kwa uzembe karibu na shule zao. Shughuli hii inawaunganisha Polisi , watoto, madereva na jamii nzima kwa njia iyoleta manufaa kwa wote,”amesema .

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania Fatma Abdallah amesema kila mtoto anastahili safari salama ya kwenda shule na na kurudi , hivyo kupitia mpango wa Be Road Safe Africa , Puma Energy pamoja na mshirika wake wa utekekelezaji Amend Tanzania, wadau wa usalama barabarani na jumuiya za mitaa imejitoa kutokomeza janga la majeraha ya barabarani.

“Tumejitolea kulinda watoto na vijana wa Tanzania.Kampeni hii inazingatia mpango wa usalama barabarani wenye mafanikio unaoungwa mkono na Puma Energy na kutekelezwa na Amend Tanzania kati ya mwaka 2013 na mwaka 2020.

Mpango huu uliwanufaisha zaidi ya watoto 130,000  katika shule zipatazo 115 nchini Tanzania katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Geita, Mbeya Mwanza, Ruvuma na Zanzibar.Tunajivunia kuendeleza urithi huu,”amesema Fatma Abdallah.

Aidha amesema eneo lenye idadi ya watoto wenye umri mdogo wengi na wenye kasi kubwa ya ongezeko la watu duniani, tabaka la kati linalokuwa na idadi inayoongezeka ya magari barabarani, idadi ya watu walioathiriwa na ajali za barabarani huenda ikaongezeka katika ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Hivyo mpango wa usalama barabarani wa Puma Energy unakusudia kuboresha usalama wa watoto wa kiafrika barabarani kwa sasa na kuwatayarisha kuwajibika kwa matumizi mazuri ya barabara katika siku zijazo.

“Usalama barabarani ni nguzo ya mkakati wa uwajibikaji kwa kampuni wa Puma Energy huku kampeni ya Be Road Safe ikiwa ni sehemu ya mpango mpana wa ‘Be Puma Safe’ unaojumuisha pia uweeshaji wa wananchi na vijana.”

Mwakilishi wa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sajini katika uzinduzi wa Programu ya elimu ya usalama barabarani ya ‘Be Road Safe Afrika’ inayotekelezwa na Kampuni ya Puma Energy Tanzania, Kamishna wa Polisi Nsato Marijani (wa nne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa uzinduzi huo uliofanyika leo Oktoba 3, jijini Dar es Salaam. 

Wengine ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Puma Energy Dk.Selemani Magige (wa sita), Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo Fatma Abdallah (mwenye ushungi), Kamishna Msaidizi wa Polisi na Mnadhimu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Pili Misungwi (wa kwanza kushoto), Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Amend Simon Kalolo (wa kwanza kulia), mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Swalehe Msechu (wa tatu kushoto)  pamoja na wanafunzi kutoka baadhi ya shule za msingi za mkoani Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad