HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, October 30, 2023

DIWANI BAKARI KIMWANGA AGAWA KOMPYUTA KILA TAWI AKITOA TAARIFA UTEKELEZAJI WA ILANI MAKURUMLA

 


Na Said Mwishehe, Michuzi TV

DIWANI wa Kata ya Makurumla wilayani Ubungo mkoani Dar es Salaam Bakari Kimwanga amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) huku akitumia nafasi hiyo kugawa kompyuta kwa ajili ya matumizi ya ofisi katika matawi yote ya CCM yaliyopo ndani ya Kata hiyo.

Aidha ametumia nafasi hiyo kumshukuru Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika Kata ya Makurumla ambazo zimewezeshwa kwa kutekelezwa kwa miradi ya maendeleo ikiwemo ya ujenzi wa miundombunu ya barabara, elimu, afya na ujenzi wa kingo katika mifereji ya mito.

Akizungumza wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani katika Mkutano Mkuu maalum wa Kata Kimwanga pamoja na mambo mengine ametumia nafasi hiyo kukabidhi kompyuta kwa ajili ya matumizi ya ofisi za Chama Cha Mapinduzi( CCM) na lengo kuu ni kuhakikisha taarifa za Chama zinachapishwa ndani ya kompyuta za ofisi kama sehemu ya kutunza kumbukumbu na siri za Chama.

"Katika siku hii maalum ya kutoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu katika Kata ya Makurumla , naomba pia nieleze kuwa nimenunua kompyuta ambazo nazitoa bure na kuzikabidhi kwa Ofisi za Chama za Kata yetu, "amesema Kimwanga baada ya Mkuu wa Wilaya Hashim Komba aliyekuwa mgeni rasmi kukabidhi kompyuta hizo kwa matawi hayo.

Kuhusu taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu, Kimwanga amemshukuru Dk.Samia Suluhu kwa uongozi wake shupavu na namna ambavyo kupitia Serikali yake ya Awamu ya Sita wana Makurumla wamemwagiwa fedha katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Pia amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Ubungo ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo ambaye muda wamekuwa bega kwa bega katika kuhakikisha wanahudumia wananchi wa kata hiyo.

“Ni wazi kwa maana ya mkutano maalum wa utekelezaji wa Ilani ni wa kwanza kufanyika kwa maana mara zote tumekuwa tukiishia katika halmashauri kuu Kata ya Makurumla lakini sasa chini ya viongozi mbalimbali tukiongozwa na Mwenyekiti wetu Idd Toatoa na kamati yake ya siasa nimeamua kutoa taarifa hii ili ifike kwa wananchi kwa urahisi zaidi.”

Aidha amefafanua Tanzania inatekeleza dira ya taifa ya maendeleo 2025,dira hiyo inalenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 watanzania waishi katika nchi ambayo imeendelea na yenye watu ambao wana kiwango cha juu cha ubora na maisha huku umasikini wa kutupwa likibaki kuwa historia.

Kupitia taarifa hiyo ameeleza kwa kina maendeleo ambayo yamepatikana katika Kata hiyo kupitia utekelezaji wa Ilani huku akielezea hali ya barabara katika kata hiyo.

Amesema TARURA na TANROADS ndio wamekuwa na jukumu la kuhudumia barabara hizo kwa mujibu wa sheria huku akifafanua wakati CCM wanachukua kijiti cha kuongoza Makurumla hali ya barabara zao za ndani ilikuwa katika hali mbaya.

“”Moja ya ahadi tuliyoahidi mbele ya wananchi mwaka 2020 ni kuhakikisha tunajenga barabara hizi.Kupitia TARURA tumefanikiwa kujenga barabara katika kata yetu na ujenzi unaendelea,”amesema.

Pia amesema kupitia mradi wa DMDP wamejenga mfereji mkubwa unatoka barabara kubwa ya Morogoro ,Mikumi Kisiwani mpaka Mburahati kwa kujenga kingo kwa gharama ya Sh.milioni 234.8 ikiwa ni pamoja na ulipaji fidia kwa nyumba ambazo zimeathirika kwa kubomolewa kupisha mto.

Pia kupitia Mfuko wa Jimbo walipata Sh.milioni Saba ambapo walifanikiwa kurudisha mawasiliano barabara ya Mloka wakati kwa upande wa eneo la daraja la Mwinyi hali ilikuwa mbaya lakini TARURA kupitia fedha za kila jimbo wamejenga barabara na mifereji ya maji kwa thamani ya Sh.milioni 120.

Akizungumzia mradi wa DMDP Kimwanga amesema mwaka huu wa fedha 2023/2024 wakazi wa kata hiyo wamefanikiwa kupata ujenzi wa mto China kwa kilometa 9 ambapo watajenga kingo zake na kusaidia kupunguza hali ya mafuriko ambayo yanawakabili wakazi waliopo kando mwa mto huo.

Aidha amezungumzia mafanikio lukuki katika sekta ya elimu na afya katika kata hiyo akitolea mfano katika elimu Shule ya Msingi Dk.Omari imepata Sh.milioni 40 na kukarabati vyumba nane vya madarasa ambayo sasa yamekamilika na yanatumika.

Amesema Shule ya Msingi Karume wamepata Sh.milioni 120 ambapo pia wamefanikiwa kujenga vyumba sita vipya vya madarasa wakati Shule ya Msingi Mianzini wamekarabati vyumba vitatu vya madarasa kupitia mapato ya ndani.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Hashim Komba amesema amepata nafasi ya kuwa Mkuu wa Wilaya Iringa Mjini, Wilaya ya Nachingwea na sasa Wilaya ya Ubungo lakini hajawahi kuona Diwani anatoa kompyuta kwa ajili ya kukiwezesha Chama lakini Kimwanga ameweza na amekuwa mfano wa kuigwa.

"Nilikuwa Wilaya ya Iringa ambako kule tuna wilaya mbili za kichama Iringa Mjini na Iringa Vijijini , nimekwenda kuhudumu Nachingwe na sasa niko Wilaya ya Ubungo lakini katika maeneo yote hayo leo ndio nimemuona diwani wa kwanza ananunua kompyuta anapeleka katika matawi ya Chama Cha Mapinduzi.

" Kimwanga umefanya jambo kubwa kweli kweli, wajibu sasa tulionao ni kuhakikisha makatibu wote wa tawi watafutiwe mtaalam wa kompyuta wapate mafunzo ya kompyuta na baada ya hapo tuanze kutafakari kununua printa ili iwe ni rahisi kuandika na kutoa,tunataka Kata ya Makurumla iwe mfano, "amesema Komba.

Kuhusu taarifa ya utekelezaji wa Ilani Kata ya Makurumla, Mkuu wa Wilaya Komba amesema anakubaliana na yote yaliyoelezwa katika taarifa hiyo na kwamba wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2020 vyama vya siasa vilipita kwa wananchi kunadi sera zao na watanzania wakaichagua CCM.

" Leo hii tunaye Rais shupavu , hodari , makini Dk.Samia ambaye hayumbishwi maneno kidogo vitendo zaidi .Katika ngazi ya ubunge Ubungo tunaye Profesa Kitila Mkumbo. Ngazi ya udiwani Kata ya Makurumla tunaye Bakari Kimwanga anayo miaka yake mitano anaangalia Ilani inasema nini ngazi ya mitaa tunao viongozi wetu wa mitaa nao wameibeba ilani

"Ilani yetu inazungumza barabara, afya ,maji, elimu na huduma nyingine za kijamii.Niwaambie wana CCM kwa niliyoyasoma katika utekelezaji wa Ilani hii iliyowasilishwa na diwani wa kata ya Makurumla yote ni sahihi, hivyo Wana Makurumla tembeeni kifua mbele.

Aidha amesema kuna mambo mengi yamefanyika na mengine yanaendelea na yapo hatua mbalimbali za utekelezaji, huku akieleza mdari wa DMDP umeleta matunda makubwa kwenye mto ng’ombe kwani wakazi wa eneo hilo walikuwa wanapata adha ya mafuriko lakini sasa wameshasahau mafuriko.

"Mto China ndani ya wilaya yetu ya Ubungo sio hadithi sio historia kama ilivyosomwa katika taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi tayari mhandisi mshauri ameshapatikana na ameshaingia saiti na mwenyezi Mungu azidi kumjalia afya njema Rais Dk.Samia Suluhu Hassan mapema mwakani mwaka 2024 mtawaona wakandarasi wakiwa bize na ujenzi wa mto huu,

"Hakuna jambo ambalo Diwani amelizungumza halitafanyika ,nikiwa misimamizi wa shughuli za Serikali katika wilaya hii nina hakika yanayokuja yatawafurahisha kila wana Makurumla waliko katika maeneo yetu, " amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam Hashim Komba akizungumza wakati wa Mkutano Maalum wa Kata ya Makurumla ambapo Diwani wa Kata ya Makurumla Bakari Kimwanga alikuwa akitoa taarifa ya  utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu katika kata hiyo.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad