HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, October 31, 2023

CPC WAWEZESHA VIJANA 50 KUPATA MAFUNZO SHULE YA UONGOZI YA MWALIMU NYERERE KIBAHA

Naibu Katibu Mkuu CCM  bara Anamringi Macha  akizungumza  na washiriki  wakati alipokua mgeni  rasmi kwenye ufunguzi wa mafunzo ya siku kumi  Uongozi  hao  yaliyodhaminiwa  na  Chama Cha Kikomunisti Cha China kwa vijana 50 yanayofanyika katika  Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kwa Mfipa Wilayani Kibaha Mkoani Pwani  leo Oktoba 30,2023.

Na Khadija Kalili, Michuzi Tv
CHAMA Cha Kikomunisti cha nchini China (CPC), kimetoa ufadhili wa mafunzo mafupi ya siku kumi kwa wanachama 50 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka Umoja wa Vijana na UWT ambao wamechaguliwa kote nchini lengo likiwa ni kuwajengea uwezo masuala ya Siasa, uchumi na mkakati wa kuendeleza mahusiano kati ya nchi ya China na Tanzania.

Hayo yamesemwa wakati akifungua mafunzo hayo Naibu Katibu Mkuu CCM bara CDE Anamringi Macha katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kibaha Mkoani Pwani leo Oktoba 30,2023.

CDE Anamringi amesema kuwa mafunzo haya ni mahsusi kwa ajili ya kuwajengea uwezo Viongozi ili na wao waweze kwenda kutoa elimu ya mafunzo watakayo yapata baada ya kuhitimu.

Macha amesema kuwa viongozi hao watapata fursa ya kupewa mafunzo hayo kupitia wawezeshaji ambao pia ni Viongozi Wasomi wabobezi na wanazuoni pia ni viongozi wakongwe katika historia ya nchi kwa kufanya kazi kwa miaka mingi serikalini ili wawafundishe viongozi hao uvumilivu katika kulitumikia taifa.

Amewataja baadhi ya Wawezeshaji hao kuwa ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa na Katibu Mkuu kwa kipindi cha miaka kumi,pia alikua Mkuu wa Chuo Cha CCM Kivukoni Mzee Philip Mangula, Komredi Stephen Wassira, alikuwa Naibu Katibu Mkuu Visiwani Abdallah Mabodi, Prof. Samuel Wangwe , Prof. Paramagamba Kabudi.

Aidha katika mafunzo haya wakufunzi kutoka CPC ambao ni Jiang Wen,Wang Yao na Tan Xin watatoa mada ya mahusiano ya nchi mbili hizi katika sekta ya uongozi, kibiashara, mahusiano na ushirikiano wa China kiuchumi, na siasa ili waweze kuiva na kuwa mabalozi katika kizazi hiki na kijacho.

"Tutawafundisha mbinu kwa nini CPC wameweza kudumu na kuwa chama kikongwe kilichodumu madarakani kwa miaka 100 tangu kilipoanzishwa" amesema Macha.

Aidha amesema kuwa Viongozi hao watafundishwa masuala ya maendeleo, mafanikio ya nchi ya China kwa sasa na mikakati iliyopo kuelekea miaka ijayo.

Ameongeza kuwa CCM kimewakusanya viongozi hao wa UVCCM na UWT ili kuendelea kuwafunda vijana wake ili watambue kuwa wana wajibu nini cha kufanya kwa Taifa lao badala ya kuendelea kutegemea taifa liwafanyie kitu gani.

"Moja ya matatizo makubwa kwa vijana wetu sasa hivi wanakosa uvumilivu wanaingia katika maeneo wakitaka mambo yabadilike kwa haraka yakiwahusu wao kwahiyo tunapowaweka hapa tunawafunda na kuwaeleza umuhimu wa uongozi" amesema

Aidha amesisitiza kuwa viongozi wataendelea kuwaweka vijana kwenye nafasi za uongozi na kwamba mabadiliko ya nafasi yanapotokea ni kutaka kuona nani anafaa kwenye nafasi hiyo hasa katika utendaji na kuleta maendeleo.

Hatahivyo Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM bara ameonya tabia ya baadhi ya viongozi vijana kulewa madaraka na badala yake wametakiwa kufanyakazi kwa kuzingatia weledi.

Amesema baadhi ya viongozi vijana wa sasa wengi wamekuwa hawana uvumilivu na kwamba baadhi ya nafasi za uongozi walizonazo wamekuwa wakizitunia vibaya na kwamba CCM haita sita kuwaondoa na kuwachukulia hatua.

"Lazima tuwe wakweli tatizo tulilonalo sasa hivi vijana wanakosa uvumilivu wanaingia kwenye uongozi na kutaka mambo kubalika Kwa haraka huku wengine wanalewa madaraka badala ya kutumia nafasi kwa kufanya kazi iliyokusudiwa na kuanza kufanya vitu kinyume na inavyotakiwa, mtu huyo hatuwezi kumuacha tutamuondoa mara moja" amesema

Aidha Macha amesema lengo la Chama Cha Mapinduzi ni kuwalea vijana na kuwa viongozi bora na kwamba mafunzo hayo yanalengo la kuwafunda kiungozi na wanawajibu wa kulifanyia taifa mambo makubwa.

Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji wa Baraza la Umoja wa Wanawake Taifa (UWT), Mariamu Ulega amemshukuru Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha hayo mafunzo "hii ni fursa kubwa kwa wanawake kwa sababu ukimuelimisha mwanamke umeielimisha jamii nzima" hivyo elimu hii tutakayoipata tutakwenda kuipeleka kwa jamii hususani katika ziara mbalimbali ambazo zinafanywa UWT" amesema.

"Kama sasa hivi kumekua na ziara zinazoendelea kupitia Mwenyekiti wa UWT Taifa Mary Chatanda ambapo wanapita kufanya mikutano mbalimbali katika ngazi za Kata, Vijiji na Mkoa.

Akizungumzia kuhusu chaguzi za serikali za mitaa mwakani amesema Ulega amesema kuwa wanawake wajitokeze kuchukua fomu za kugombea huku ametoa wito kwa wanawake wengine kuwasapoti kuwasaidia ili waweze kushinda" amesema Mariamu.

Mariamu amewakumbusha wananchi kujitokeza kwenye mikutano mbalimbali ya chaguzi zijazo na kusikiliza sera za chama na kukipa nafasi zaidi CCM.

Naye mshiriki wa mafunzo hayo Mhandisi Fatma Rembo amesema kuwa anategemea kuwa baada ya kupata mafunzo haya wanatarajia kuja kuwa viongozi bora zaidi kwa kuliongoza taifa.

Wakufunzi kutoka Chama Cha Kikomunisti Cha China (CPC) Jiang Wen,Wang Yao na Tan Xin wakifuatilia ufunguzi  wa mafunzo  ya viongozi hao.
Mjumbe  wa Kamati ya Utekelezaji  wa Baraza UWT Mariam Ulega, akizungumza  na waandishi wa habari katika ufunguzi wa mafunzo ya siku kumi ya Uongozi yaliyodhaminiwa  na  Chama Cha Kikomunisti Cha China kwa vijana 50 yanayofanyika katika  Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kwa Mfipa Wilayani Kibaha Mkoani Pwani  leo Oktoba 30,2023.
Mhandisi  Fatma  Rembo ambaye pia ni mshiriki  wa mafunzo, akizungumza  na waandishi wa habari katika ufunguzi wa mafunzo ya siku kumi ya Uongozi yaliyodhaminiwa  na  Chama Cha Kikomunisti Cha China kwa vijana 50 yanayofanyika katika  Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kwa Mfipa Wilayani Kibaha Mkoani Pwani  leo Oktoba 30,2023.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad