VIFO VICHACHE MANYARA VILICHANGIA WENGI KUTOSHIRIKI CHANJO YA UVIKO-19 - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, July 9, 2022

VIFO VICHACHE MANYARA VILICHANGIA WENGI KUTOSHIRIKI CHANJO YA UVIKO-19

 

Joseph Lyimo

IMEELEZWA kuwa vifo vichache vilivyotokea mwaka jana kutokana na maambukizi ya UVIKO-19 vilivyangia kuwa na mwamko mdogo kwa wananchi wa Mkoa wa Manyara kushiriki kupata chanjo ya ugonjwa huo.

Baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Manyara, wanadai kuwa watu wengi hawakupata maambukizi na waliopata hawakufariki kutokana na maambukizi ya UVIKO-19 hivyo kusababisha mwamko wa kuchanja kuwa mdogo.

Kutokana na hali hiyo watu 30,000 walijitokeza kwenye Mkoa wa Manyara, kwenye kupata chanjo, idadi ambayo ni sawa na asilimia 3.7 tu ya lengo la wananchi 135,000 waliotarajiwa.

Mkazi wa kata ya Nangara mjini Babati, Husna Ombay anaeleza kuwa wananchi wa mji huo hawakushiriki ipasavyo kutokana na vifo vichache vilivyotokea.

“Hata hivyo hapa Babati kulitokea vifo vilivyosababishwa na changamoto ya kupumua na kufanya watu waende wakapate chanjo ya UVIKO-19 kwenye hospitali ya mji, vituo vya afya na zahanati.

Anasema baada ya kuona vifo vinavyohisiwa vimetokana na UVIKO-19 na watu wanasafirishwa kwenda kuzikwa makwao, wananchi wakawa na hamasa ya kuchanja ila awali hawakushiriki kutokana na kutokuwepo kwa vifo hivyo.

“Wananchi wa mikoa ya jirani ya Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha, pamoja na maeneo mengine ikiwemo jijini Dar es salaam, watu wake walijitokeza kuchanja kwa wingi kutokana na vyombo vya habari kuonyesha vifo vinavyotokea maeneo hayo,” anaeleza Ombay.

Mkazi wa mji mdogo wa Katesh wilayani Hanang’ John Gapchojiga, anasema kuwa watu wengi hawakuwa na hofu ya kupata maambukizi ya UVIKO-19 kutokana na kuona uchache wa watu wanaokufa au kupata maambukizi.

“Mwitikio haukuwa mkubwa kutokana na vifo vichache, wewe unadhani watu wangekuwa wanakufa wengi nani angebaki kwenye kuchanga si kila mtu angekimbilia kwenye chanjo? Amehoji Gapchojiga.

Mkazi wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro, Japhary Matimbwa anasema kwenye mji huo watu wengi walishiriki kupata chanjo baada ya kupata elimu kwenye vyombo vya habari na kwa wataalam wa afya.

“Hata Mirerani kuna mwingiliano wa watu kutokana na kuwepo kwa uchimbaji wa madini ya Tanzanite, hivyo wengi walishiriki japokuwa wapingaji hawakosekani kwenye shughuli yoyote ile,” anasema Matimbwa.

Mkuu wa mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere hivi karibuni akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, anakiri wananchi wa mkoa huo kutoshiriki ipasavyo kwenye chanjo ya UVIKO-19 kwa kipindi kilichopita kutokana na kutokea vifo vichache.

Hata hivyo, Makongoro anasema kuwa hivi wamejipanga kuhakikisha wananchi wengi zaidi wa mkoa huo wanapatiwa chanjo kwani wataendelesha zoezi hilo kwa kutoa elimu na kuchanja nyumba hadi nyumba ili kuondokana na athari ya awali ya mwamko kuwa mdogo kwenye kuchanja.

“Wataalamu wa afya wanatueleza kuwa maambukizi ya UVIKO-19 bado yapo, hivyo wananchi kwa umoja wetu tushiriki kwa wingi kupata chanjo kwani tukichanja na kasha kupata maambukizi hayo hatutapata athari kubwa endapo hatuna chanjo,” anaeleza RC Makongoro.

Anasema kuwa ameshazungumza na viongozi wa wilaya kuanza wakuu wa wilaya, wakurugenzi, wenyeviti wa halmashauri, wabunge, madiwani na wataalamu wa afya kuhakikisha kuwa zoezi la chanjo ya UVIKO-19 linafanyika ipasavyo.

Kwa upande wake, mganga mkuu wa mkoa wa Manyara, (RMO) Dkt Damas Kayera amekiri kuwa wananchi wa mkoa huo walikuwa na mwamko mdogo wa kupata chanjo baada ya kuona maambukizi na vifo vichache vimetokea eneo hilo.

Hata hivyo, RMO Dkt Kayera anasema kuwa hivi sasa wananchi wa Manyara, wamepata mwamko mpya kwani wameshiriki mno katika kupatiwa chanjo ya UVIKO-19 tofauti na awali.

Anasema hadi hivi sasa watu 135,000 wa mkoa huo wameshapatiwa chanjo ya UVIKO-19 na wanatarajia lengo la wananchi 669,516 wanaotarajia kupatiwa chanjo watafikiwa.

“Tupo sehemu nzuri kwani hadi hivi sasa tumefikia asilimia 30 kutoka asiliamia 3.7 japokuwa lengo ni kufikia asilimia 40 hadi mwishoni mwa mwezi Julai na kufikia asilimia 70 mwezi Desemba mwaka huu,” anasema Dkt Kayera.

Meneja wa mpango wa chanjo wa Taifa wa Wizara ya Afya Dkt Florian Tinuga anasema hadi sasa mkoa wa Ruvuma ndiyo unaoongoza kitaifa kwa kufikia asilimia 40 ya uchanjaji.

Dkt Tinuga anaeleza kwamba lengo la kitaifa ni kuhakikisha kuwa wanafikia lengo la kufikia asilimia 70 ya kutoa chanjo dhidi ya UVIKO -19 ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad