HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, July 9, 2022

MTENDAJI MKUU MAHAKAMA ATOA WITO KWA WANANCHI KUANDIKA WOSIA


Na Mary Gwera, Mahakama

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ametoa wito kwa wananchi hususani wanaume kuandika wosia ili kuepusha migogoro mbalimbali ikiwemo ya kugombea mali kwa familia wanazoziacha.

Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijni Dar es Salaam  tarehe 08 Julai, 2022 alipotembelea banda la Mahakama ya Tanzania lililopo katika Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ‘Sabasaba’, Prof. Ole Gabriel amesema kuwa familia nyingi hususani wajane na watoto wamekuwa wakikabiliana na migogoro ya kugombea mali zilizoachwa na marehemu.

“Wajane wengi wanakabiliwa na migogoro kutoka kwa ndugu pindi mume anapofariki, hivyo ni rai yangu kwa Watanzania na haswa wanaume wenzangu kuandika wosia ili kuepusha matatizo yanayotokea kwa mjane na Watoto,” amesema Prof. Ole Gabriel.

Mtendaji Mkuu ameongeza kuwa katika jitihada za kuhakikisha kuwa Mahakama inashughulikia kwa ukaribu masuala ya familia ikiwemo Mirathi, Mahakama ilianzisha kituo maalum cha kushughulikia masuala ya familia hivyo kuwataka wananchi kutosita kupata huduma zinazotolewa katika kituo hicho.

Aidha; Mtendaji Mkuu amesema katika kipindi cha Maonesho ya ‘sabasaba’ moja ya huduma zinazotolewa katika banda la Mahakama ni pamoja na kutoa elimu ya Wosia na Mirathi hivyo ni vyema wananchi watembelee banda hilo ili kujua zaidi.

Kwa upande mwingine, Mtendaji Mkuu huyo amewakumbusha wananchi kuendelea kutumia namba ya huduma kwa mteja ya Mahakama ‘Call Centre’ ambayo ni 0752 500 400 ili kupata utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazowasibu kuhusu Mahakama.

“Tumeanzisha hii ‘call centre’ maalum kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, unapokutana changamoto yoyote usimpigie Jaji Mkuu au Jaji Kiongozi au Msajili Mkuu bali piga namba 0752 500 400 inayopatikana masaa 24,” amesema Mtendaji Mkuu.

Mahakama ya Tanzania ni moja ya Taasisi zinazoshiriki katika Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa lengo ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu taratibu na huduma inazotoa.
 Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akimsikiliza Bw. Daniel Msangi, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Kitengo cha Maboresho Mahakama ya Tanzania alipokuwa akitoa elimu kwa Mtendaji huyo wakati alipotembelea banda la Mahakama ya Tanzania linalotoa huduma katika Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa 'Sabasaba' 2022. Prof. Ole Gabriel ametembelea banda hilo na mengine kadhaa alipotembelea maonesho hayo mapema  tarehe 08 Julai, 2022.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisaini kitabu cha wageni wakati alipowasili katika Ofisi ya 'TANTRADE'  tarehe 08 Julai, 2022.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akipata maelezo kuhusu Mahakama Inayotembea 'Mobile Court' kutoka kwa Hakimu anayehudumia katika Mahakama hiyo Mhe. Consolatha Kavishe. Mahakama hiyo inatoa huduma katika Moanesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa 'Sabasaba' 2022.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisaini kitabu cha wageni katika banda la Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi alipotembelea banda hilo lililopo ndani ya banda la Mahakama ya Tanzania katika Maonesho ya 'Sabasaba' 2022.
Maelezo kutoka kwa Kiongozi Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja 'Call Centre' Bi. Evetha Mboya (kulia). Kulia kwa Bi. Evetha ni Mhe. Charles Mrema, Hakimu Mkazi Mwandamizi anayehudumu katika kituo hicho pia.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad