HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, June 3, 2022

MKEMIA MKUU ASISITIZA MATUMIZI SALAMA YA MAABARA ZA MASHULENI

Kaimu Mkemia Mkuu wa Serikali, Sabanitho Mtega akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao na Maafisa Elimu Sekondari na Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari katika kuwajengea uwezo katika kusimamia maabara za kemia na kemikali. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Ofisi za Hazina jijini Dar es Salaam.Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Daniel Ndiyo akielezea majukumu ya Mamlaka kwa Maafisa Elimu Sekondari na Wakuu wa Shule za Sekondari kwenye Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi za Hazina jijini Dar es Salaam.


Na Mwandishi wa GCLA
MAAFISA Elimu Sekondari na Wakuu wa Shule za Sekondari nchini wamesisitizwa kusimamia vyema maabara za kemia na kemikali na kuhakikisha maabara hizo zinakidhi vigezo ambavyo sheria inataka.

Rai hiyo imetolewa na Kaimu Mkemia Mkuu wa Serikali, Sabanitho Mtega wakati akifungua kikao cha Maafisa Elimu Sekondari na Wakuu wa Shule za Sekondari wa mkoa wa Dar es Salaam kilichoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na kufanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa Hazina Jijini Dar es Salaam.

“Baada ya kikao hiki, naamini mtaenda kuyatekeleza yote yaliyojadiliwa hapa pamoja na kuibua changamoto ambazo zitajitokeza lakini pia kuangalia namna bora ya kukabiliana nazo,” alieleza Mtega.

Aidha, Mtega aliwashauri wataalamu, walimu na wanafunzi wanaotumia maabara za kemia na kemikali kufanya kazi kwa kutumia vifaa maalum vilivyoainishwa ili kuhakikisha wanalinda afya zao na afya ya jamii pamoja na kufuata sheria na kanuni za matumizi salama ya kemikali.

“Unapotumia kemikali unapaswa kufahamu aina za kemikali na madhara yake kwa sababu kemikali nyingine zina madhara makubwa kwa afya ya binadamu na mazingira na nyingine zimefutwa kutokana na Mikataba ya Kimataifa”. alisisitiza Mtega.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Kenton ya Jijini Dar es Salaam, Abdullah Kashogi aliipongeza Mamlaka kwa kutoa mafunzo hayo yenye maelekezo muhimu ya kuzingatia matumizi sahihi na salama ya maabara za shuleni.

“Semina hii imetupatia faida kubwa kwa sababu shule nyingi za Sekondari zina maabara ambazo zinatumiwa na walimu na wanafunzi hivyo maelekezo yaliyotolewa na wataalamu wa GCLA yametupa faraja na upeo wa kuweza kujua kwamba wanafunzi wetu na walimu wao wanaweza kujilinda vipi na madhara ya kemikali wakiwa maabara.” Alisema Kashogi.

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) ina utaratibu wa kutoa mafunzo kwa wadau mbalimbali wanaotumia kemikali wakiwemo wanafunzi ili kuhakikisha Mamlaka hiyo inatimiza matakwa ya kisheria ya kulinda afya za watu na mazingira.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad