HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, June 2, 2022

MAKAMU WA RAIS AHUTUBIA MKUTANO WA UN SWEDEN

 

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango leo tarehe 2 Juni 2022 ameshiriki mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Stockholm +50 unaoendelea nchini Sweden. Katika mkutano huo, viongozi kutoka mataifa mbalimbali duniani pamoja na wawakilishi wa jumuiya za kimataifa wametoa ahadi pamoja na mapendekezo mbalimbali ya namna ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira duniani.

Akizungumza katika mkutano huo, Makamu wa Rais Dkt. Mpango amesema ili kuhakikisha dunia inakua salama kwa viumbe wote wanaoishi, hakuna budi kutekeleza kikamilifu makubaliano mbalimbali ya kimataifa ya kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira yaliofanyika maeneo mbalimbali duniani kama vile Rio de Jeneiro, Paris, Kyoto pamoja na Glasgow. Amesema kinachohitajika ni utayari wa kisiasa pamoja na jitihada za pamoja katika kukabiliana na changamoto hizo ambazo zinasababishwa na shughuli za binadamu.

Aidha Makamu wa Rais amesema Tanzania imefanya jitihada mbalimbali katika kupambana na uharibifu wa mazingira ikiwemo kulinda misitu ya asili pamoja na juhudi za kitaifa za upandaji miti huku ikienda sambamba na kuhifadhi kilometa za mraba 307,800 ambazo ni sawa na asilimia 32.5 ya eneo lote la nchi kwaajili ya Hifadhi za Taifa pamoja na misitu.

Makamu wa Rais amewakaribisha wawekezaji kuwekeza nchini Tanzania katika teknolojia rafiki kwa mazingira ikiwemo teknolojia zinazoweza kubadili taka kuwa nishati ya gesi na mbolea. Pia amawaalika watafiti kutoka mataifa yalioendelea kushirikiana na makampuni pamoja na watafiti wa ndani nchini Tanzania kwa kuendeleza teknolojia rahisi na rafiki kwa mazingira katika kutumia nishati ya jua na upepo iliopo nchini Tanzania.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema pamoja na Tanzania kuchukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira bado suala hilo lipaswa kupewa kipaumbele na mataifa yote kwani juhudi za Tanzania pekee hazitoweza kukabiliana na changamoto hiyo duniani.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali waliohudhuria ufunguzi wa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Stockholm +50 unaoendelea mjini Stockholm nchini Sweden leo tarehe 2 Juni 2022.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akihutubia katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Stockholm +50 unaoendelea mjini Stockholm nchini Sweden leo tarehe 2 Juni 2022.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akishiriki mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Stockholm +50 unaoendelea mjini Stockholm nchini Sweden leo tarehe 2 Juni 2022.





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad