HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, June 29, 2022

BENKI YA CRDB YATOA GAWIO LA SHILINGI BILIONI 36.1 KWA SERIKALI

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay (wa tatu kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wa pili kushoto) wakikabidhi mfano wa hundi kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba (katikati) ikiwa ni sehemu Gawio la Serikali lililotolewa na Benki ya CRDB, katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma leo Juni 29, 2022. Wengine pichani ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais - Tamisemi, David Silinde (wa pili kulia), Naibu Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana, Patrobas Katambi (kulia) pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru.
Dodoma, 29 Juni, 2022 - Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba amepokea gawio la shilingi bilioni 36.1 linalotokana na uwekezaji wa Serikali ndani ya Benki ya CRDB kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay. 
 
Makabidhiano hayo ya hundi kifani yalifanyika katika Ofisi za Wizara ya Fedha Dodoma na kuhudhuriwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mheshimiwa, David Silinde, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Vijana, Patrobas Katambi, na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Fedha, Taasisi na Mashirika ya umma yenye hisa ndani ya Benki ya CRDB, pamoja na Bodi, Menejementi na wafanyakazi wa Benki ya CRDB.

Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Fedha aliipongeza Benki hiyo kwa kutoa gawio kwa Serikali, Dkt. Nchemba aliipongeza Benki ya CRDB kwa kupata matokeo mazuri ya fedha mwaka 2021 ambayo yamepelekea kuongezeka kwa gawio kwa wanahisa ikiwamo Serikali.
 
“Ongezeko hili la gawio ni kiashiria tosha kwa Serikali kuwa Benki yetu ya CRDB inazidi kuimarika zaidi kutokana na mikakati madhubuti ya kibiashara iliyojiwekea na jambo linalowapa moyo Watanzania na wawekezaji kuwa benki inatoa huduma bora katika jamii”, alisema Dkt. Nchemba.

Dkt. Nchemba alisema fedha zilizopatikana kupitia gawio hilo zitakwenda kusaidia utekelezaji wa miradi ambayo Serikali imeianisha katika vipaumbele vya bajeti ya mwaka 2022/2023. “Kipekee kabisa niipongeze Bodi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Benki ya CRDB kwa kazi nzuri mnayoifanya,” aliongezea Dkt. Nchemba.

Aliipongeza Benki ya CRDB kwa matokeo mazuri ya fedha iliyopata katika nusu ya kwanza ya mwaka huu 2020 ambapo faida ya Benki imeongezeka kwa asilimia 111 kufikia shilingi bilioni 90 kutoka shilingi bilioni 43 zilizoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2021. “Mkiendelea na kasi hii mwakani tunategemea kupata gawio nono zaidi,” alisema Dkt. Nchemba.
 Dkt. Nchemba alizitaka taasisi nyengine kuiga mfano wa Benki ya CRDB katika kuleta faida kwa Serikali na Wanahisa kutokana na Uwekezaji. Alizitaka Taasisi na Mashirika yote ambayo Serikali inahisa kuweka mikakati madhubuti itakayoleta tija, huku akiwataka viongozi wake kutjitathmini kiutendaji.
 
Akizungumzia umuhimu wa ushiriki wa taasisi za fedha katika maendeleo ya taifa, Dkt. Nchemba aliipongeza Benki ya CRDB kwa kupunguza riba katika mikopo ya kilimo na wafanyakazi. “Kiwango cha riba cha tarakimu moja katika mikopo ya kilimo kufikia asilimia 9 kutoka asilimia 20 iliyokuwa ikitozwa hapo awali ni cha kihistoria, hongereni sana,” alisema.

Aidha, aliipongeza Benki kwa kutenga fedha kwa ajili ya uwezeshaji kwa kundi la wajasiriamali nchini kwa ajili ya kuwasaidia kuondokana na changamoto zilizotokana na janga la UVIKO-19. Kwa upande wa sekta ya kilimo alibainisha mkataba ambao benki hiyo imeingia na Shirika la Umoja wa Mataifa la GCF kuwezesha kilimo cha kisasa kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi utasaidia kuleta mapinduzi makubwa katika sekta hiyo nchini.
 Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema kuwa gawio hilo ni sehemu ya faida ya shilingi bilioni 268.2 baada ya kodi ambayo Benki hiyo imeipata katika mwaka wa fedha 2021. Pia ameeleza kuwa Benki hiyo itaendelea kutoa huduma bora ili kukidhi mahitaji ya wanahisa wake na wananchi kwa ujumla.
 
“Katika Mkutano wa Wanahisa uliofanyika kidijitali mwezi Juni mwaka huu, Wanahisa wa Benki ya CRDB walipitisha kwa pamoja gawio la shilingi 36 kwa hisa ikiwa ni ongezeko la asilimia 64 na hivyo kufanya gawio la mwaka huu kufikia shilingi bilioni 94,” aliongezea Nsekela.
 
Nsekela alimhakikishia Dkt. Nchemba kuwa Benki ya CRDB kupitia kauli mbiu yake ya “Tupo Tayari” itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha nchini huku akielezea kuwa benki hiyo sasa hivi imejikita zaidi kwenye uwekezaji wa mifumo ya kidijitali ya kutolea huduma kama CRDB Wakala, SimBanking, na Internet banking kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Pamoja na kukabidhi gawio kwa Serikali kuu kupitia mfuko wa uwekezaji wa DANIDA, Benki ya CRDB pia imekabidhi gawio kwa taasisi na mashirika mbalimbali ya Serikali ikiwamo PSSSF, NSSF, ZSSF, NHIF, Local Government Loans Board, Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU), Umoja Unit Trust Scheme, pamoja na halmashauri Mbinga, Shinyanga, Mufindi, Chunya na Rungwe.

Akipokea gawio kutokana na uwekezaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vina na Walemavu, Mheshimiwa Patrobas Katambi alizihimiza taasisi nyegine za umma nchini kuwekeza katika hisa ili kupanua wigo wa mapato katika taasisi zao. 
Serikali ndio mwanahisa mkubwa ndani ya Benki ya CRDB kutokana na kuwa na umiliki wa asilimia 21 kupitia mfuko wa uwekezaji wa DANIDA kushirikiana na Serikali ya Denmark, huku taasisi na mashirika ya umma yakiwa na umiliki wa hisa za asilimia 17.1.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa akizungumza katika hafla ya kukabidhi Gawio la Serikali kutoka Benki ya CRDB, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma leo Juni 29, 2022.
Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais - Tamisemi, David Silinde akizungumza katika hafla ya kukabidhi Gawio la Serikali kutoka Benki ya CRDB, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma leo Juni 29, 2022.
Naibu Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana, Patrobas Katambi akizungumza katika hafla ya kukabidhi Gawio la Serikali kutoka Benki ya CRDB, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma leo Juni 29, 2022.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru akizungumza katika hafla ya kukabidhi Gawio la Serikali kutoka Benki ya CRDB, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma leo Juni 29, 2022.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad