HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, May 10, 2022

RPC MANYARA ATAKA USHIRIKIANO KUKOMESHA MATUKIO YA UKATILI

 


Na Mwandishi wetu, Mirerani
KAMANDA wa polisi wa Mkoa wa Manyara, Benjamin Kuzaga amewataka wananchi na viongozi wa eneo hilo kushirikiana kwa pamoja ili kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia ambayo yamekithiri Manyara.

Kamanda Kuzaga ameyasema hayo wakati akizungumza na viongozi wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro, viongozi wa dini na wazee maarufu wa mji huo.

Amesema mkoa wa Manyara ni wapili kitaifa kwa matukio ya ukatili wa kijinsia hivyo jamii inapaswa kushirikiana ili kutatua tatizo hilo ambalo limekithiri.

"Hata mkuu wa mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere huwa anasema tupambane tuondokane na ukatili tubaki kuongoza kwenye kukusanya mapato na mengineyo siyo ukatili wa kijinsia kwani tumezidisha," amesema Kamanda Kuzaga.

Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Adam Justin Kobelo ametoa ombi kwa kamanda Kuzaga kuongeza magari mawili kwa ajili ya askari wa kituo cha polisi Mirerani.

"Polisi wa Mirerani wanahudumia tarafa nzima ya Moipo na zaidi hivyo kuwa na gari moja au mawili hawawezi kutenda kazi zao ipasavyo," amesema Kobelo.

Mdau wa maendeleo wa mji huo, Jafari Matimbwa amesema mkuu wa kituo cha polisi Mirerani, SP Paul Ngolo anapaswa kutembelea nyumba za ibada na kutoa elimu ya ulinzi shirikishi.

Matimbwa amesema pia askari wa kituo cha polisi Mirerani wanafanya kazi kwenye mazingira magumu hivyo wakiongezewa magari watengewe pia bajeti ya mafuta ya magari hayo.

Mwenyekiti wa mtaa wa Manyara, Boaz Ambonya amesema kwenye mji mdogo wa Mirerani hakuna huduma ya gari la zimamoto hivyo wananchi wanaathirika pindi ajali ya moto ikitokea.

Mwenyekiti wa mtaa wa Getini, Juma Selemani ametoa ombi kwa kamanda Kuzaga kufikisha kilio cha mahakama ya wilaya inayohamishika ili ihudumie watu wa Mirerani.

Mjumbe wa mamlaka ya mji huo Claudia Dengesi amesema jamii inapaswa kushirikiana na dawati la jinsia la polisi ili kuhakikisha wanatokomeza ukatili wa kijinsia.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad