Na Muhidin Amri,Songea
KAMATI
ya usimamizi wa Huduma za Afya ya mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na
shirika lisilokuwa la Kiserikali la MDH-Amref Health Africa, imeanza
Kampeni ya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu kwa wananchi wanaoishi
katika mazingira duni na hatarishi.
Maeneo
hayo ni kata ya Ruvuma na Bombambili katika Manispaa ya Songea,ambayo
yanatajwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa kifua kikuu katika wilaya
ya Songea mkoani Ruvuma.
Akizungumza
jana,Mratibu wa kifua kikuu na ukoma mkoa wa Ruvuma Dkt Xavier Mbawala
alisema,kampeni hiyo imehusisha kata hizo kutokana na wakazi wake wengi
kuishi kwenye makazi duni ambayo ni hatarishi na rahisi kupata ugonjwa
huo.
Alisema,moja
ya makundi hatarishi yaliyoko katika hatari ya kupata maambukizi ya
kifua kikuu ni umaskini katika jamii ikiwamo kuishi chumba kimoja watu
wengi,nyumba zisizokuwa na mwanga na hewa ya kutosha.
Alisema,
ndiyo maana Serikali ya mkoa kupitia wataalam wa kitengo cha kifua
kikuu na wadau wa mandeleo Shirika la MDH na Amref Afrika imedhamiria
kutokomeza kabisa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2035.
Kwa
mujibu wa Dkt Mbawala ni kwamba,katika kuhakikisha mpango huo
unafanikiwa wameanza kwenda kila wilaya kutoa elimu na kufanya uchunguzi
wa ugonjwa huo ili jamii iweze kufahamu na kuchukua hatua ya haraka
ikiwamo kuwahi Hospitali kupata matibabu.
Dkt
Mbawala alisema, kampeni hiyo itafanyika katika wilaya zote za mkoa huo
na matumaini kuwa italeta tija kubwa na itasaidia kuokoa maisha ya watu
ambao wameambukizwa ugonjwa huo lakini wameshindwa kwenda katika vituo
vya kutolea huduma za matibabu kutokana na sababu mbalimbali.
Dkt
Mbawala alieleza kuwa,ugonjwa wa kifua kikuu unatibika na muhimu kwa
mtu aliyepata ugonjwa huo kuwahi haraka ili kuepuka vifo na kuambukiza
wengine.
“Serikali
yetu ya mkoa wa Ruvuma inashirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo
ikiwamo MDH- Amref Health Africa katika kuboresha huduma za afya ili kwa
pamoja tuweze kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu ifikapo mwaka
2035”alisema.
Kwa
upande wake Mratibu wa kifua kikuu na ukoma Manispaa ya Songea Dkt
Emanuel Kiwale alisema, hali ya maambukizi ya kifua kikuu katika
manispaa ya Songea ni makubwa ambapo amezitaja kata zinazoongoza kuwa na
wagonjwa wengi wa kifua kikuu ni Ruvuma na Bombambili.
Dkt
Kiwale alisema, hali hiyo inachangiwa sana na umaskini kwa wakazi wake
ambapo wanalazimika kuishi watu wengi katika chumba au nyumba moja
isiyokuwa na mwanga au hewa ya kutosha.
Baadhi
ya wakazi wa kata ya Ruvuma,wameipongeza Serikali kupeleka huduma ya
uchunguzi katika maeneo yao kwani itasaidia sana kuokoa maisha ya watu
wengi hasa wazee ambao hawawezi kufika kwenye vituo vya kutolea huduma.
Hadija
Ismaila alisema,kuna watu wanasumbuliwa na ugonjwa huo kwa muda mrefu
lakini wameshindwa kwenda kupata matibabu kwenye vituo na Hospitali
kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo nauli ya kutoka nyumbani hadi
Hospitali.
Alisema,badala
yake wanaendelea kuteseka na hata wapo waliopoteza maisha na kuiomba
Serikali na wadau wa afya kuhakikisha wanasogeza huduma zake karibu na
wananchi badala ya huduma hizo kupatikana makao makuu ya kata,wilaya na
mkoa.
Ibrahim
Salum alisema,huduma hiyo ni nzuri kwani inatoa majawabu ya shida za
wananchi wenye maradhi ambao wana tabia ya kumeza dawa bila kupata
ushauri wa Madaktari.
Amewapongeza
watoa huduma kwa kazi wanaofanya ya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu
kwa wananchi,na kuwataka kuendelea kuwasaidia watu ambao wanakabiliwa
na changamoto nyingi za kimaisha ikiwamo maradhi ya mara kwa mara.
Wahudumu
wa Afya ngazi ya jamii(CHW)wakiwasikiliza baadhi ya wananchi waliofika
kupata huduma ya uchunguzi wa kifua kikuu wakati wa kampeni ya
uchunguzi wa ugonjwa huo inayotolewa bure na wizara ya Afya kupitia
kitengo cha kifua kikuu na ukoma Hospitali ya mkoa wa Ruvuma kwa
kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la MDH-Amref Health Africa.
Muhudumu
wa Afya ngazi ya jamii9CHW) kata ya Ruvuma katika Manispaa ya Songea
Aziza Kivina kulia,akimsikiliza mkazi wa mtaa wa Mibulani Hadija Mohamed
aliyefika kupata huduma ya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu wakati
wa kampeni ya kupambana na ugonjwa wa TB inayolenga kuibua na
kuwaanzishia dawa wale watakaobainika kuwa na ugonjwa huo.
No comments:
Post a Comment