WAZIRI
wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Stergomena
Lawrence Tax (Mb) amefanya ziara ya kutembelea Shirika la Mzinga kwa
lengo la kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Shirika.
Akiwa
katika ziara yake katika Shirika hilo alipata fursa ya kutembelea
maeneo mbalimbali na kujionea shughuli kadhaa zinazoendelea, kupatiwa
maelezo ya kina ikiwa ni pamoja na hatua zilizofikiwa katika kuzalisha
mazo ya msingi, mafanikio, yaliyopatikana, changamoto na mipango
waliyojiwekea.
Hii
ni ziara ya kwanza ya Mheshimiwa Waziri kutembelea Shirika hilo tangu
ateuliwe na kuapishwa rasmi na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kuwa
Waziri wa Ulinzi na JKT tarehe 13 Septemba, 2021.
Akiongea
na Watumishi wa Shirika alibainisha kuwa ”nimekuwa nikijitahidi
kupanga muda wa kutembelea Shirika la Mzinga kwa muda kidogo, nashukuru
kuwa leo nimepata fursa ambapo nimeweza kupata wasaa wa kuja hapa
kuzungumza na ninyi lakini pia kutembelea Shirika, kujionea mwenyewe ,
kupata uelewa mpana wa shughuli zinazofanywa hapa mzinga na kuzitambua
changamoto”.
Dkt.
Stergomena alikumbusha umuhimu wa Shirika hili kwa kusema kuwa” kama
tunavyofahamu, Shirika la Mzinga ni muhimu sana, siyo tu kwa JWTZ na
kwa Wizara lakini pia kwa mustakabali wa maslahi mapana ya Taifa letu
kiulinzi, kiusalama na hata kiuchumi. Unyeti wa majukumu ya Shirika
hili umeainishwa bayana katika Aya 4 (1), (2) ya Sheria ya Mwaka 1969
ya kuanzishwa kwa Shirika, lakini pia unyeti wa Shirika umeainishwa
katika Notisi ya Serikali (Government Notice) Namba 196 kama
ilivyochapishwa katika Gazeti la Serikali la mwaka 1973”.
Akitoa
taarifa ya kwa Mheshimiwa Waziri, Meneja Mkuu, Brigedia Seif Hamis
alisema “Shirika Mama la Mzinga lilianzishwa mwaka 1971 ukiwa ni mradi
kwa ajili ya kuzalisha mazao kwa matumizi ya JWTZ. Tarehe 13 Septemba,
1974 mradi huu ulibadilishwa na kuwa Shirika la Umma (Public
Corporation) chini ya Wizara ya Ulinzi na JKT kwa Tamko la Serikali Na.
219”.
Brigedia
Jenerali Hamis aliongeza kwa kusema kuwa “Shirika la Mzinga kisheria
linao wajibu wa kuzalisha mazao ya msingi na mitambo, kufanya tafiti
mbalimbali, kukarabati vifaa na mitambo mbalimbali na kutekeleza
majukumu yote muhimu kwa maendeleo ya Shirika na Taifa kwa ujumla.”.
“Shirika
la Mzinga linajishughulisha na shughuli kuu mbili, kwanza, ni shughuli
za kuzalisha mazao ya msingi ya mwaka 1971 na yale mazao yaliyoongezwa
mwaka 2012. Pili, Shirika linajishughulisha pia, na shughuli mbadala ili
kujiongezea kipato kwa lengo la kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka
Serikalini”, alimaliza.
Shirika
limeendelea kufanya tafiti mbalimbali ambazo zimelenga kuboresha mazao
linayoyazalisha. Mbali na kufanya tafiti Shirika pia, limeendelea
kufanya maboresho kwa kununua mitambo mipya itakayotumika katika
kuzalisha mazao ya msingi na mitambo, mafunzo kwa wataalamu wa Shirika,
kuendeleza ushirikiano baina ya mashirika yaliyo chini ya Wizara ya
Ulinzi na JKT katika kubadilishana uzoefu pamoja na maboresho ya
miundombinu ya shirika.
Sambamba
na maboresho hayo, juhudi kubwa zimeendelea kufanyika katika kutatua
changamoto za uchakavu wa mitambo na majengo ya karakana, upungufu wa
rasilimali watu, ubovu wa barabara, uvamizi wa mipaka ya eneo la
Shirika pamoja na usalama wa kiwanda ambapo uzalishaji wa zao la msingi
umeanza kuimarika zaidi hadi kufikia asilimia 97.5. Kiwango ambacho
hakijawahi kufikiwa tangu kuanzishwa kwa Shirika hili.
No comments:
Post a Comment