HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, March 4, 2022

WATU ZAID YA 126 WAJITOKEZA KUFANYIWA UCHUNGUZI WA MATATIZO YA USIKIVU NA AFYA YA MASIKIO.

 


Janeth Raphael - MichuziTv Dodoma


Ikiwa leo ni maadhimisho ya siku ya usikivu duniani
Wananchi zaidi ya 126 walijitokeza kufanyiwa uchunguzi wa matatizo ya usikivu na afya ya Masikio katika kambi maalumu ya uchunguzi inayoendelea katika Hospitali ya Benjamini Mkapa Dodoma.

Kambi hiyo ya siku tatu inayofanyika kuanzia tarehe 01-03 Machi, inaendeshwa na Madaktari Bingwa wa Masikio, Pua na Koo kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga & Mloganzila), Hospitali ya Benjamini Mkapa, KCMC, Bugando, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na Hospitali ya Mkoa ya Dodoma.

Akizungumzia mwenendo wa kambi hiyo, Dkt. Costantine Kaniki kutoka Hospitali ya Mkoa wa Dodoma amesema kati ya wagonjwa 126 waliojitokeza 55 walilalamika kuwa na usikivu hafifu lakini baada ya uchunguzi 31 sawa na asilimia 56 ndio waliobainika kuwa kweli wana tatizo na kati yao wanawake ni 18 na wanaume ni 13.

“Miongoni mwa hao waliofanyiwa uchunguzi wawili walibainika kupoteza usikivu kabisa ambao kiumri mmoja ana miaka 69 wakati mwingine ana miaka 22” amesema Dkt. Kaniki.

Akizungumzia sababu mbalimbali zinapelekea mtu kupoteza usikivu Dkt. Godlove Mfuko kutoka Muhimbili Mloganzila amesema kuwa zipo sababu nyingi ikiwemo mtoto kuzaliwa njiti na athari za dawa lakini kelele inatajwa kuwa ndio sababu kubwa inayopelekea watu wengi kupoteza usijivu duniani.

“Sauti kubwa inaharibu masikio na kupelea usikivu hafifu kwa kuwa sauti kubwa inaharibu seli za usikivu na hupelekea mtu kusikia milio isiyo ya kawaida au kupoteza usikivu.

Amesema kwamba watu wanaofanya kazi au wenye mazoea ya kutembelea kwenye maeneo yenye kelele nyingi wapo katika hatari za kupoteza usikivu.

“Changamoto ni kubwa sana hasa kwa watu wenye umri kati ya miaka 18-45 ambapo wengi wao wameathiriwa na sababu mbalimbali lakini sababu kubwa ni kelele zilizopitiliza”

Kambi hiyo maalumu ya upimaji wa usikivu inafanyika ikiwa kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya usikivu duniani inayoadhimishwa tarehe 3 Machi kila mwaka, mwaka huu imebeba kauli mbiu isemayo 'ili usikie vizuri maishani mwako sikiliza kwa taadhali'.

 


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad