CRB yawapa neno makandarasi wazalendo, yataka waungane kupata miradi mikubwa - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, January 26, 2022

CRB yawapa neno makandarasi wazalendo, yataka waungane kupata miradi mikubwa

 

Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), injinia Consolatha Ngimbwa akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa makandarasi wazalendo unaoendelea mkoani Dodoma. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo Joseph Tango na kulia ni Naibu Msajili wa Bodi, Injinia David Jere

Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) Injinia Consolata Ngimbwa akitoka kwenye ufunguzi mkutano wa makandarasi wazalendo unaoendelea mkoani Dodoma. Katikati ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Joseph Tango na kulia ni Naibu Msajili, David Jere.
Naibu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Injinia David Jere akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa makandarasi wazalendo unaofanyika mkoani Dodoma. Katikati ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Consolatha Ngimbwa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Joseph Tango.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MAKANDARASI wazalendo wameambiwa kwamba bila kuungana na kuwa na makampuni yenye nguvu ya mtaji na ujuzi watabaki kuwa watazamani huku kazi kubwa za ujenzi zikichukuliwa na kampuni za kigeni.

Hayo yamesemwa leo Januari 26,2022 mkoani Dodoma na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Injinia Consolata Ngimbwa, wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa makandarasi wazalendo kuhusu wajibu wa makandarasi katika miradi ya ujenzi.

Amesema kampuni kubwa za kigeni zimekua zikipata miradi mingi ya ujenzi kutokana na kuunganisha rasilimali walizonazo na ndizo zimekuwa zikifanikiwa kupata miradi mikubwa ya ujenzi inayogharimu fedha nyingi.

“Kufanya kazi kwa ubia siyo utamaduni wa siku nyingi sana lakini wenzetu wameanza zamani sana. Tuache ubinafsi tuingie ubia kwasababu hata ukipata changamoto ichukue kama changamoto tu ya kukufanya usonge mbele na kuwa muwazi kwa mtu unayetaka kuingia naye ubia,” amesema

Amesema baadhi ya makandarasi wazalendo wamekuwa wakikwama kuungana kutekeleza miradi mikubwa kutokana na ubinafsi wa baadhi yao ambao hawaweki uwazi hivyo kusababisha migogoro baina yao wakati wa utekelezaji wa miradi.

“Najua kuna changamoto wakati mwingine kwa waliojaribu lakini hiyo iwe changamoto tu ya kukupa uzoefu wa kusonga mbele kwasababu hata mzazi anapopata changamoto kwenye uzazi hawezi kuacha kuzaa eti kwa sababu tu alipata shida,” amesema

Vile vile Injinia Ngimbwa ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuanza kutoa kazi nyingi za ujenzi na kuwataka makandarasi wazalendo kuchangamkia fursa hiyo.

Amesema kuna kazi nyingi za ujenzi ambazo zimekuwa zikitangazwa kwa miradi hata ya ujenzi wa madarasa na barabara ambayo makandarasi wazalendo wanaweza kupata.

Amesema wanachotakiwa kufanya ni kujaza zabuni zao ka umakini mkubwa na kuachana na kawaida ya kuwapa watu wengine wawajazie huku akiwataka kuitekeleza miradi hiyo kwa ufanisi.

“Kuna tabia ya kutumia watu wengine kuwajazia zabuni sasa unamwamini mtu anakujazia kumbe ndkiye anayekuangusha, tumia muda mwingi kutulia ili ujaze kitu kinachoeleweka kwasababu wakati mwingine unakosa kazi kwa uzembe wa uliyemwamini,” amesisitiza.

Injinia Ngimbwa pia amewataka wakandarasi hao wawe na chama kimoja chenye nguvu kubwa ambacho kitakuwa sauti yao wanapokuwa na changamoto mbalimbali badala ya kuwa na vyama vingi visivyo na tija.

Naye Naibu Msajili wa CRB Injinia David Jere alisema makandarasi wanapaswa kulipa ada ya mwaka kwa wakati kwasababu ni takwa la kisheria na kwamba wale ambao watakaidi watachukuliwa hatua kali.

Amesema CRB ilianzisha Mfuko wa Kusaidia Makandarasi (CAF) ambapo makandarasi wanaweza kukopa fedha kwaajili ya kuanza kutekeleza miradi anayopata lakini wengi hawajaajiunga ili kunufaika na fedha hizo.

Amesema makandarasi wanaopata mikopo hiyo wanapaswa kuirejesha kwa wakati ili kuwezesha wenzao kupata mikopo kama hiyo pindi wanapopata zabuni za ujenzi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad