HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, January 26, 2022

SACH Israel, Canada watoa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 81

 


Wataalamu wabobezi wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiziba tundu la moyo wa mtoto kwa njia ya upasuaji wa bila kufungua kifua kupitia tundu dogo linalotobolewa kwenye paja kwa kutumia mtambo wa Cathlab (Catheterization Laboratory). Vifaa vya kuziba tundu hilo vimetolewa msaada na Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Israel na Canada.

Mafundi sanifu wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa katika mashine iliyowekwa dawa ya kuwezesha kuonesha tundu lililopo kwenye moyo wakati wataalamu wabobezi wa magonjwa ya moyo kwa watoto wakiziba tundu la moyo wa mtoto kwa njia ya upasuaji wa bila kufungua kifua kupitia tundu dogo linalotobolewa kwenye paja kwa kutumia mtambo wa Cathlab (Catheterization Laboratory
Picha na JKCI

SACH Israel na Canada watoa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 81 kwa ajili ya matibabu ya moyo kwa watoto

Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
SHIRIKA la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Israel na Canada limetoa msaada wa vifaa tiba vya kufanya uchunguzi wa matatizo ya moyo na vya kutibu magonjwa ya moyo vyenye thamani ya shilingi 81,791,175/= ambavyo vinatumika kwa watoto wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Uchunguzi huo pamoja na tiba unafanyika kwa njia ya upasuaji wa bila kufungua kifua kupitia tundu dogo linalotobolewa kwenye paja kwa kutumia mtambo wa Cathlab (Catheterization Laboratory) ambayo ni maabara inayotumia mionzi maalum kwa ajili ya uchunguzi wa matatizo na tiba za magonjwa ya moyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi leo jijini Dar es Salaam Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto Stella Mongella alisema vifaa hivyo ambavyo vilitumwa kwa ndege kutoka nchini Israel vitafanya uchunguzi wa mishipa ya damu ya moyo na mapafu kwa watoto 10 , kuziba matundu ya moyo kwa watoto 12 na matibabu ya dharura kwa watoto wachanga watatu .

“Vifaa tulivyovipokea ni vya kuziba matundu 12, kufanya uchunguzi 10 na vifaa vitatu vyenye puto maalum ambalo linatumika kwa ajili ya kutoa huduma ya dharura kwa watoto wachanga wenye shida ya moyo ambao mishipa yao mikubwa ya moyo imejigeuza. Mshipa mkubwa wa moyo unaotakiwa kutokea chumba cha kulia umetokea kushoto na mshipa wa chumba cha kushoto umetokea kulia”,.

“Watoto wachanga hawa huwa wanaumwa sana siku za mwanzo na wanahitaji matibabu maalum ya kuwaongezea ukubwa wa tundu ambalo liko katikati ya moyo kwenye vyumba vya juu vya moyo, kwa kumuongezea hilo tundu kunampa unaafuu wakati anasubiri kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo”, alisema Dkt. Stella.

Daktari huyo bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto aliwashukuru SACH Israel na SACH Canada ambao wametoa msaada wa vifaa hivyo ambavyo wanavitumia kufanya uchunguzi wa vyumba vya moyo, mishipa ya damu inayotoka na inayoingia kwenye moyo pamoja na kupima msukumo wa damu kwenye mapafu na kwa watoto ambao mioyo yao ina matundu wanayaziba.

Kwa upande wake Deogratius Nkya ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alisema tangu mwaka 2015 hadi 2020 upasuaji wa aina hiyo kwa watoto ulikuwa unafanywa na madaktari kutoka nje lakini kuanzia mwaka jana 2021 madaktari wazawa wameanza kufanya upasuaji huo.

Dkt. Nkya alisema kwa mwaka jana wa 2021 ambapo madaktari wazawa walianza kufanya upasuaji huo mdogo walifanya uchunguzi kwa watoto 76 na kuzibua mishipa ya damu kwa watoto watatu.

Alizitaja faida za upasuaji wa aina hiyo ni mtoto anakaa wodini siku chache baada ya siku mbili au tatu tangu afanyiwe upasuaji anaruhusiwa. Pia watoto wanaofanyiwa upasuaji wa aina hiyo hawahitaji kufanyiwa upasuaji mkubwa wa kufungua kifua.

“Ninatoa wito kwa wananchi hasa wazazi wazitambue dalili za ugonjwa wa moyo kwa watoto wakiona mtoto haongezeki uzito vizuri, anapata maambukizi ya ugonjwa wa mapafu mara kwa mara na anachoka haraka wampeleke hospitali mapema ili aweze kufanyiwa uchunguzi mapema na kupata matibabu kama atakutwa na matatizo”,.

“Faida ya kumtibu mtoto akiwa mdogo atakuwa vizuri na hatapata shida, muda mzuri wa kumtibu mtoto mwenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ni ndani ya miezi sita hadi miaka miwili tangu alipozaliwa. Jambo la muhimu ni kwa wazazi wawe na bima za afya na wawakatie watoto wao pia, kwani gharama za matibabu ni kubwa na kama mtoto atakuwa na bima ya afya akiwa na shida atatibiwa kwa wakati”, alisema Dkt. Nkya.

Naye Elizabeth Silabi kutoka wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya ambaye mtoto wake alitibiwa na vifaa hivyo vya msaada aliwashukuru Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto kwa vifaa walivovitoa ambavyo vimemsaidia mtoto wake kutibiwa pia aliwashukuru madaktari pamoja na wauguzi kwa huduma ya matibabu waliyoitoa kwa mwanawe.

Alisema mtoto wake akiwa na umri wa miaka mitatu alikuwa na tatizo la kukosa nguvu, baada ya kufanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Igongwe iliyopo wilayani Rungwe walitambua alikuwa na shida na kumtuma katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya ambapo baada ya kumfanyia uchunguzi aligundulika kuwa na tundu kwenye moyo.

“Baada ya kufika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) mtoto alifanyiwa uchunguzi na kupatiwa huduma ya matibabu ya upasuaji mdogo wa moyo na kutibiwa tatizo alilokuwa nalo, sasa hivi anaendelea vizuri na ameshaanza mazoezi daktari ameniambia wakati wowote tutaruhusiwa na kurudi nyumbani”, alishukuru Elizabeth.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad