Mwakilishi wa Wazee wanaolelewa katika Makazi ya Wazee Wasiojiweza Kibirizi Mkoani Kigoma Veronica Ramadhan akishukuru kwa zawadi ya Mbuzi waliokabidhiwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Ali Khamis alipofanya ziara kituoni hapo. Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mwanaidi Ali Khamis amewataka wananchi kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalam wa afya nchini kujikinga na ugonjwa wa homa ya mapafu inayoletwa na virusi vya wa Corona.
Naibu Waziri Mwanaidi Ali Khamis ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake Mkoani Kigoma katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa huo pamoja na Makazi ya wa Wazee Kibirizi.
Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan itahakikisha inawalinda wananchi wake dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona kwa kuhakikisha elimu ya kujikinga inatolewa kwa kasi.
“Niseme tuchukue tahadhari zote tunawe mikono kwa maji tiririka, tuvae barakoa na tuepuke misongamano ili tuweze kuondokana na maambukizi ya ugonjwa huu ambao wimbi la tatu limeibuka” alisema Naibu Waziri Mwanaidi
Aidha, Naibu Waziri Mwanaidi amekagua Dirisha maalum kwa ajili ya utoaji wa huduma kwa wazee ambapo ameeleza kuvutiwa kwake na huduma zinazotolewa na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kulivalia njuga suala la kuboresha huduma kwa kundi hilo muhimu kwa Taifa.
Amewaagiza watendaji katika sekta ya Afya kushirikiana na maafisa Ustawi wa Jamii katika ngazi zote kuhakikisha kwamba huduma za afya na huduma nyingine za kijamii zinaboreshwa ili Wazee waishi maisha bora na yenye staha.
Akisoma taarifa ya Hospitali ya Maweni, Mganga Mfawidhi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Dkt. Osimundi Dyegura amesema huduma za katika Hospitali hiyo zimeboreshwa ikiwa ni pamoja kuanzishwa kwa madirisha maalum kwa makundi maalum zikiwemo huduma kwa wazee.
Pamoja na mafanikio hayo Dkt Dyegura amesema miongoni mwa changamoto zinazoikabili Hospitali hiyo ni pamoja na uchakavu wa baadhi ya majengo na uhaba wa madaktari Bingwa kwa baadhi ya magonjwa.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mwanaidi ametembelea Makazi ya Wazee Wasiojiweza Kibirizi Mkoani Kigoma ambapo amevutiwa na huduma zinazotolewa na maafisa kwa kushirikiana na uongozi wa Halmashauri ya Manispaa na Mkoa wa Kigoma.
Amesisitiza kuwa Serikali inawatambua na kuwathamini Wazee wote nchini hivyo wana kila sababu ya kutembea kifua mbele wakiwa na imani kwamba Serikali itaendelea kuboresha huduma kwa wazee kadiri inavyopata rasrimali.
Akizungumza kwa niaba ya Wazee, Katibu wao, Veronica Ramadhan amemshukuru Naibu Waziri kwa kuwatembelea na kuwapelekea Zawadi ya Mbuzi wawili kwa ajili ya kitoweo na kushukuru kwa huduma wanayoipata katika Makazi hayo.
Bibi Veronica ameshukuru kwa zawadi hiyo na kusema imewaongezea moyo wa Imani kwa serikali huku akituma salamu za shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaelekeza wasaidizi wake kuyatembelea makundi maalum likiwemo kundi la Wazee.
Pia katika ziara yake Naibu Waziri Mwanaidi ametembelea Dawati la Polisi la Jinsia Wilayani Kigoma ambapo ameelezwa kuwa kiwango cha ukatili wa kijinsia Mkoani kiko juu na hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa na kuvielekeza vyombo vinavyoshughulikia na kesi za vitendo vya ukatili kuhakikisha kesi hizo zinashughulikiwa kwa haraka na watuhumiwa pamoja na wahanga wa vitendo hivyo wanapata haki yao.
No comments:
Post a Comment