*******************************
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Deogratius John Ndejembi leo ametembelea jengo la Benki ya Equity katika maonesho ya Sabasaba Jijini Dar es Salaam na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanyika na kusema kuwa uwepo Benki hiyo ni msaada mkubwa kwa Wananchi huku akipongeza mpango wa benki hiyo wa uwezeshaji vikundi uitwao “Eazzy Kikundi” kuwa ni ukombozi halisi kwa wananchi wa chini.
"Nimefurahishwa sana kusikia habari za mpango huu wa “Eazzy Kikundi” ambao unahusika kuwaunganisha wananchi hususan wajasiliamari kama Bodaboda, Mama ntilie na wengineo katika makundi na hivyo kuwawezesha kiuchumi kupitia mikopo na elimu ya fedha. Serikali siku zote imeunga mkono juhudi hizi ambazo pamoja na kuongeza juhudi za kujenga uchumi jumuishi, lakini pia zinasaidia kuongeza vipato binafsi na pato la taifa kwa ujumla. Elimu ya Fedha na mitaji ni kilio kikubwa sana kwa vijana wa Tanzania. Kwa hili naipongeza sana Equity Bank kwa kuja na wazo hili” alisema Mh.Ndejembi.
Kwa upande wake Mkuu wa Masoko wa Benki ya Equity Bw.Godwin Semunyu amesema kuwa pamoja kutoa huduma zote za kibenki katika maonesho hayo, Benki ya Equity pia inaendesha darasa maalum la masuala ya fedha na uwekezaji kwa vikundi vya wajasiliamari vinavyoshiriki maonesho hayo. "Equity Bank ni benki pekee kwenye maonesho haya ambayo ina darasa maalum la masuala ya fedha na uwekezaji. Lengo letu ni kutoa ufahamu juu ya masuala ya fedha ili kuwapa wateja wetu nafasi ya kufanya maamuzi na uwekezaji sahihi. Benki pia imekuwa ikiwahamisisha wananchi kutumia kadi zetu mpya za Eazzy Card ambazo ni kadi za malipo ya awali na hivyo kuwaondolea uhitaji wa pesa taslimu” alisema.
No comments:
Post a Comment