Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof.
Kitila Mkumbo (Mb) akipata maelezo ya namna umwagiliaji mashamba ya miwa
unavyofanyika.
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa kiwanda cha sukari cha Bagamoyo ambacho uzalishaji wake unatarajiwa kuanza mwezi juni mwaka 2022 kwa kuzalisha tani elfu 30 hadi 35 kwa kuanzia na kitakapokamilika kitazalisha tani laki moja (100,000) kwa mwaka katika kukidhi mahitaji ya sukari nchini.
Mhe. Prof. Mkumbo ameyazungumza hayo leo tarehe 13 Juni, 2021 alipotembelea mradi wa ujenzi wa Kiwanda kikubwa cha sukari kilichopo Bagamoyo na kujionea mashamba ya miwa na mabwawa ya maji kwa ajili ya umwagiliaji wa miwa.
Mhe. Prof. Mkumbo amesema kuwa moja ya vipaumbele vya Serikali ni kuwekeza katika viwanda ambayo vitazalisha bidhaa ambazo tunazihitaji kwa kiasi kikubwa na moja ya bidhaa hizo ni sukari, kwa sasa tuna mahitaji ya sukari ambayo ni tani 655,000 kwa mwaka ambapo uzalishaji wa sasa kwa viwanda vyote vya sukari ni tani 386,000 mpaka mwezi Mei mwaka huu uzalishaji ulikuwa ni tani 256,000 ambayo ni asilimia 60 ya mahitaji yote ambapo asilimia 40 inabidi tuagize kutoka nje ya nchi.
Aidha Mhe. Prof. Mkumbo amesema kuwa kwa sasa Tanzania tuna viwanda vya sukari takribani vitano ambavyo vilikuwa vya serikali wakapewa sekta binafsi ili kuviendeleza, kiwanda hiki cha kuzalisha Sukari cha Bagamoyo ni cha umiliki wa sekta binafsi kwa asilimia 100.
Naye Mkurugenzi wa mawasiliano wa makampuni ya Bakhresa ambaye ndiye mratibu wa mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha sukari Bagamoyo ndugu Hussein Sufian amesema mradi huo unahusisha maeneo makubwa mawili kuendeleza shamba la kilimo cha miwa na ujenzi wa kiwanda.
Aidha amesema kuwa ujenzi wa kiwanda umefikia asilimia 90 na changamoto iliyopo ni ubovu wa miundombinu ya barabara kutoka makurunge hadi kiwandani na pia upatikanaji wa huduma ya maji ya uhakika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ambapo wanashirikiana vyema na Wizara ya maji ambao wana mpango wa kujenga bwawa kwa ajili ya utatuzi wa changamoto hiyo. Aidha ameishukuru TANESCO ambapo kwa sasa umeme umekwishaunganishwa na hawatumii tena majenereta.
Ndugu Sufian ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kushughulikia changamoto wanazopata kwa wakati na kuipongeza serikali ya wilaya ya Bagamoyo kwa juhudi wanazofanya katika kuhakikisha kiwanda kinakamilika mapema kwa muda uliopangwa na kuanza kazi kwani kiwanda kwa awamu ya kwanza kinategemea kuajili wafanyakazi zaidi ya elfu moja (1,000) na baada ya awamu zote tatu kukamilika kiwanda kitaajili wafanyakazi zaidi ya elfu nne (4,000.)
Mkuu wa
wilaya ya Bagamoyo Mhe. Zainab Kawawa amesema kuwa ofisi yake inashughulukia
changamoto ya uvamizi wa ardhi kwa eneo walilopewa, na serikali ipo katika
mpango wa kumuongezea eneo mwekezaji huyo mzawa kati ya hekta 12,000
zilizobakia baada ya kupewa hekta 10,000 ili kumaliza changamoto hiyo ya
wavamizi wa ardhi.
No comments:
Post a Comment