HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, June 14, 2021

TUNAHITAJI UWEKEZAJI WA VIWANDA UNAOTUNZA MAZINGIRA-WAZIRI JAFO

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo, akionyeshwa mtungi wa gesi unavyozalishwa katika kiwanda cha Lake Steel Company Limited kinachozalisha gesi na nondo Kilichopo Kibaha mkoani Pwani.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani jafo, akikagua mtaro wa maji machafu katika kiwanda cha Prance International Company Limited kilichopo Misugusugu Kibaha Mkoa wa Pwani.
Meneja wa Kiwanda cha Prance International Company Limited Bw. Salum Mohamed (aliyenyanyua mkono), akitoa maelezo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani jafo, juu ya namna wanavyotekeleza maagizo waliyopewa na NEMC. Prance ni Kiwanda kinachozalisha sabuni kilichopo Misugusugu, Kibaha Mkoa wa Pwani. Wa tatu kulia Meneja wa Kanda ya Mashariki Kasikazini (NEMC) Bw. Arnold Mapinduzi pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe. Martin Ntemo (pili kulia).
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo, akikagua mazingira katika kiwanda cha Lake Steel Company Limited Kilichopo Kibaha mkoani Pwani. Wa pili kulia ni Meneja wa NEMC Kanda ya Mashariki Kasikazini Bw. Arnold Mapinduzi
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo, akitoa maelekezo kwa Bwana Deusi Antony Meneja wa kiwanda cha Vunjo Afro Company kinachozalisha nondo, kilichopo Misugusugu, Kibaha mkoani Pwani.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo, akionyesha maji machafu yanayozalishwa na kiwanda cha Vunjo Afro Company ambayo yanakwenda kwenye mazingira bila kutibiwa, kiwanda hiko kipo Misugusugu Kibaha mkoani Pwani.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Selemani Jafo amesema kuwa, Taifa linahitaji uwekezaji wa Viwanda ambavyo vinalinda na kuhifadhi mazingira yetu kwa manufaa ya Kizazi kilichopo na kijacho. Alisisitiza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Hassan Suluhu, anataka uwekezaji wa viwanda lakini unaojali maslahi,afya na Mazingira kwa ujumla.

Amesema hayo mjini Kibaha alipofanya ziara katika kiwanda cha Vunjo Afro Company ambacho mwanzoni kilikuwa kina fahamika kwa jina la shark tachi Ltd kinachozalisha misumari, kilichopo eneo la Misugusugu, wilayani hapo. Alifanya ziara hiyo ili kujionea hali ya kimazingira katika kiwanda hicho. Katika ziara yake Mhe. Jafo alibaini changamoto mbalimbali za kimazingira pamoja na kubadilisha jina la kiwanda bila kutoa taarifa NEMC.

Aidha Mhe.Jafo amewataka wenye kiwanda hicho kufanya uzalishaji bila ya kuchafua mazingira kwani Serikali inataka maisha bora kwa Wananchi wenye afya bora na salama. Ameendelea kusema kuwa mazingira ya kiwanda hicho hayajamridhisha lakini hatakifunga ila ametoa wiki mbili kwa kiwanda hiko kuhakikisha maji yanayotumika wakati wa uzalishaji hayatiririshwi kwenda kwenye mazingira, pia amewataka watoe taarifa juu ya utupaji wa uchafu au vumbi linalobaki kutoka kwenye chuma baada ya kuzalisha.

“vumbi litokanalo na chuma ni hatari sana kwa Maisha ya binadamu na viumbe hai, ikiwa kama kiwanda mnashindwa kueleza kuwa hili vumbi mnalipeleka wapi basi kwa asilimia kubwa ni wachafuzi wa mazingira yetu na hamna huruma na wananchi juu ya Maisha yao bali mnaangalia masilahi yenu. Kutokana na kushindwa kujieleza vizuri natoa wiki mbili kwenu mnieleze wapi mnapeleka vumbi hili, niseme tu kweli sijaridhika na mazingira na mwenendo wa kiwanda hiki, tunataka uwekezaji lakini uwekezaji wenye tija kwa Taifa, hivyo NEMC hakikisha mnafanya ukaguzi na kutoa maelekezo kwa kiwanda hiki” alisema Waziri Jafo.

Kwa upande wake Meneja wa kanda ya Mashariki Kaskazini (NEMC) Bwana Arnold Mapinduzi, amesema kuwa kiwanda cha Vunjo Afro Company ambacho kilisajiliwa Baraza kwa jina la Shark Tachi Limited, kabla ya kuanza uzalishaji kilijisajili NEMC ili kufanya Tathmini ya Athari kwa mazingira lakini baadaye kiliamua kuanza uzalishaji kabla ya kumaliza Mchakato, hivyo walivunja sheria ya Mazingira ya mwaka 2005. Bwana Mapinduzi ameendelea kusema kuwa lakini hata hivyo wakati wa ukaguzi katika kiwanda hicho walibaini utiririshwaji wa maji kutoka kwenye kiwanda na kwenda kwenye mazingira na kuwataka wahakikishe maji wanayopeleka kwenye mazingira wanayatibu.

Vile vile Mh. Jafo amefanya ziara ya kushtukiza katika kiwanda cha France International Company Limited, kinachozalisha sabuni ya unga kilichopo Misugusugu Kibaha Pwani, ili kujionea namna wanavyofanya shughuli zao kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira. Akiwa kwenye ziara hiyo amebaini kiwanda kimezingatia kwa kiasi Fulani maelekezo waliyopewa na NEMC na kuwataka wamalizie kuweka zuio eneo wanalo hifadhia makaa ya mawe. Pia ametembelea Kiwanda cha Lake steel Company Limited kinachozalisha nondo na gesi kilichopo Kibaha Pwani amekipongeza kwa namna kinavyofanya shughuli zake kwa kujali utunazaji wa mazingira

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe. Martin Ntemo, amesema kuwa wilaya itaendelea kupitia viwanda hivyo na pale Baraza linapokuja kufanya ukaguzi katika viwanda waendelee kushirikiana nao ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kwa pamoja. Amesema kuwa uwekezaji katika Wilaya ya Kibaha uwe na neema kwa wananchi na isiwe njia ya kuwakandamiza wananchi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad