HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, June 14, 2021

SHAKA AWAPA UJUMBE WANASIASA VYAMA VYA UPINZANI











Na Mwandishi Wetu, Tanga

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa rai kwa baadhi ya vyama vya siasa nchini kujitathimini ili viweze kufanya siasa ya kisayansi na kuacha tabia yao ya kufanya siasa za unajimu na ubashiri.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka ameyasema hayo katika vikao vyake na viongozi na wanachama wa CCM wa Kata za Madanga, Mwera na Pangani Magharibi zote za wilayani Pangani mkoani hapa.

Shaka yupo kwa ziara ya siku tatu Mkoa wa Tanga, ambapo aliwataka wapinzani kuchagua moja kati ya kuamini na kufuata sayansi ya siasa ambayo inahimiza katika kuweka Milano thabiti, kuimarisha oganaizesheni ya chama cha siasa na kujifanyia tathmini ama waendelee kufanya siasa za matukio, utabiri na porojo za kisiasa ambazo zinaleta hamasa ya muda mfupi na kamwe haziviimarishi vyama hivyo.

Amesema kitendo cha hivi karibuni cha baadhi ya viongozi wakuu wa vyama vya upinzani kutumia majukwaa ya kisiasa kupalilia mbegu za ukanda, ukabila na udini hakikubali na hakiendani na hulka na desturi zetu watanzania hivyo amewaomba wananchi kuwapuuza badala yake waendelee na mipango ya shughuli za kujiletea maendeleo.

“Chama Cha Mapinduzi kinalaani vikali kauli zote za uchochezi na ubaguzi kwa kutumia ukabila, ukanda na udini zilizoanza kutolewa na kushamiri kutoka katika vinywa vya baadhi ya viongozi wa upinzani nchini.

" CCM inaendelea kuamini kuwa tabia hiyo sio utamaduni wa watanzania bali ni uroho na ubinafsi wa kutafuta madaraka kwa nguvu baada ya sera zao kukataliwa na wananchi na kujikuta wakitapatapa kutafuta huruma ambayo hawastahili kabisa” alisema Shaka.

Aidha amekumbusha wosia wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipowahi kuwaonya wanasiasa wanaotumia siasa za Kibaguzi, ukanda na ukabila kama hoja ya kusaka kuungwa mkono na kupata madaraka wamefilisika kisiasa na ni watu hatari kwa mustakabali wa amani na mshikamano wa Taifa letu.

“Msingi mkubwa wa ushindi wa chama cha siasa ni maandalizi ya kimkakati, mkusanyiko wa takwimu na matumizi ya sera bora kama nyenzo muhimu inayokipatia ushindi chama cha siasa, wajifunze kwa CCM ambapo viongozi wake tumeshuka chini kabisa mashinani, hii ndio tofauti yetu na vyama vyingine CCM hubadilika kulingana na mahitajio ya nyakati husika na sio kuigawa jamii ili kupata huruma ya kabila fulani ama dini fulani ili kushika dola” alisema Shaka

Kuhusu ziara hiyo katika mashina Shaka amesema wameamua kushuka chini ili kutekeleza matakwa ya Katiba ya CCM ibara 21 na 22 zinazoelezea kuwa shina ndio msingi mkuu wa chama hicho hivyo kuna kila haja ya kuimarisha uhai wa CCM kuanzia ngazi ya chini kabisa ambayo ni shina.

“Pamoja na kuimarisha ngazi ya mashina ili kukiongezea nguvu za kisiasa Chama Cha Mapinduzi lakini pia tutapata nafasi ya kuisimamia Serikali kwa kukagua miradi ya maendeleo iliyo katika hatua mbalimbali ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.

" Vile vile ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa katika Mkutano Mkuu maalum mwishoni mwa mwezi Aprili, 2021. Kwa maelekezo hayo tumefanya ziara Mkoa wa Tanga.

"Ambapo Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo leo hii atakuwa wilaya ya Kilindi na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga yeye atakuwa wilaya ya Mkinga mkoani Tanga,” amefafanua Shaka.

Amewataka watanzania wote kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe Rais Samia Suluhu Hassan ili iendeleze kazi kubwa ya kuijenga nchi yetu na kuifikisha mbali zaidi kimaendeleo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad