HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, April 12, 2021

WAKULIMA WA TUMBAKU KUPATA NEEMA KUPITIA USHIRIKA

 

Mradi wa Pamoja wa Wakulima wa zao la Tumbaku Tobbacco Cooperative Joint Enterprise Limited (T.C.J.E) wametakiwa kutumia mfumo wa Ununuzi wa Pamoja Bulk Procurement (B.P.S) kwa lengo la kusaidia wakulima wa Tumbaku kupitia Vyama vya Ushirika kupata pembejeo za kilimo kwa bei nafuu.

Maagizo hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe Aprili 11, 2021 wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa 3 wa T.C.J.E Mkoani Morogoro.

Naibu Waziri ameeleza kuwa ili mkulima wa Tumbaku aweze kupata pembejeo ikiwemo Mbolea kwa gharama nafuu ni vyema Mradi huo ukafanya taratibu za kukusanya mahitaji ya pembejeo za wakulima wa Tumbaku kutoka kwenye Vyama vya Ushirika wanachama wa Mradi huo. Akiongeza kuwa kufanya hivyo kutapunguza riba za gharama za mikopo ya mabenki, mianya ya ubadhilifu na kuondokana na madeni hewa ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara.

“T.C.J.E katika msimu mpya wa Tumbaku mwaka huu 2021 hakikisheni mahitaji ya wakulima ya Mbolea yanakusanywa mapema na mnunuzi anasambaza mbolea hiyo moja kwa moja kwa wakulima kupitia Vyama vya Ushirika,” alisema Naibu Waziri

Aidha, Mhe. Bashe alieleza kuwa Kilimo ni Sekta muhimu inayochangia kutoa ajira kwa watanzania kwa wastani wa asilimia 60 hadi 75 na kuchangia pato la Taifa kwa wastani wa asilimia 25. Hata hivyo, Naibu Waziri amebainisha kuwa mapato kutokana na zao la Tumbaku kwa sasa yameshuka kutoka Dola Millioni 300 hadi 146.5 jambo ambalo linachangiwa na kushuka kwa uzalishaji pamoja na kupungua kwa matumizi ya zao hilo.

Pamoja na mambo mengine Naibu Waziri amesema bado Serikali ina dhamira ya kuendelea kulinda na kusimamia zao la Tumbaku. Akiongeza kuwa Ilani ya Chama Tawala imetoa maelekezo mahususi ya kuimarisha na kujenga Ushirika.

Ili kuhakikisha kuwa Ushirika unaendelea kuendeshwa kwa kufuata Sheria Naibu Waziri Bashe amemuagiza Mrajis wa Vyama vya Ushirika kukamilisha ripoti ya baadhi ya Vyama vya Ushirika ambavyo vina shutuma za ubadhilifu na ripoti hizo ziwasilishwe katika Mamlaka husika kwaajili ya hatua zaidi.

Akiongea wakati wa Mkutano huo Naibu Waziri amempongeza Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege kwa utekelezaji wa kuanza utaratibu wa kutumia wahitimu wa Vyuo vikuu katika shughuli za uendeshaji wa Vyama vya Ushirika kwa lengo la kutoa fursa kwa wahitimu hao kujitolea kutumia weledi wao katika nyanja mbalimbali na wao kupata uzoefu wa kazi. Alisema kuwa hatua hiyo ni jambo la kupongezwa kwani wahitimu wengi wanamaliza vyuo na hawana sehemu za kukuza taaluma zao na wakati huohuo Ushirika unapata fursa ya watendaji wasomi watakaoongeza tija kwenye vyama hivyo.

Mkutano huo ulifuatiwa na Uchaguzi wa Viongozi wa T.C.J.E uliowezesha kupata Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti pamoja na Wajumbe wa Bodi uliofanyika kwa mujibu wa Sheria Na.6 ya Vyama vya Ushirika ya mwaka 2013. Hatua ambayo itafuatiwa na Mafunzo elekezi, makabidhiano, fomu za kiapo na maadili yatakayowezesha kuzingatiwa kwa Sheria, Kanuni na Taratibu za Ushirika.

Naibu Waziri Mhe.Hussein Bashe akisistiza janbo wakati wa Mkutano Mkuu wa  Mradi wa Pamoja wa Wakulima wa zao la Tumbaku Tobbacco Cooperative Joint Enterprise Limited (T.C.J.E) wakati wa Mkutano Mkuu wa tatu uliofanyika Mkoani Morogoro April 11, 2021.


Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akifafanua masuala ya Ushirika wakati wa Mkutano Mkuu wa  Mradi wa Pamoja wa Wakulima wa zao la Tumbaku Tobbacco Cooperative Joint Enterprise Limited (T.C.J.E) wakati wa Mkutano Mkuu wa tatu uliofanyika Mkoani Morogoro

Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Morogoro Bw. Keneth Shemdoe akieleza masuala ya Ushirika wa Mkoa wa Morogoro wakati wa Mkutano Mkuu wa  Mradi wa Pamoja wa Wakulima wa zao la Tumbaku Tobbacco Cooperative Joint Enterprise Limited (T.C.J.E) wakati wa Mkutano Mkuu wa tatu uliofanyika Mkoani Morogoro April 11, 2021

 





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad