HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, April 12, 2021

PROF MKUMBO AAGIZA UIMARISHWAJI WA SEKTA YA VIWANDA NA BIASHARA ILI ICHANGIE KIWANGO KIKUBWA CHA UKUAJI WA UCHUMI

 

Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo (Mb)  ametoa maelekezo kwa ajili ya kuimarisha sekta ya viwanda na biashara ili  sekta hizo zichangie kwa kiwango kikubwa  katika ukuaji wa uchumi na kutekeleza malengo ya  Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa III wa miaka mitano 2021/22 – 2025/26,  Ilani ya CCM ya uchaguzi 2020 na Maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita  na Ushauri na maoni maelekezo ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukuza uchumi wa Viwanda nchini.  

Profesa Mkumbo ametoa maelekezo hayo alipokutana na menejimenti ya wizara na wakuu wa taasisi zilizochini ya wizara hiyo kwa lengo la kutoa  mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu ya Wizara katika kikao kilichofanyika  tarehe 10/04/2021 katika ukumbi wa Chuo cha Biashara jijini  Dodoma.

Akiongea katika kikao hicho, Waziri alisema Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025 inalenga kuona Tanzania inahitimu na kuondokana kuwa nchi masikini  inayotegemea kilimo na uchumi wa uzalishaji duni na kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025  ambapo wananchi wengi wajihusihe na kilimo cha kisasa kinachofunganishwa na viwanda na huduma. Hivyo alisisitiza kuwa ili kufikia dira hii wizara hiyo ina nafasi na mchango mkubwa  katika kufanikisha azma hiyo.

“ Uchambuzi wa maudhui ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na  Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa III wa miaka mitano 2021/22 – 2025/26 unaonesha wazi kabisa nafasi ya Sekta ya Viwanda na Biashara…sisi kama Wizara tunatarajiwa kutoa mchango karibu kwa kila eneo la matokeo tarajiwa.”

Alisema pia katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa III wa miaka mitano 2021/22 – 2025/26, malengo sita kati ya malengo mahsusi 12 yanahusu sekta ya viwanda na biashara, kati ya vipaumbele vitano vya mpango huo vitatu vinahusu wizara hiyo, katika Sekta 30 za mpango  huo Sekta 6 zinahusu  Wizara na katika hatua 156  hatua 54  zinahusu  Wizara ya Viwanda na Biashara.


“Taasisi zote zilizochini ya Wizara ya Viwanda zinamchango mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango wa taifa wa Maendeleo wa III wa miaka mitano 2021/22 – 2025/26, malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020, Maelekezo ya Serikali awamu ya sita. Hivyo nawasihi muendelee kufanya kazi kwa mujibu wa Sheria Kanuni na taratibu zinazosimamia taasisi zenu katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi na si kuwa kikwazo”

Hata hivyo, Profesa Mkumbo alisema hakusudii kutumia muda mwingi katika kutunga Sera, Sheria na mikakati na kuwa yeye analenga katika utekelezaji na kuona matokeo ya utekelezaji huo kwa kuchochea ukuaji wa haraka wa Sekta ya Viwanda na Biashara.

Pia aliwataka wataalamu wa Idara ya Sera na Mipango ya Wizara kusimamia uhuishaji wa nyaraka mbalimbali za kisera na sheria  ili ziende na wakati na kuakisi maudhui ya Mpango wa tatu wa Maendeleo na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Akitoa maelekezo mahususi kwa upande wa sekta ya viwanda, Profesa Mkumbo alitaka kuwa bayana na dhana na aina ya viwanda tunavyotaka kuviendeleza hapa nchini, kuwa na kanzi data ya kisasa ya viwanda. Pia alielekeza katika kupima maendeleo ya viwanda kwa kuzingatia kiwango cha uzalishaji na ajira, kuweka mazingira namasharti rahisi katika kukuza na kuchochea viwanda vidogo vidogo vinavyotumia teknolojia rahisi na ya kisasa na vilivyojikita vijijini na mijini,

Profesa Mkumbo pia alisisitiza mkazo katika kuwatambua, kuwawezesha na kuwahudumia wawekezaji katika viwanda vikubwa na vyenye tija katika uchumi na kuhuisha Mkakati wa Viwanda nchini, ikiwemo dhana ya EPZ na SEZ. Alisema pia kusimamia kwa karibu miradi ya kielelezo iliyopo katika Mpango wa Maendeleo wa Tatu wa Taifa ambayo ni mradi wa Chuma wa Mchuchuma na Liganga, Magadi Soda wa Engaruka, ujenzi wa Kiwanda cha Sukari-Mkulazi na kanda Maalum za Uchumi na Maeneo Maalum ya Uwekezaji

Profesa Mkumbo alisema pia kuimarisha utafiti na matumizi yake katika maendeleo ya viwanda, ikiwemo kuwa na ushirikiano wa karibu na taasisi za utafiti na elimu ya juu na kupanua na kuboresha mahusiano na ushirikiano na taasisi za sekta binafsi.

“ Pia kuimarisha ushirikiano na OR-TAMISEMI katika maendeleo ya viwanda vidogo vidogo, tunataka kuona uwezekano wa kuwaongeza majukumu maafisa biashara wa Halmashauri ili pia wasimamie viwanda vidogo vidogo katika maeneo yao kwa kushirikiana na SIDO.”

Kwa upande wa sekta ya biashara, Profesa Mkumbo aliweka msisitiza katika suala la kujenga imani kwa wafanyabiashara kupitia, uwazi na mawasiliano chanya ya mara kwa mara. “Tunataka tunapokutana na wafanyabiashara tufanye mazungumzo yenye tija ya kubadilisha mikakati ya kukuza biashara na masoko, badala mikutano hiyo kutumika tu kama jukwaa la kusikiliza malalamiko ya wafanyabiashara.”

Alisema pia kuendelea kuzipitia kanuni za mamlaka za udhibiti zinazoonekana kukwamisha biashara, kuchochea na kuhamasisha tabia ya kujali wateja miongoni mwa watendaji wa Serikali wanaohudumia sekta mbalimbali za biashara.

Profesa Mkumbo alisema pia kuipitia na kufanya tathimini ya utekelezaji wa “Blue Print” kwa lengo la kuona maeneo ambayo bado hayajatekelezwa na kusimamia utekelezaji wake kikamilifu na kwa haraka, kushirikiana na OR-TAMISEMI, kuchambua na kuchakata kwa umakini maoni ya wabunge na wadau wengine kuhusu haja ya kuwa na Mfuko mmoja wa Mtaji kwa ajili ya wajasiriamali na wafanya biashara wadogo.

Alisema pia kuratibu na kusimamia uanzishwaji wa sera ya maendeleo ya sekta binafsi, ikiwemo biashara ndogo zinahitaji upendeleo maalumu ili kukua na kuweka msisitizo wa pekee katika kutafuta masoko ya bidhaa za Tanzania ndani ya nchi na nje ya nchi na kuratibu na kusimamia uanzishwaji wa maeneo maalum ya kibiashara hususani kwa maeneo ya mipakani. Pia, kuona namna ya kuimarisha eneo maalumu la kibiashara la Kariakoo ambalo kihistoria limekuwa likifanya vizuri na kuwalinda walaji.

Aidha, Profesa Mkumbo amesisitiza haja ya watendaji wa wizara na wataasisi kubadilisha mtizamo katika utendaji kazi na kuwa na “corporate thinking” na tabia ya kujali wateja kwa kuzingatia kuwa wadau tunaowahudumia ni wafanyabiashara.

Pia amewalekeleza wataalamu wa wizara hiyo kuhakikisha wanatoa ushauri wa kitaalamu wenye ushahidi wa kisayansi na ameahidi atatoa ushirikiano mkubwa kwa wafanyabiashara

Aidha, Profesa Mkubwa alisikiliza maoni na changamoto mbalimbali zinazozikabili taasisi hizo kutoka kwa Wakuu wa Taasisi kutoka TBS, WMA, BRELA, TANTRADE, SIDO, NDC, EPZA, FCC, FCT, WRRB, TIRDO, CAMARTEC, TEMDO na CBE na kuahidi kuzitatua.

 

 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad