Na. Hassan Mabuye, Mwanza
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi imeanza kutekeleza mradi wa utambuzi wa kila kipande cha
ardhi kwa ajili ya kupanga, kupima na kumilikisha vipande vya ardhi kwa
kutoa leseni za makazi ndani ya siku 14.
Akizungumza wakati wa
uzinduzi wa mradi huo wa utambuzi na utoaji wa leseni za makazi katika
viwanja vya shule ya msingi Mabatini wilaya ya Nyamagana Naibu Waziri wa
Ardhi Mhe. Dkt. Angeline Mabula amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano
chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli kupitia Wizara ya Ardhi imekusudiwa
kuwatambua wananchi wote wanaoishi katika makazi ambayo hayajapangwa
hivyo kuwapimia na kuwamilikisha ardhi yao.
Amesema lengo la
mradi huu ni kuondokana na changamoto za kukosa miliki ya ardhi kisheria
ikiwemo kuendeleza maeneo yao huku akiwasisitiza wananchi hao
kuhakikisha wanalipa kodi ya pango la ardhi mara baada ya kukabidhiwa
leseni hizo za makazi.
Aidha Naibu Waziri Dkt Mabula akawaasa
wananchi hao kuhakikisha wanaendeleza miliki zao kwa kufuata sheria na
taratibu za mipango miji pamoja na kulipa kodi ya pango la ardhi kwa
wakati.
"Usipolipa kodi ya ardhi utaletewa Ilani ulipe na
ukiendelea kukaidi utapelekwa katika baraza la ardhi ulipe, ikifika
miezi sita hujalipa sheria inamtaka afisa ardhi mteule afute miliki yako
bila hata kukwambia" Alisema Dkt. Mabula.
Kwa upande wake
Kamishina wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mwanza Bwana Eliah Kamihanda
amefafanua kuwa mradi huu ujulikanao kwa jina la 'fit for purpose' una
lengo la kutambua vipande vya ardhi vilivyoendelezwa bila kufuata
sheria na taratibu za mipango miji (makazi holela).
Kamihanda
meongeza kuwa vipande vya ardhi 5,957 vinatarajia kutambuliwa na
kumilikishwa kupitia utoaji wa leseni za makazi kwa mkoa wa Mwanza
pekee, Wakianzia kata ya Mabatini huku tangu kuanza kwake mwezi januari
mwaka huu kwa kata hiyo vipande vya ardhi 111 vimeshatambuliwa na
kutolewa leseni za makazi kwa wamiliki wake
Nae mratibu wa
mpango huo kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Godfrey
Machabe akaongeza kuwa mpango wa kupanga, kupima na kumilikisha vipande
vya ardhi kwa kutoa leseni za makazi kwa kuanzia unatekelezwa katika
mikoa miwili nchi nzima ikiwemo Mwanza na Arusha hivyo kuwataka wananchi
kutumia vizuri fursa hiyo ili kupata umiliki wa kisheria kwa vipande
vya ardhi wanavyovimiliki
Moja ya wananchi walionufaika na mradi
huo Bwana Yona Fumi Ng'wenhelwa mkazi wa kata ya Mabatini akaishukuru
Serikali kupitia wizara ya ardhi kwa kuendesha zoezi hilo kwani
limemsaidia kutatua kero ya kukosa Mali isiyohamishika kisheria pindi
anapotakiwa kumdhamini ndugu yake au kukopa katika taasisi za fedha
sambamba na kuridhishwa na kasi ya maandalizi na utoaji wa leseni hizo
kwani umetumika muda mfupi mpaka kuipata leseni yake ya makazi.
No comments:
Post a Comment