SONGWE TUMESHAAMUA KURA ZOTE ZA URAIS NI KWA DK.JOHN MAGUFULI' - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 1, 2020

SONGWE TUMESHAAMUA KURA ZOTE ZA URAIS NI KWA DK.JOHN MAGUFULI'

Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Songwe

MGOMBEA ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyepita bila kupingwa katika jimbo la Songwe, Philip Mulugo, amesema wana Songwe zawadi watakayompa Dk. John Magufuli, kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu ni ushindi wa kishindo kutoka na maendeleo makubwa aliyowapatia wananchi wa jimbo hilo.

Mulugo amesema hayo leo Oktoba 1, 2020 katika mkutano wa kampeni za mgombea urais kupitia CCM Dk.Magufuli ambaye amefika Mkoa wa Songwe kuomba ridhaa ya wananchi wachague tena ili aweze kuendelea kuwatumikia katika kuwaletea maendeleo na kutekeleza yake ambayo amekuwa akiahidi ya kuijenga Tanzania mpya.

Amefafanua katika Mkoa wa Songwe kuna mambo makubwa ya maendeleo yamefanyika katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Dk.Magufuli ambaye amefanya makubwa kuliko kipindi kingine cha  nyuma.

Kwa upande wa jimbo la Songwe ambalo tayari yeye amepita bila kupingwa, Serikali katika kipindi cha miaka mitano chini ya Rais Dk.John Magufuli wamepokea Sh.bilioni 2.8  na kati hizo Sh.bilioni moja zimetumika katika ujenzi wa vituo vya afya na Sh.bilioni 1.8 kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Songwe.

 

Akizungumzia sekta ya maji , Dk.Magufuli amewapa  Sh.bilioni 5.2  na hiyo ni katika kipindi cha miaka mitano tu."Huko nyuma hatukuwahi kupata fedha kwa kiwango hicho kwani ndani ya miaka 15 walipata Sh.bilioni mbili tu.Kutokana na fedha hizo za miradi ya maji kati ya vijiji 43 walivyonavyo vimebakia vijiji 15 ambavyo havina maji.Tumepewa fedha na miradi inaendelea kutekelezwa,"amesema Mulugo.

Kuhusu barabara , amesema katika kipindi cha miaka mitano Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya barabara na kwa eneo la Mkwajuni inajengwa barabara ya kilometa 1.5 ambapo wamepata fedha kutoka Wakala wa Barabara Vijijini(TARURA) pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania(TANROADS).

Wakati katika elimu amesema Songwe wamepata Sh.bilioni 4.2 kwa ajli ya elimu bila malipo pamoja na ujenzi wa miundimbu ya elimu.Kuhusu umeme vijijini umeme vimebaki vijiji 13 tu kati ya vijiji 43.

"Katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu mwaka huu nimeona  vijiji ambavyo vimebakiwa vitawekewa umeme vyote.Tunaposema Dk.Magufuli atashinda kwa kishindo Songwe tunamaanisha kwa yale ambayo ametundea,"amesema Mulugo.

Akizungumzia upande wa mikopo kwa ajili ya kuwawezesha wanawake na vijana , chini ya Dk.Magufuli wamepata Sh.milioni ya makundi  hayo 969 ambazo zimetolewa mikopo kwa makundi hayo.Pia amesema Songwe ni Wilaya changa lakini wamepata Sh.bilioni 3.9 kwa ajili ya kujenga jengo la  utawala la halmashauri.

"Tunamshukuru Dk.Magufuli na Serikali yake kwa namna ambavyo amekuwa na upendo mkubwa na Songwe yetu, ahadi yetu kwake ni kumpa kura nyingi na tunataka Songwe tuongoze kwa kumpa kura nyingi.Kwa upendo wake ametupatia Sh.bilioni 1.4 kwa ajili ya kuwezesha kaya masikini,"amesema Mulugo.

Pia amesema kwa upande wa barabara kazi kubwa imefanyika katika kipindi cha miaka mitano ambapo wananchi ni mashahidi huku akifafanua kuwa tayari Serikali imetangaza kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara inayotoka Mbalizi ,Chang’ombe, Mkwajuni hadi Makongorosi.

"Tumeshapata Sh.milioni 800 kwa ajili ya kufanyika upembuzi yakinifu wa barabara hii.Kwa unyenyekevu mkubwa , ndugu zangu nawaomba tuongoze kwenye kura za Rais wetu Dk.Magufuli katika uchaguzi mkuu mwaka,"amesema Mulugo.


Mgombea Urais kupitia Chama cha Mapinduzi CCM, Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Wananchi Vwawa katika mkutano wa Kampeni za CCM uliofanyika katika uwanja wa Tacri Mbimba mkoani Songwe leo tarehe 01 Oktoba 2020.

 Wananchi wa Vwawa mkoani Songwe wakimsikiliza Mgombea Urais kupitia Chama cha Mapinduzi CCM, Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli wakati akiwahutubia katika uwanja wa Tacri Mbimba mkoani Songwe leo tarehe 01 Oktoba 2020. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad