HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 1, 2020

MAJALIWA: DKT. MAGUFULI ANAYO REKODI NZURI YA KUFANYA KAZI, TUMPE NCHI



 Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwakabidhi nakala ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe, Dotto Biteko, katika mkutano wa kampeni, uliyofanyika katika Kata ya Igulwa, wilayani Bukombe, kwenye mkutano wa kampeni, Oktoba 1, 2020. Katikati ni Mgombea Udiwani Kata ya Igulwa, Richard Mabenga.
Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwahutubia wananchi wa Kata ya Igulwa, wilayani Bukombe, katika mkutano wa kampeni, Oktoba 1, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe, Dotto Biteko (kulia), akinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 kwa wananchi, baada ya kukabidhiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, katika Kata ya Igulwa, wilayani Bukombe, kwenye mkutano wa kampeni, Oktoba 1, 2020. Kulia ni Mgombea Udiwani Kata ya Igulwa, Richard Mabenga. 

Wananchi wa Kata ya Isingiro, wakifurahia hotuba ya Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, wakati akiwahutubia, katika mkutano wa kampeni, uliyofanyika katika Kata ya Igulwa,  wilayani Bukombe, Oktoba 1, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


 

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa wilaya ya Bukombe, mkoani Geita wamchague Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu wanamjua historia yake na anayo rekodi nzuri ya kufanya kazi.

 

"Dkt. Magufuli tunamjua. Alikuwa Waziri katika nchi hii kwa miaka 20. Alikuwa Waziri wa Ujenzi akajenga barabara ambazo sote leo tunaziona. Alipoenda Wizara ya Ardhi, akapiga marufuku ya watumishi wa Wizara hiyo kujilimbikizia viwanja vinne vinne.”

 

Ametoa wito huo leo (Alhamisi, Oktoba mosi, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa Ushirombo katika mkutano uliofanyika kata ya Igulwa, wilayani Bukombe.

 

"Nimekuja kuwaomba kura zenu. Ni lazima tumpe kura mtu ambaye tunaijua historia yake ya kwamba aliwahi kuwa kiongozi na ameweka historia."

 

Amewataka wananchi hao wamchague kiongozi ambaye anaweza kuisimamia Serikali yake. "Usipokuwa makini unaweza kumpa mtu nchi halafu akashindwa kuisimamia nchi. Kiongozi anayefaa, mwenye uwezo wa kuratibu rasilmali zetu na kuzisimamia, si mwingine bali ni Dkt. Magufuli."

 

Amehimiza wakazi hao wawachague wagombea wa CCM ili waweze kuzungumza lugha moja. "Ni muhimu tuwe na madiwani ili waunde Baraza lao la Madiwani, waongee lugha moja na wapeleke hoja zao kwa Mbunge wao."

 

Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko kwenye ziara ya kumuombea kura mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. Magufuli alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Bukombe, Bw. Dotto Biteko na mgombea udiwani wa kata ya Igulwa, Bw. Richard Mabenga.

 

"Dkt. Magufuli amekuwa Rais kwa miaka mitano, aliyoyafanya katika kipindi kifupi tunayaona. Dkt. Magufuli huyu, wala rushwa ndiye kiboko yao. Leo niko mbele yako, bila kujali chama chako cha siasa, ninakuomba umpigie kura Dkt. Magufuli. Niko mbele yenu, ninawaomba kura za wagombea wa CCM," amesisitiza.

 

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema wilaya ya Mbogwe imetengewa sh. bilioni 3.9 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za Makao Makuu ya Wilaya hiyo.

 

Akielezea kuhusu sekta ya maji, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imetoa fedha kwa ajili ya uboreshaji wa miradi ya maji ikiwemo mradi wa maji Kabanga – Nhomolwa ambao ulipatiwa sh. bilioni 1.2. “Fedha nyingine zilizotolewa ni shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji Mbogwe ambao utanufaisha maeneo ya Kasosobe, Bwelwa na Iboya.”

 

Amesema upanuzi wa mradi wa maji Nyakafuru umepatiwa sh. milioni 633 ambao utanufaisha maeneo ya Lulembela na Nyakafuru, Shinyanga A & B pamoja na usimikaji wa nguzo za umeme huko Nyakafuru, Shenda na Masumbwe.

 

Mheshimiwa Majaliwa amemaliza ziara yake mkoani Geita na anaendelea kutafuta kura katika Mkoa wa Shinyanga.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad