HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 1, 2020

Balozi Seif afanya ziara katika ofisi za Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na udhibiti Dawa za Kulevya

 

 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwapongeza Watendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya kwa kazi kubwa ya kudhibiti Janga la Dawa za Kulevya Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Viongozi Waandamizi wa Kiserikali alipofanya ziara fupi kwenye Ofisi ya Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar iliyopo Migombani Mjini Zanzibar.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar Bibi Kheriyangu Mgeni Khamis Kulia akimkaguza Balozi Seif Ali Iddi sehemu mbali mbali za Vitengo vya Ofisi yake.
 Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mohamed akifafanua jambo wakati wa ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwenye jingo la Tume ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Picha na – OMPR – ZNZ.

 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kazi kubwa inayoendelea kutekelezwa kwa pamoja kati ya Watendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na udhibiti Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na Vyombo vya Dola imesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa wimbi la uingizwaji wa Dawa za Kulevya Nchini.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati alipofanya ziara fupi ya kuwatembelea Watendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na udhibiti Dawa za Kulevya waliohama kutoka Kidongo Chekundu kutokana na ufinyu wa Ofisi na hivi karibuni kuhamia kwenye Jengo jengine liliopo Migombani Mjini Zanzibar.

Alisema Serikali Kuu iliamua kukaza kamba katika mapambano yake dhidi ya janga la Dawa za Kulevya ambalo ni hatari kwa Afya za Vijana wanaojihusisha na matumizi ya Dawa hizo ambazo matokeo yake hupelekea kupunguza nguvu kazi ya Taifa.

Balozi Seif alieleza kwa mujibu wa Sheria Nambari 9 ya Mwaka 2009 ni kosa kwa mmiliki, mkaazi au msimamizi wa Nyumba, jengo au mahali popote kuruhusu kutumika katika kutayarisha Dawa za Kulevya kwa ajili ya matumizi au kutengeneza, kuzalisha, kusambaza na kuuza.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitahadharisha wazi kwamba wapo baadhi ya Watu katika harakati zao za kimaisha wameamua kujihusisha na biashara ya Dawa za Kulevya bila ya kujali kwamba bidhaa yao inayokwenda kwa watumiaji wa kilevi hicho hatimae huathirika Kiafya na kushindwa kujitegemea kimaisha.

Balozi Seif aliwapongeza Watendaji wa Tume hiyo ya Kitaifa ya Kuratibu na udhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar kwa kazi kubwa wanayoifanya licha ya kuzunguukwa na mazingira magumu.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar Bibi Kheriyangu Mgeni Khamis alisema ipo faraja kubwa kwa Watendaji wake kupata Ofisi nyengine kubwa itakayowapa nafasi kubwa ya kufanya Kazi zao kwa ufanisi mkubwa.

Bibi Kheriyangu alisema licha ya kuhamia kwenye jengo hilo lakini kinachosubiriwa kwa sasa kwa jiengo hilo ni kufanyika kwa marekebisho kwa mujibu wa maelekezo ya Wakala wa Ujenzi chini ya usimamizi wa Wafanyakazi wahandisi Wazalendo.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana ya udhibiti wa uingizaji, usambazaji na uuzaji wa Dawa za Kulevya hapa Nchini.

Bibi Kheriyangu alisema katika kuhakikisha kwamba jukumu hilo linafikia mafanikio ya juu tayari ipo miongozo iliyoandaliwa ya namna ya kuelekeza taratibu za kupiga vita janga hilo thakili lililopoteza nguvu kazi ya Taifa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad