
Mgombea
Mwenza wa CCM na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akizungumza na
wananchi waliojitokeza kwenye uzinduzi wa awamu ya tatu ya Kampeni za
chama hicho wilayani Kongwa leo.

Mbunge Mteule wa Kongwa na Spika wa Bunge,Job Ndugai akihutubia kwenye kampeni za CCM katika eneo la Mkoka wilayani Kongwa.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akizungumza katika mkutano wa kampeni katika eneo la Mkoka wilayani Kongwa, Dodoma.

Mbunge
wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Alhaji
Adam Kimbisa akiwapungia mkono wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wa
kampeni katika eneo la Mkoka wilayani Kongwa ambapo chama hicho
kimezindua awamu ya tatu ya kampeni zake.

Mjumbe
wa Kamati Kuu ya CCM na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda akisalimiana
na Mgombea Ubunge wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam
Ditopile walipokutana kwenye uzinduzi wa awamu ya tatu ya kampeni za CCM
leo.
Charles James, Michuzi TV
CHAMA
cha Mapinduzi CCM leo kimezindua kampeni zake kwa awamu ya tatu huku
ikisema wana uhakika wa kuibuka na ushindi kwenye kura za Urais, Wabunge
na Madiwani kwa asilimia 89.
Uzinduzi
huo umefanyika katika eneo la Mkoka wilayani Kongwa ambapo mgeni rasmi
Mgombea Mwenza na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan na
kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa chama hicho,
Dk Bashiru Ally, Spika wa Bunge na mbunge mteule wa Kongwa, Job Ndugai.
Akizungumza
katika mkutano huo, Mama Samia amewaomba watanzania kujitokeza kwa
wingi Oktoba 28 kwenda kupiga kura kwa wagombea wa CCM ili kutengeneza
mafiga matatu yatakayowatumikia kwa miaka mitano mingine.
Amesema
imani waliyopewa kwa miaka mitano na wananchi imewafanya wafanye kazi
kubwa ya kuwatumikia na kuomba waiamini tena CCM kwa kipindi kingine cha
miaka mitano.
"
Tumefanya mambo makubwa sana hapa Kongwa na Tanzania kwa ujumla, hakuna
eneo ambalo halijaguswa tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza
changamoto na kufanya maboresho kwenye nyanja mbalimbali.
Leo
hii Kongwa kila kijiji kina umeme, na awamu ijayo tumepanga kuhakikisha
kila nyumba inakua na umeme, sekta ya afya, miundombinu, elimu na
nishati. Mkituamini na kutuchagua tena tutafanya zaidi ya awamu ya
kwanza," Amesema Mama Samia.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu, Dk Bashiru Ally amesema uzinduzi huu wa awamu
ya tatu una mikakati Maalum kuliko awamu mbili ile ya kwanza Dodoma na
ya pili iliyozinduliwa mkoani Kagera.
Amesema
awamu ya nne wataizindua visiwani Zanzibar na wanazo awamu sita tofauti
ambazo zimebeba mikakati na mbinu mahususi za kushinda uchaguzi huo.
"
Nasikia wenzetu wanataka kuvua jezi wavalishane jezi moja, wanaangaika
kama wendawazimu, wamepagawa na kuchanganyikiwa, sisi kazi ni moja tu
kuwashinda bila kujali udhaifu wao.
Kila
siku tuna mikutano 20 ya kampeni kitaifa kwa maana ya Mgombea Urais,
Mgombea Mwenza na Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,
tuna mikutano 600 kila siku ya Wabunge na Madiwani, wenzetu hata
hawaeleweki walipo, ni dhaifu kuliko nyakati zote," Amesema Dk Bashiru.
Nae
Mbunge wa Kongwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai amemuahidi Mama Samia
kuwa Kongwa itaongoza kwa kura kwa asilimia 100 na wala hakuna kura
itakayoenda upinzani.
No comments:
Post a Comment