HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, July 7, 2020

WAKULIMA JIFUNZENI UHIFADHI BORA KUEPUKA SUMUKUVU KWENYE MAZAO-BASHE


Naibu Waziri Kilimo Hussein Bashe akitazama mahindi yaliyo shambani ambayo tayari yameanza kuathiriwa na wadudu katika kijiji cha Engusero wilaya ya Kiteto jana wakati alipofungua mafunzo ya wakulima kudhibiti sumukuvu.
Naibu Waziri Kilimo Hussein Bashe ( aliyeinama) akitazama mahindi yaliyowekwa chini ya ardhi katika makazi ya mkulima kijiji cha Engusero wilaya ya Kiteto na kuwa katika hatari ya kupata fangasi wanaosababisha sumukuvu.Lengo la ziara hiyo ni kutoa elimu ya udhibiti wa sumukuvu kwa wakulima.
Afisa Kilimo toka wizara ya Kilimo Magret Natai (kushoto) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe wakati alipotembelea shamba la mkulima kuzindua mafunzo ya udhibiti tatizo la sumukuvu kwenye mazao kijiji cha Engusero wilaya ya Kiteto jana.
Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Engusero wilaya ya Kiteto wakifuatilia mkutano wa mafunzo ya kudhibiti tatizo la sumukuvu yanayotolewa na mradi wa TANIPAC chini ya wizara ya Kilimo .
Naibu Waziri Kilimo Hussein Bashe (kulia) akisalimiana na mkulima (bibi ) wakati alipomkabidhi zawadi ya mfuko bora wa kuhifadhia nafaka katika kijiji cha Engusero wilaya Kiteto jana.Kushoto aliyeshika mfuko ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Usalama wa Chakula Dkt.Honest Kessy
(Picha na Habari Wizara ya Kilimo)

………………………………………………………………………

Serikali imesema katika kuhakisha tatizo la sumukuvu kwenye mazao ya wakulima linapatiwa ufumbuzi elimu kwa wakulima ni muhimu kutolewa.

Kauli hiyo imetolewa leo wilayani Kiteto na Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alipofungua mafunzo ya udhibiti sumukuvu kwa wakulima wa kijiji cha Engusero kwa niaba ya vijiji vingine 28.

Bashe amesema wakulima wanapaswa kuelimishwa zaidi kutambua namna ambavyo mazao yao hususan mahindi na karanga yanavyoweza kuchafuliwa na sumukuvu ili waweze kudhibiti kwani tatizo hili linasababisha hasara kwa mazao yao na pia afya za binadamu.

Bashe alipongeza mradi wa kudhibiti sumukuvu (TANIPAC) kwa kuandaa mafunzo hayo kwa wakulima ili watambue namna sahihi ya kukabiliana na tatizo la sumukuvu.

“ Mkulima ndio mgani namba moja,hivyo ukimfundisha kanuni bora za kilimo ataweza pia kuwafundisha wakulima wenzake” alisisitiza Bashe

Naibu Waziri Bashe aliongeza kusema kuwa wakulima kupitia mradi wa TANIPAC watajifunza kutambua namna mazao yao yanavyoweza kuchafuliwa na fangasi wanaosababisha sumukuvu katika vijiji vyao ikiwemo kutoweka mahindi chini ya ardhi.

Akiwa katika ukaguzi wa shamba la mfano la mahindi kijiji cha Engusero Naibu Waziri huyo alijionea jinsi mahindi yalivyoanza kuharibiwa na wadudu kufuatia kuchelewa kuvunwa na kuagiza kuwa wataalam wa wizara waandae kalenda ya Kilimo

“TANIPAC andaeni kalenda ya Kilimo ikionesha mkulima aanze lini kupanda,kupalilia,kuweka mbolea na muda gani ni muaka kuvuna mahindi .Hii ikifanyika itapunguza mathara kwa wakulima wa Kiteto na maeneo mengine kulingana na ikolojia” alisema Bashe

Alisema serikali pia itajenga kituo cha umahiri eneo la Kibaigwa kwa lengo la kuwasaidia wakulima wengi zaidi kupata taaluma ya shughuli za Kilimo “VETA ya Kilimo”

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa kudhibiti Sumukuvu Clepin Josephat alisema mafunzo hayo yanafanyika katika wilaya nne za Kiteto, Babati, Kondoa na Chemba ambapo wanalenga kuwafikia wakulima 1400 katika siku nane za mafunzo hayo

Clepin aliongeza kuwa mradi huo utajenga ghala la kisasa la kuhifadhia mazao ya nafaka litakalokuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 2000 katika kijiji cha Engusero wilaya ya Kiteto lenye ukubwa wa ekari 10,000.

“ Tunapaswa kuamini kuwa madhara ya sumukuvu yapo,tujitokeze kupata elimu.Fangasi wa kuvu wanaishi ardhini wakulima epukeni kuweka mahindi na karanga chini baada ya kuvuna ili wadudu wasiweze kuathiri mazao yenu ” alisema Clepin

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Bashe alikagua shamba la mkulima wa mahindi na kisha aliongea na wananchi wa kijiji cha Engusero ambapo walielezea kero ya bei ya mbegu za mahindi na alizeti kuwa zipo juu hivyo wakulima kushindwa kuzinunua.

Katika hatua nyingine Bashe aliagiza kuwa Wakurugenzi wa Halmashauri nchini ambapo miradi ya TANIPAC inafanyika watoe ardhi bure bila kudai fidia kama ilivyofanyika kwa wilaya ya Kiteto

“ Hakuna kulipa fidia kwa miradi ya TANIPAC ,hivyo halmashauri itakayodai fidia ya ardhi ondoeni mradi na kupeleka wilaya nyingine” alisisitiza Naibu Waziri Bashe.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto Tamimu Kambona aliwasihi wakulima wanaoshiriki mafuzo kutokwepa gharama katika kuhifadhi mazao yao ili yasichafuliwe na sumukuvu hali itakayoathiri upatikanaji bei nzuri sokoni.

“ Tatizo kwenye wilaya yetu ya Kiteto lipo kubwa na linasababisha hasara sana kwa wakulima hivyo lazima tuwafundishe wakulima kanuni bora za Kilimo na kuepuka sumukuvu “ alisema Kambona

Wilaya ya Kiteto katika msimu huu inatarajia kuvuna mahindi tani 270,000 tofauti na tani 160,000 za msimu wa 2019/20 kutokana na uwepo wa hali ya hewa nzuri na usimamizi wa wataalam wa Kilimo. Mwisho

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad