WANANCHI KIJIJI CHA MKONGOGULIONI WANUFAIKA NA UJENZI WA MRADI WA MAJI WA RUWASA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, 7 July 2020

WANANCHI KIJIJI CHA MKONGOGULIONI WANUFAIKA NA UJENZI WA MRADI WA MAJI WA RUWASA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme kushoto,akimtiwisha ndoo ya maji mkazi wa kijiji cha Mkongo Idna Ngonyani mara baada ya Mkuu wa mkoa kufungua moja kati ya vituo vya kuchotea maji katika kijiji hicho ikiwa ni utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji inayojengwa na wakala wa maji vijijini Ruwasa wilayani Namtumbo.
Mkuu wa mkoa wa RUvuma Christina Mndeme kulia akicheza kwa furaha na baadhi ya wanawake wa kijiji cha Mkongo wilayani Namtumbo mara baada ya kufungua kituo cha kuchotea maji kijijini hapo kilichojengwa na wakala wa maji vijijini Ruwasa wilaya ya Namtumbo,Mkuu wa mkoa yupo katika ziara ya kukagua nakutembelea miradi mbalimbali ya maji katika wilaya zote tano za mkoa huo. Picha na Mpiga Picha Wetu

……………………………………………………………………….

Na Mwandishi Wetu,RUVUMA

WANANCHI wa Kijiji cha Mkongogulioni wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, wameanza kunufaika na matunda ya Serikali yao ya awamu ya tano baada ya wakala wa maji vijijini Ruwasa kukamilisha ujenzi wa mradi mkubwa wa maji.

Wakizungumza mbele ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme baadhi ya wananchi hao walisema, kijiji chao hakijawahi kupata maji ya bomba kwa muda mrefu,lakini Serikali ya awamu ya tano imefanikiwa kupeleka maji ya bomba baada ya miaka 59.

Hidna Ngonyani(43) Hassan Makalani walisema,kukamilika kwa mradi wa maji ni faraja kubwa hususani wanawake ambao walikuwa wanaangaika na kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji kwenye mito na madimbwi ambayo maji yake sio safi na salama.

Hidna Nyongani, ameishukuru serikali kwa kukamlisha mradi huo ambao hawakufikiria kama utakamilika haraka kutokana na mkandarasi wake Kipera Contractors Co Ltd kusua sua huku wakazi hao wakiendelea kukabiliwa na kero kubwa ya maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya kila siku.

Aidha alisema,kupatikana kwa huduma ya maji katika kijiji chao inakwenda kuimarisha ndoa ambazo ziliyumba kutokana na waume zao kukosa imani pale wanawake wanapochelewa kurudi nyumbani kutoka kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya familia.

“tunamshukuru sana Serikali yetu ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wetu John Magufuri kwa kutujali sisi wananchi wake,tunakuomba Mkuu wa mkoa tufikishie shukurani zetu za upendo kwake,tunahaidi kutumia maji haya kuharakisha maendeleo katika kijiji chetu”alisema Ngonyani.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ameipongeza Ruwasa wilaya na mkoa kwa kusimamia vizuri mradi huo na kuwataka wananchi wa Mkongogulioni kutunza miundombinu yake na kutumia maji hayo kujiletea maendeleo.

Mndeme alisema, mradi wa maji Mkongogulioni ni kati ya miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano,kwa hiyo wananchi wa kijiji hicho hawana budi kumshukuru Rais Dkt John Magufuri kwa upendo wake mkubwa na kukubali kutoa fedha ambazo zimekamilisha mradi huo.

Alisema, Serikali itaendelea kuboresha huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo barabara,elimu,afya na maji ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo na wananchi wapate muda mwingi wa kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo na kujikwamua na umaskini.

Kwa mujibu wa Mndeme,Serikali imeipatia wilaya ya Namtumbo kiasi cha shilingi bilioni 13 ambazo zinakwenda kukarabati,kujenga na kuimarisha huduma ya maji kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Mndeme, amempa mwezi mmoja meneja wa Ruwasa wilaya ya Namtumbo kuhakikisha vituo vyote 30 vya kuchotea maji viwe vinatoa huduma hiyo badala ya vituo 17 vya sasa ili kutosheleza mahitaji ya maji katika kijiji hicho ambacho kina idadi kubwa ya watu.

Naye meneja wa Ruwasa wilaya ya Namtumbo David Mkondya alisema,mradi wa maji katika kijiji cha Mkongogulioni Nahimba unatekelezwa chini ya usimamizi wa program ya maendeleo ya Sekta ya maji ya maji(WSDP)kupitia program ndogo ya maji na usafi wa mazingira vijijini(RWSSP).

Alisema, mradi huo ulisainiwa kwa mara ya kwanza mwaka 2013 na utekelezaji wake ulianza mwaka 2017 na ulitarajiwa kukamilika mwezi Februari 2020 chini ya mkandarasi Kipera Contractors& General Supplies Co Ltd ya Songea.

Alimweleza Mkuu wa mkoa kuwa, mradi wa maji Mkongogulioni Nahimba unakusudiwa kuhudumia wananchi wapatao 8007 katika vijiji vya Mkongogulioni, na Nahimba kwa gharama ya shilingi bilioni 2,069,975.521 ambapo hadi sasa fedha zilizotumika kutekeleza mradi huo ni shilingi bilioni 1,387,965,270.40.

Mkondya alisema,mradi huo unatekelezwa kwa awamu moja ambapo kazi zilizopangwa kufanyika ni ujenzi wa tanki la lita 25,000 katika kijiji cha Nahimba na ukarabati wa matenki mawili yenye ujazo wa lita 150,000 kijiji cha Mkongo na lita 25,Kijiji cha Nahimba.

Alitaja kazi nyingine zilizotarajiwa kufanyika ni pamoja na kujenga chanzo kimoja cha kukusanya maji(Intake),ununuzi wa mabomba ya laini kuu na laini ya usambazaji maji,kuchimba mtaro na kulaza mabomba km 15 na laini ya usambazaji maji km17.84. ujenzi wa vituo 46 vya kuchotea maji.

Kwa mujibu wake,hadi sasa kazi zilizofanyika ni uchimbaji wa mtaro na ulazaji wa bomba za kusambaza maji kijiji cha Nahimba,ujenzi wa matenki ya kuhifadhia maji,ujenzi wa chanzo,ulazaji wa bomba kuu na vituo 46 vya kuchotea maji.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad