HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 9 January 2019

MWANRI AAGIZA UCHUNGUZI KWENYE UJENZI WA TENKI LA MAJI KATIKA KIJIJI CHA IBELAMILUND WILAYANI UYUI

Na Tiganya Vincent, Tabora
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri amesitisha kwa muda siku mbili kuendelea na ujenzi wa tenki ya ujazo wa lita laki tatu uliokuwa ukiendelea katika Kijiji cha Ibelamilundi wilayani Uyui baada ya kuzuka utata wa idadi ya nondo zilizokuwa zikitakiwa katika mzuko wake ambao unasababisha uduni wa ubora.

Hatua hiyo inalenga kutuma timu ya wataalamu ambao watakaochunguza kama ujenzi wake umezingatia maagizo yaliyopo kwenye ramani ya ujenzi na uko katika ubora unaotakiwa.

Mwanri ametoa kauli hiyo wilayani Uyui baada ya kauli za wataalamu kutofautiana na idadi ya nondo ambazo zimeshawekwa katika tenki hilo zikisubiri umwagaji wa zege

Alisema katika maelezo ya mkandarasi na takwimu zilizopo katika ramani zilionyesha kuwa tenki hilo lingechukua nondo 170 kukamilisha mzunguko lakini baada ya kuziheshabu zilikutwa 125.

Mwanri alisema ili kuepuka kujengewa tenki lililo chini ya kiwango ni vema wataalamu wapitie na kudhiirisha kuwa idadi ya nondo zilizosukwa katika tenki hilo zitatoa tenki bora.

Alisema likijengwa tenki chini ya kiwango cha matakwa ya michoro ya kihandisi linaweza kusababisha Serikali kupata hasara na kuwa na uwezekano kutokea maafa kama likipasuka kutokana na kutokuwa na ubora uliokusudiwa.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa alimtaka Mhandisi Mshauri wa mradi huo akiwa kama msimamizi Mkuu wa Serikali katika ujenzi wa mradi huo  kuhakikisha kazi inayofanyika inakuwa na ubora unaotakiwa na inalingana na fedha zilizolipwa.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema timu hiyo halitachukua muda mrefu ili kuhakikisha ujenzi wa mradi huo unaendelea na  kukamilika kwa muda ulipangwa.

Katika hatua nyingine Mwanri aliwataka wakazi wa maeneo yote ambayo mradi hiyo ya kuleta maji kutoka ziwa Victoria inatekelezwa kuhakikisha wanalinda vifaa vya Wakandarasi kwa kuwafichua watu wachache wenye tabia mbaya za wizi ili kutokuwa kikwazo cha kukamilisha mradi kwa wakati.

Alitoa kauli hiyo kufuatia malalamiko ya uwepo wa wizi wa nondo na saruji katika mradi wa  ujenzi wa tanki la Nzega mjini.

Mwanri aliwaagiza Polisi kuhakikisha wanaimarisha ulinzi na kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kuhusika na kuhujumu mradi kwa kuiba vifaa vya wakandarasi,

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Said Ntahodi alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli kwa kuwapelekea mradi wa maji katika Wilaya ya Uyui kutoka ziwa Victoria.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuwapunguzia adha ya kutafuta maji kwa watumishi na wananchi wa  maeneo ambayo mradi huo utapita na hivyo kuwapunguzia gharama za kutumia fedha nyingi kutafuta maji.

Ntahodi alimuomba Mkuu wa Mkoa wa Tabora kuwafikishia shukurani zao kwa Rais Magufuli kwa kutekeleza ahadi yake ya kuwaondolea shida ya maji wakazi wa Isikizya na maeneo mengine ya Uyui.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi Tabora(TUWASA) Mukama Bwire alisema kuwa jumla ya vijiji 33 vilivyopo kando kando ya barabara kutoka Nzega hadi Tabora watanufaika na huduma ya maji safi na salama mara baada ya kukamilika mradi huo.
  Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri (aliyechumaa) akipima upana wa nondo zilizotandazwa chini ya mradi wa ujenzi wa tenki la maji katika Kijiji cha Ibelamilundi wilayani Uyui wakati wa ziara yake na Kamati ya Ulinzi na Usalama kutembelea mradi wa maji wa ziwa Victoria.
  Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri (katikati) akiwa ameshika nondo zilizoleta utata kabla ya kuanza zoezi za kuzihesabu ili kuona kama idadi yake inawiana na ile iliyopo katika mchoro wa ujenzi wa tenki la maji katika Kijiji cha Ibelamilundi wilayani Uyui wakati wa ziara yake na Kamati ya Ulinzi na Usalama kutembelea mradi wa maji wa ziwa Victoria.
 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri (katikati) akipima upana wa nondo zilizosukwa kwenye  mradi wa ujenzi wa tenki la maji katika Kijiji cha Ibelamilundi wilayani Uyui wakati wa ziara yake na Kamati ya Ulinzi na Usalama kutembelea mradi wa maji wa ziwa Victoria.
 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri (katikati) akiwa katika zoezi la kuhesabu nondo nyembamba zilizosukwa kwenye mradi wa ujenzi wa tenki la maji katika Kijiji cha Ibelamilundi wilayani Uyui wakati wa ziara yake na Kamati ya Ulinzi na Usalama kutembelea mradi wa maji wa ziwa Victoria. Picha na Tiganya Vincent
 Nondo za ujenzi wa tenki la maji katika Kijiji cha Ibelamilundi wilayani Uyui ambazo zimesababisha mashaka na kumfanya Mkuu wa Mkoa wa Tabora kusitisha kwa muda wa siku mbili kuendelea ya ujenzi hadi hapo timu ya wataalamu kutoka Mkoani watakaidhinisha kuwa idadi yake inalingana na zile zilizopo katika michoro.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad