HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 14 December 2018

SERIKALI KUZISHUSHIA RUNGU TAASISI ZISIZOJIUNGA NA MFUMO WA GePG IFIKAPO JUNI 30, 2019

Na Josephine Majura na Peter Haule WFM, Dodoma
Serikali imezitaka taasisi zote ambazo bado hazijajiunga na Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali (GePG) kuhakikisha wamejiunga na mfumo huo kabla ya  Juni 30, 2019.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatib Kazungu, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Doto James, wakati wa Mkutano wa mwaka wa  wadau wa utumiaji wa mfumo wa GePG Jijini Dodoma.  

Dkt. Kazungu, alisema kuwa hakutokuwa na fedha yoyote ya umma itakayokusanywa nje ya Mfumo wa GePG, hivyo wakati mwafaka wa kujiunga na kuunganishwa  na mfumo huo ni sasa. “Napenda kusisitiza kuwa, ni lazima kutumia mfumo huu kwa kuwa unaongeza ufanisi na uwazi katika ukusanyaji wa Fedha za Umma na pia utaratibu wa matumizi ya  GePG unatoa fursa ya kuwa na njia nyingi za kulipia na kuwapa walipaji wa huduma za Serikali utaratibu rafiki wa kufanya malipo”, alieleza Dkt. Kazungu.

Utaratibu wa makusanyo kabla ya mfumo wa GePG haukua rafiki kwa kuwa ilikuwa ni vigumu kuthibitisha malipo na pia  kuwa na foleni ndefu kwenye Ofisi za Serikali zilizosababishwa na zoezi la kufanyiwa tathmini ya malipo ya huduma na kuthibitisha malipo. Alisema ili kukabiliana na changamoto hizo katika ukusanyaji wa Fedha za Umma, Juni 2017, Serikali iliifanyia marekebisho Sheria ya Fedha za Umma (PFA) ya mwaka 2001 na kuongeza kipengele kinachotaka Fedha zote za umma zikusanywe kupitia Mfumo wa Government e-Payment Gateway (GePG).

Lengo la kuanzishwa kwa GePG ni kutatua changamoto zilizopo kwenye Mfumo uliokuwepo wa ukusanyanji wa fedha za umma ili kuongeza uwazi na udhibiti wa fedha za umma, kuboresha na kurahisisha namna ya kulipia huduma za umma na pia kupunguza gharama zinazoambatana na ukusanyaji wa fedha hizo ambapo mfumo huo ulianza kutumiwa rasmi na taasisi za umma mwezi Julai 2017 baada ya majaribio yake kukamilika.

Alisema kuwa utaratibu GePG unaenda sambamba na utekelezaji wa maelekezo mengine ya Serikali yanayohusu makusanyo ikiwemo yale yanayotaka akaunti kuu za makusanyo za taasisi za umma kuwepo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hivyo ni lazima kuhakikisha akaunti za Taasisi za ummaa za makusanyo zilizoko Benki Kuu zimewasilishwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya fedha na mipango ili ziunganishwe na GePG.

Mpaka sasa takribani Benki kumi na moja (11) na mitandao sita(6) ya malipo kwa njia ya simu za kiganjani zimeshaunganishwa na mfumo huo. Dkt. Kazungu alisema kuwa ni vyema taasisi za Serikali kuwa na akaunti za makusanyo kwenye benki zaidi ya moja kati ya benki zilizoungwa na GePG ili kuwarahisishia walipaji wa huduma za serikali kwa kuwa malipo yote yanayopitia GePG hayatozwi ada za miamala na benki hizo, hivyo kuongeza akaunti za makusanyo hakutoongeza gharama za miamala kwa taasisi za umma.

Alibainisha kuwa kutekelezwa kwa rai hiyo kutaondoa hatari ya taasisi ya umma kukosa huduma ya malipo endapo benki inayotumiwa itashindwa kutoa huduma kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuvunja makubaliano ya namna ya kuzihudumia akaunti zilizounganishwa kwenye mfumo.

Naibu Katibu Mkuu Kazungu amewataka wajumbe wa mkutano huo kuwa chachu katika kuboresha utendaji kwa vitendo kwa kutoa huduma nzuri kwa wananchi zinazohusisha ukusanyaji wa Fedha za Umma katika maeneo yao ya kazi baada ya kumalizika kwa mkutano huo.

Kwa upande wake Mkurungezi wa Mifumo ya Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. John Sausi, alisema kuwa mfumo huo umekuwa na tija tangu ulipoanzishwa kwa kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha inaweza kuona makusanyo yote yanayoingia hivyo kuongeza ufanisi wa upatikanaji wa mapato, uwajibikaji na uwazi.

Alisema kuwa, jumla ya Taasisi 326 zimeunganishwa na Mfumo wa GePG na miongoni  mwa Taasisi hizo ni Wakala wa Misitu, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)

Amezitaja changamoto za Mfumo huo kuwa ni pamoja na Benki 11 tu ndizo zinazotumia mfumo huo kati ya Benki zaidi ya 50, hivyo kuleta mkanganyiko kwa wadau wanaotumia  mfumo huo.

Mkutano wa wadau wote wanaotumia Mfumo wa GePG ni wa kwanza kufanyika nchini ukiwa na lengo la kubaini na kutatua changamoto za mfumo huo tangu ulipoanzishwa.
 Mkurugenzi wa Mifumo ya Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. John Sausi, akieleza kuhusu bidhaa mpya zitakazo wasilishwa kwa wadau wa mfumo wa ukusanyaji mapato (GePG) wakati wa Mkutano wa wadau hao uliofanyika katika ukumbi wa Kambarage Jijini Dodoma.
 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu ambaye ni mgeni rasmi akifungua mkutano wa wadau wa mfumo wa ukusanyaji mapato (GePG) wa uliofanyika katika ukumbi wa wa Wizara ya Fedha na Mipango (Kambarage) Jijini Dodoma.
 Meza kuu ikiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu (katikati) wakifuatitia kwa makini maelezo ya wadau wa mfumo wa ukusanyaji mapato (GePG), Jijini Dodoma
 Baadhi ya Washiriki wa mkutano wa mwaka wa mfumo wa ukusanyaji mapato (GePG), wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu (hayupo pichani), uliofanyika katika ukumbi wa Kambarage Jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu ambaye ni mgeni rasmi akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mkutano wa mwaka wa watumiaji wa mfumo wa ukusanyaji mapato uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Kambarage Jijini Dodoma. (Picha na Josephine Majura MoFP Dodoma)No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad