HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 14 December 2018

HUDUMA YA KUUNGANISHIWA MAJI NI KWA MKOPO- CEO DAWASA

Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja akizungumza na wanahabari (hawapo pichani).

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
MAMLAKA ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) imewataka wananchi wa mtandao mpya kujiunga na huduma ya maji safi kwani kwa sasa inatolewa kwa mkopo.

Hayo yamesemwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja wakati wakuelezea mikakati ya mamlaka hiyo iliyofanyika na iliyopo ndani ya siku 100 za DAWASA mpya.

Luhemeja amesema, lengo la kuunganishwa kwa mkopo ni kuhakikisha wanaunganisha wateja wapya 60,000 katika eneo la Salasala na eneo lililopo kati ya Kiluvya, Mbezi na Bagamoyo.

Amesema, ili kunufaisha wakazi wengi zaidi, wananchi wanakumbushwa kuwa huduma ya kuunganishiwa maji inatolewa kwa mkopo na watakubaliana na ofisi za mkoa husika katika ulipaji kama ni miezi sita au mwaka.

"Tunawakumbushwa wateja walio katika mtandao mpya ambao ni maeneo ya Salasala, Kiluvya, Mbezi na Bagamoyo kwenda katika ofisi za DAWASA za Mkoa kwa ajili ya kuweza kufahamu utaratibu na kujiunga na huduma ya maji safi na salama kwa mkopo na malipo yatakuwa ni makubaliano kama ni miezi sita au mwaka,"amesema Mhandisi.

Luhemeja ameeleza kuwa, katika kuunganishiwa kwa mteja mpya vifaa vyote vya kufanya maunganisho mapya kama mabomba, viungo na mita vipo na uchimbaji wa mitaro kwa ajili ya kulaza mambomba vyote vinafanywa na DAWASA.

Amesisitiza kuwa, wananchi wasichangishwe kwa ajili ya kazi hiyo, pia wapate maelezo kamili kutoka kwa ofisi za DAWASA za mkoa zilizopo maeneo tofauti na zaidi akitaja nyaraka watakazotakiwa kwenda nazo ni pamoja na barua ya utambulisho kutoka serikali ya mtaa, picha ndogo mbili (passport size) na nakala ya kitambulisho.

Pamoja na hilo, DAWASA imefanikiwa kurejesha wateja wa zamani 434 waliokatiwa maji kutokana na madeni sugu na kwa sasa wameingia makubaliano ya wateja hao kulipa madeni yao kidogo kidogo.

1 comment:

  1. Kazi inafanyika na inaonekana kikubwa ni wananchi Wa maeneo tajwa kuchangamka na fursa hii ya Siku mia moja za DAWASA Mpya. by LAZARO NGORO WATISA

    ReplyDelete

Post Bottom Ad