HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, December 14, 2018

CHANELI MPYA YA UTALII YA TBC IITWAYO TANZANIA SAFARI KUWASHWA KESHO

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa, anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika sherehe za uzinduzi wa Chaneli mpya ya Utalii,  Tanzania Safari Channel, utakaofanyika katika studio za TBC, Mikocheni, Jijini Dar es Salaam tarehe 15/12/2018 kuanzia saa 2.30 asubuhi.
Chaneli ya Safari ambayo imeanzishwa kwa ushirikiano wa TBC na wadau wengine wa utalii wakiwemo Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Uhifadhi Ngorongoro (NCAA) na Bodi ya Utalii Tanzania, itaanza kurusha vipindi vya majaribio kuanzia siku hiyo ya uzinduzi.

Mchakato wa kuanzisha chaneli hii ulihusisha pia mikutano na wadau wa sekta binafsi ambao shughuli zao zinahusiana na masuala ya utalii.
Aidha, Tanzania Safari Channel ambayo lengo lake ni kutangaza vivutio vya utalii nchini itarusha matangazo yake kutokea Mikocheni kwa muda na hatimaye itahamia Dodoma baada ya jengo la TBC Makao Makuu kujengwa.
Hivyo Chaneli mpya ya Utalii inatarajiwa:

a) Kuongeza uelewa kwa wananchi na jumuia ya kimataifa kuhusu vivutio vya utalii vinavyopatikana Tanzania kwa mfano wanyama pori, maeneo ya kihistoria, maeneno mahsusi ya kijiografia, mimea na wanyama ili kuongeza pato la Taifa litokanalo na utalii;
b) Kuongeza uelewa kwa wananchi na jumuia ya kimataifa kuhusu maeneo ya uwekezaji kiutalii;
c) Kuhamasisha utalii jamii ili kuwezesha jamii zinazozunguka maeneo ya utalii kunufaika na huduma za utalii;
d) Kuhamasisha uhifadhi wa mazingira ya asili na utamaduni kwa ajili ya uchumi endelevu;
e) Kuwahamasisha watanzania kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Nchini; 

Mwaka 2016, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) lililishirikisha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) katika wazo la kuanzisha Chaneli ya televisheni kwa ajili ya kutangaza Utalii Nchini na nje ya Nchi. TANAPA walisema wao wasingeliweza kuanzisha Chaneli ya Televisheni peke yao kwa sababu uendeshaji wa chombo cha habari haikuwa moja ya majukumu ya Shirika hilo. 

Wazo hili lilipata msukumo mkubwa wakati Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, alipozuru TBC tarehe 16/5/2017 na kuelekeza uongozi wa TBC uangalie uwezekano wa kuanzisha Chaneli ya Utalii kwa kushirikiana na TANAPA.

Tarehe 21/6/2017 Wakuu wa Taasisi ambazo ni wadau wa utalii, TANAPA, NCAA, TTB na TBC walisaini mkataba wa kuanzisha Chaneli ya Utalii, jijini Dodoma.  Aidha, katika Makubaliano yaliyosainiwa siku hiyo wadau waliazimia kuwa pamoja na kuanza rasmi mchakato wa kuanzisha chaneli ya utalii bado milango ilikuwa wazi kwa wadau wengine kujiunga.
Wadau wengine ambao pia wamejiunga na mchakato huu ni pamoja na Bodi ya Filamu (TFB), Idara ya Uvuvi, Mamlaka ya Uhifadhi wa Wanyamapori (TAWA), Wakala wa Misitu (TFS), Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).

VIPINDI NA MAUDHUI
Ili kuweza kuwa na Chaneli bora na endelevu, maudhui yanatakiwa yapatikane wakati wote, hivyo wadau wamepewa majukumu mahsusi kuhakikisha wanatengeneza vipindi  chini ya uratibu wa TBC. 
Vyanzo vya vipindi vya chaneli vinatarajiwa kuwa:
a) Vinavyotengezwa na watozi wa ndani ya TBC;
b) Vinavyotoka kwa Taasisi wadau;
c) Vinavyotoka kwa wadau wengine wa utalii;
d) Vinavyotengenezwa kwa pamoja na vyombo vingine vya utangazaji vya utalii (co-production); na
e) Vinavyonunuliwa kutoka watozi binafsi wa ndani na nje.

Edna .K.Rajab
MKUU WA KITENGO CHA MAWASILIANO, TBC 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad