HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 26 November 2018

Waziri Kamwelwe aomba subira kwa TBA, Aridhishwa ujenzi wa Ihungo Boys

Na Mwandishi Wetu, Bukoba
WAKATI Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe ameomba taasisi za serikali, Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wizara, ambazo zimeipa kazi Wakala wa Majengo ya Serikali Tanzania (TBA), kuwa na subira kwa kuwa inaupungufu wa wafanyakazi, lakini ameridhishwa na ujenzi wa shule ya sekondari ya Wavulana ya Ihungo ya mkoani Kagera iliyojengwa na taasisi hiyo.
Akifafanua Mhe. Kamwelwe amesema TBA wanakumbwa na changamoto kubwa ya upungufu wa wafanyakazi, ambapo kwa Tanzania nzima wanawafanyakazi 300 pekee, ambao wanajitoa kwa kufanya kazi kwa bidii, ambapo idadi kamili inayotakiwa ni wafanyakazi 1700.
Hatahivyo, ameipongeza TBA kwa kufanya kazi nzuri za ujenzi mbalimbali za majengo ya serikali kwa kutumia thamani halisi ya fedha tofauti na wakandarasi binafsi wamekuwa na gharama kubwa.
“Utendaji wa TBA bado unaleta mashaka nchi nzima na nimefanya nao kikao nikabaini wapo wafanyakazi 300 pekee na wanatakiwa angalau 1000 ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi, hivyo nashauri pamoja na kusikia malalamiko kila upande kutoka kwa Wakuu wa Wilaya, Mikoa, Bungeni na Watendaji wengine wa serikali, ninayafanyia kazi likiwemo la uhaba wa wafanyakazi,” amesema Mhe. Kamwelwe.
Baadhi ya kazi za ujenzi wanazofanya na walizofanya TBA ni pamoja na ujenzi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma mkoani Dodoma; ujenzi wa hospital ya Mkoa wa Simiyu na Ujenzi wa nyumba za watumishi wa umma mikoa mbalimbali. Akizungumzia ujenzi wa shule ya sekondari ya wavulana ya Katika hatua nyingine, Mhe. Kamwelwe ameipongeza TBA kwa ujenzi wa shule ya kisasa ya sekondari ya wanaume ya Ihungo iliyoathirika na tetemeko la ardhi lililotokea Kagera 2016.
“Nawapongeza sana kwa kujenga shule nzuri tena kwa gharama nafuu ya Bil. 10.4, ukiangalia wengine walitaka kujenga kwa Bil. 36, hivyo TBA wameokoa fedha nyingi sana za Watanzania na kiwango chao cha kazi ni kizuri,” amesema Mhe. Kamwelwe. Naye Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Kagera, Mhandisi Herico Bahati amesema ujenzi wa shule hiyo ulianza Oktoba 5, 2016, ambapo kuna majengo matatu ya ghorofa ya madarasa yenye vyumba 24, ofisi 12 za walimu, jengo la vyoo 80, mabweni matatu yenye vyumba 96, nyumba 30 za walimu, upanuzi wa bwalo la chakula na wamechimba kisima cha maji.
Shule hiyo inawanafunzi 600, ambapo sasa pia imeongezewa wanafunzi 751 wa shule ya Sekondari ya Bukoba waliohamishiwa hapo kwa muda baada ya shule yao kuezuliwa paa na upepo mkali uliotokea Oktoba 2018.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Muleba, ambaye pia anakaimu wilaya ya Bukoba Mjini, Mhandisi Richard Ruyangu ameishukuru serikali kwa kuijenga tena shule hiyo na sasa wanafunzi wanaendelea na masomo.
“Tunaishukuru serikali ya Awamu ya Tano ya Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa kutujengea tena shule nzuri na tunaimani kwa mazingira haya watoto watasoma kwa bidii, na hata walimu hali kadhalika watafundisha kwa moyo tumeona wamejengewa nyumba nzuri na za kisasa tena zipo maeneo ya karibu na shule itakuwa hawatoki mbali kuja kufundisha,” amesema Mhandisi Ruyangu.
Kiranja mkuu wa shule hiyo, Bw. Athuman Mohamed kwa niaba ya wanafunzi wenzake, ameishukuru serikali kwa kuwajengea tena shule yao na wameahidi kusoma kwa bidi ili kufanya vizuri katika masomo yao.
 Waziri Mkuu wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe  (mwenye suti ya bluu) akiwaeleza jambo wanafunzi wa shule ya sekondari ya wavulana ya Ihungo ya Kagera, alipofanya ziara hivi karibuni. Kulia (mwenye suti ya udongo ni Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Bw. Philip Boniventura.
  Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo ya Serikali Tanzania (TBA) mkoa wa Kagera, Mhandisi Herico Bahati (mwenye shati la batiki) akimpa maelezo mbalimbali Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (kushoto) kuhusiana na ujenzi wa shule ya sekondari ya wavulana ya Ihungo, waliyoijenga baada ya awali kuharibiwa na tetemeko la ardhi lililotokea mwaka 2016. Mbele ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bw. Philip Boniventura.
Waziri Mkuu wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (mwenye suti ya bluu) akimsikiliza Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo ya Serikali Tanzania (TBA) mkoa wa Kagera, Mhandisi Herico Bahati (mwenye shati la batiki) akimpa maelezo mbalimbali ndani ya moja ya vyumba 96 vya mabweni ya shule ya sekondari ya wavulana ya Ihungo, waliyoijenga baada ya awali kuharibiwa na tetemeko la ardhi lililotokea mwaka 2016.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad