HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 26 November 2018

“KASI YA UMEME MIJINI NA VIJIJINI NI ILE ILE’’- WAZIRI KALEMANI

NA YASINI SILAYO, GEITA
Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Medard Matogolo Kalemani akiwa Mkoani Geita, jana Novemba 25 amesema kuwa, kasi ya utekelezaji wa jukumu la kusambaza na kuunganisha wananchi na huduma ya umeme kwa maeneo ya Mijini na Vijijini kote Nchini ni ile ile ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha kuwa huduma ya Nishati ya umeme inatumika kuchochea na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na huduma za kijamii Nchi nzima. Sisi Kama Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) na Wakala wa Usambazaji Nishati ya Umeme Vijijini (REA) tumeendelea kusimamia na kutekeleza jukumu la kusambaza na kufikisha huduma za umeme kila pembe ya Nchi ikiwa ni Mijini na Vijijini” Alisema Waziri Kalemani.  

Aliongeza kuwa hivi sasa Wizara kupitia TANESCO na REA wanaendelea kutekeleza miradi ya usambazaji umeme Vijijini, lakini umeme huo unasambazwa kwa kasi ile ile maeneo ya mijini ikiwemo mitaa yenye makazi mapya na ile ya zamani ambayo ilikuwa bado hayajafikiwa na huduma za Umeme kupitia TANESCO yenye jukumu la kusambaza huduma hiyo katika maeneo ya Mijini. Alibainisha pia katika kuimarisha zaidi mpango wa usambazaji umeme vijijini serikali imeanza maandalizi ya kutenga fedha maalumu zitakazotumika kuchochea kasi ya usambazaji umeme maeneo ya mijini.  

Akiwa katika mji mdogo wa Katoro eneo la Bulengahasi Mkoni Geita, alitoa Rai kwa TANESCO na  Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme kuongeza kasi ya kusambaza na kuunganisha  wateja na huduma ya umeme ambapo alitoa siku kumi kwa TANESCO kuhakikisha mitaa na vitongoji vingi zaidi vya eneo la katoro vinaunganishwa na umeme hivyo kuimarisha huduma za kijamii pamoja kuchochea maendeleo ya wakazi wa maeneo hayo. Aidha waziri Kalemani, mbali na kuagiza Wakandarasi, TANESCO na REA kuharakisha shughuli za usambazaji umeme. Pia aliwasisitiza na kuwahamasisha wananchi kuunganisha umeme pindi miundombinu hiyo inapofika katika maeneo yao.

 Waziri alieleza kuwa serikali imekuwa ikitenga mabilioni ya fedha kila mwaka katika kuhakikisha umeme unasambazwa na kuwafikia wananchi wote na kwa bei nafuu, hivyo ni vyema wananchi wakachangamkia fursa hiyo kujikwamua kiuchumi kwa kuunganisha umeme na kubuni miradi mbalimbali inayotumia umeme kujiingizia kipato. Kwa upande wa mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO aliyeambatana na Waziri katika ziara hiyo, Mhandisi Theodory Bayona, alielezea kupokea na kutekeleza maelekezo na maagizo yote kulingana na ilivyoelekezwa na Waziri katika ziara hiyo lakini aliongeza pia mbali na kufikisha umeme mapema, TANESCO Itaendelea na juhudi za kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuunganisha umeme pindi miundombinu inapofika katika maeneo yao na kuhakikisha wananchi wote wanaostahili kuunganisha umeme wanaunganishwa ili kuongeza idadi ya wateja wa Shirika na hivyo kuongeza zaidi mapato ya Shirika kupitia mauzo ya umeme.

 Naye Mwananchi mmoja Mkazi wa Kijiji cha Mapinduzi kilichopo kata ya Buseresere Wilayani Chato aliyehudhuria katika mkutano wa Waziri kijijini hapo na aliyejitambulisha kwa jina moja la Vedasto, aliishukuru Serikali kwa kuwajali wananchi na kuwafikishia huduma ya umeme mpaka kijijini hapo. Alisema kuwa umeme umekuja na matumaini mapya ya kimaendeleo kijijini hapo na tayari wameanza kujipanga kubuni na kuanzisha shughuli mbalimbali za kimaendeleo zinazotegemea umeme kujiingizia kipato tofauti na hapo awali ambapo walikuwa wakitegemea zaidi shughuli za kilimo, uvuvi na ufugaji pekee.
 Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Medard Kalemani, kulia akiongea na Wananchi pamoja na kutoa maelekezo kwa viongozi wa TANESCO na REA katika eneo la Bulengahasi lililopo Kata ya Katoro Mkoani Geita baada ya kukagua na kujionea maendeleo ya shuguli za usambazaji umeme eneo hilo. Kushoto kwake ni Meneja wa TANESCO Mkoa wa Geita Mhandisi Joaquim Ruweta.


Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (katikati) akiendelea na kazi ya ukaguzi wa ujenzi wa miundombinu ya kusambazia umeme katika kijiji cha mapinduzi kilichopo kata ya buseresere Wilayani Chato Mkoani Geita. Kushoto ni Meneja wa TANESCO Mkoa wa Geita Mhandisi Joaquim Ruweta na Kulia ni Diwani wa Kata ya Buseresere Bw. Godfrey Fulko

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad