HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 26 November 2018

CDF YAADHIMISHA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA

Na Agness Francis, Blogu Jamii 
SHIRIKA  la Utu wa Mtoto (CDF) kwa kushirikiana na Taasisi ya Ustawi wa jamii kupitia klabu yao ya Social work imeandaa mjadala katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia duniani. 

Mjadala huo uliowakutanisha  Wahadhiri, washauri wa Vyuo, Viongozi wa serikali ya wanafunzi, wanafunzi wa vyuo pamoja na wawakilishi wa asasi za kiraia ambapo walijadili mada inayohusu ukatili wa kingono katika Taasisi za elimu ya juu. Tafiti za hivi karibuni zinaonyesha  kuwa wanafunzi wa kike walio katika vyuo vya elimu ya juu wako katika hatari ya kufanyiwa ukatili wa kingono.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Shirika la jukwaa la Utu wa Mtoto CDF,   Lenista Derugabo akizungumza na vyombo vya habari amesema kuwa lengo la kuandaa mjadala wa kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na  masuala ya ukatili wa kingono vyuoni ni kutaka kutokomeza janga hilo linalowakumba watoto wakike hasa walio katika Elimu ya   juu na kuona jinsi gani matokeo hayo yanapotea. 

"Tumeona ni vyema kuandaa mjadala huu kwa wanafunzi wa kike ambapo wako vyuoni kwa kuwa ndio watu wanaongoza kwa kufanyiwa ukatili wa kijinsia  hasa wakiwa masomoni kwa kulazimika kutoa rushwa ya ngono ili kupata alama nzuri katika masomo"amesema Derugabo. Mwanafunzi wa Chuo kikuu Bagamoyo Yudagaspa Mmari ameeleza kuwa  vitendo hivyo vya ukatili wa kingono vinaendelea vyuoni na kwa baadhi ya wanafunzi wanapofanyiwa ukatili huo  hukaa kimya. 

"Unakuta sio wote uelewa unafanana ikitokea labda maksi hazimridhishi mwanafunzi na lengo ni ufaulu vizuri, na hana uwezo wa kumpa pesa mwalimu basi kinachofata ni kutoa rushwa ya ngono." Ameeleza Yudagaspa. Mwanasheria Naemi Silayo amewataka wanafunzi kuvunja ukimya na kuwa na ujasiri wa kuzungumza yanapotokea mambo Kama hayo. 

"Siku hizi kuna utandawazi tumia basi hata simu kurekodi mazungumzo ili uwe na uhakika wa kutosha, vile vile tunaomba Serikali kupitia wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia  iliyo chini ya Profesa Joyce Ndalichako kuweza kuunda chombo huru ambacho hakitatetea walimu wa vyuoni, kwasababu wakati mwingine wanapendeleana ikitokea mwanafunzi amezungunza ukweli"amesema Mwanasheria Silayo. 

Aidha mwanachuo Mmari ametoa wito kuwa  wanafunzi wanapokwenda masomoni wazingatie masomo ili wafaulu vizuri na kuepukana na kutoa rushwa ya ngono, na walimu wawe kama walezi na  wazazi kwao.
 Mwanasheria Naemi Silayo akizungumza na wanafunzi wa vyuo vikuu mbali mbali hapa nchini kuwataka wavunje ukimya kuwa na ujasiri wa kuzungumza pindi wanapokumbana na janga la ukatili wa kingono wanaofanyiwa na walimu wao, wakati wa kuhadhimisha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia duniani Jijini Dar es Salaam.
Wahadhili, washauri  Vyuo vikuu pamoja na  wawakilishi  wa Asasi za kiraia wakijadili mada inayohusu ukatili wa kingono katika Taasisi za elimu ya juu, katika ukumbi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya usiku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
  Wanafunzi  mbali mbali wa Elimu ya juu  waliohudhiria katika mjadala wa kuhadhimisha siku 16 ya za kupinga ukatili wa kijinsi duniani, katika ukumbi  Chuo cha Ustawi wa Jamii Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad