HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 23 November 2018

WATU 80 WAMEFARIKI KWA KIPINDUPINDU HADI SASA, VIFAA VYA LIFESTRAW SULUHISHO KUOKOA JAMII

Na Leandra Gabriel, Blogu ya Jamii

WAZIRI wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto Ummy Mwalimu amezindua huduma ya maji safi na salama kwa jamii mradi unaotekelezwa na kampuni ya Lifestraw nchini ambayo imezindua vifaa maalumu na vya kisasa ambavyo huchuja na kusalimisha maji vyema kabisa.

Akizungumza katika uzinduzi huo Waziri Ummy amesema kuwa Lifestraw wanastahili pongezi  kwa hilo walilolifanya na ni njia ya kufikia malengo ya kufikia asilimia 80 ya kutoa huduma ya maji safi na salama katika jamii.

Amesema kuwa kuanzia mwezi Januari hadi leo watu 4406 wameugua kipindupindu  na kati yao watu 80 walipoteza maisha na tatizo hilo halisababishwi na kula kinyesi pekee pia ni kutokana na ukosefu wa maji safi na vyoo, pia amesema kuwa asilimia 60 ya wagonjwa wa nje (OPD) wanaotibiwa katika hospitali hukutwa na magonjwa yanayotokana na kukosa maji safi na salama, matumizi yasiyo sahihi ya vyoo na unawaji wa mikono mara baada ya kutumia vyoo.

Aidha amesema kuwa kwa kushirikiana na Wizara ya maji wanahakikisha kuwa maji yanayosambazwa yanawekwa kinga maalumu ya kuua vijidudu katika maeneo yote na hasa yale yanayokumbwa na ugonjwa wa kipindupindu ikiwemo Mikoa ya Dar es salaam,  Pwani,  Arusha, Manyara na Singida.

Vilevile amewapongeza Lifestraw kwa kutumia teknolojia ambayo imethibitishwa na mamlaka husika nchini kuwa vifaa hivyo vinaweza kuua vijidudu kwa asilimia 99.999 na kuyaacha maji yakiwa salama kabisa.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Lifestraw nchini Fatma Mahsen amesema kuwa uzinduzi huo wa vifaa vya kuhifadhia maji ni mkakati wa kusaidia jamii katika kuhifadhi maji safi na salama kwa  matumizi ya jamii.

Fatma amesema vifaa hivyo ni salama na huhifadhi maji kwa usalama na hudumu kwa muda mrefu na watahakikisha wanasimamia hilo ili kila mwananchi anapata huduma ya maji safi na salama ili kuweza kufanikisha malengo ya kufikia asilimia 80 ya kutoa huduma ya maji safi na salama na kutokomeza kabisa mlipuko wa magonjwa yanayotokana na ukosefu wa maji safi hasa kipindupindu.

Pia Benjamin Filskov kutoka Water Mission Tanzania amesema kuwa takwimu zinaonesha kuwa watu bilioni 2.1 wanakosa maji kwa mwaka na zaidi ya watu 842,000 hufa kila mwaka kwa kukosa maji safi na salama hali inayosababishwa na mlipuko wa magonjwa hasa kipindupindu.

Imeelezwa kuwa katika mradi huo unaojumuisha nchi 20 ikiwemo Tanzania utasaidia kuboresha huduma za upatikanaji wa maji safi na salama na hadi sasa asilimia 61 ya huduma hiyo ya kutumia vifaa maalumu kwa ajili ya kuhifadhia maji imefanikiwa katika maeneo mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad