HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 23 November 2018

TFDA YATOA ELIMU YA KUANZISHA VIWANDA KWA WASINDIKAJI WADOGO WA VYAKULA MKOANI SHINYANGA

Na James Ndege - Shinyanga
TFDA inaendesha mafunzo ya siku mbili kwa wajasiriamali wadogo wa usindikaji wa vyakula mkoani Shinyanga ikiwa ni mojawapo ya mikakati yake ya kuwezesha ukuaji wa Sekta ya  viwanda nchini kwa wasindikaji 100 wa mkoa huo  kuanzia tarehe 22 – 23 Novemba 2018 katika Ukumbi wa SIDO Mkoa, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.
Mafunzo hayo yalifunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Bi. Jasinta Mboneko kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Zainab R. Telack ambaye aliwaasa wasindikaji wa vyakula hao kutumia fursa hiyo kwa ukamilifu ili waweze kukidhi vigezo muhimu vya kisheria na kuzalisha bidhaa bora, salama na zenye ufanisi ili kukidhi soko la ndani na nje ya nchi jambo litakalochangia ukuaji wa uchumi wa nchi lakini pia kulinda afya ya jamii kwa kuwa TFDA ipo karibu na kundi hili muhimu katika uanzishaji wa viwanda nchini kwa kutatua changamoto zao.
“Kafanyeni kazi zenu kwa kufuata mafundisho mtakayopewa, tunawategemea kwamba ninyi mtakuwa mabalozi wazuri kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wengine, kwenye Mkoa wetu tumejipanga kuhakikisha kwamba kila mmoja anafanya shughuli zake zilizo halali, hakuna ujanja ujanja kwenye Serikali ya awamu hii ya Awamu ya  Tano inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. Nadhani ninyi nyote mmeona kwenye vyombo vya habari kilichotokea Kahama kwa Wafanyabishara wasiotaka kufuata sheria. 

Hakuna msindikaji ambaye ataweza kudumu katika biashara bila ya kuhakikisha kuwa bidhaa inayozalishwa inakidhi vigezo vya ubora na usalama. Hii inatokana na ukweli kuwa ubora na usalama wa chakula ni sharti muhimu kwa wateja wa chakula tunaowalenga” alisema Mkuu huyo wa Wilaya wakati akisoma hotuba ya ufunguzi ya Mkuu wa Mkoa.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula wa TFDA, Bw. Justin Makisi alisema kwamba Mamlaka yake imekuwa na mkakati wa kukuza viwanda vidogo nchini toka mwaka 2006 baada ya kufanya utafiti mwaka huo  na kubaini kwamba zaidi ya 74% ya viwanda vidogo nchini vilikuwa vya usindikaji wa vyakula na kuanzia kipindi hicho ilianza kutoa mafunzo kwa wasindikaji hao kwa kila mkoa na sasa imeshafikia  mikoa 23 ya Tanzania Bara ikiwa ni sawa na 88% ya mikoa yote inayotarajiwa kufikiwa. 
“Serikali imeshatoa maelekezo kwa Taasisi zake kuwawezesha wajasiriamali na wawekezaji wengine kuanzisha viwanda ili Taifa liweze kuwa la Viwanda na Uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, TFDA tunatekeleza hilo kama mnavyoona sasa. Jambo la msingi ni kuzingatia maelekezo ya kitaalam yanayofundishwa hapa ili muweze kuzalisha bidhaa za viwanda zenye tija na ufanisi kwa ajili ya kukuza uchumi wenu na Taifa kwa ujumla ambapo mtaweza kupata soko la ndani na nje ya nchi” alisisitiza Bw. Makisi kwa washiriki.
Katika mafunzo hayo, TFDA imeshirikisha Taasisi nyingine za Serikali za Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), TANTRADE, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na BRELA ili kuwawezesha wajasiriamali kutambua mambo muhimu yanayotakiwa katika kuzalisha bidhaa.
Mgeni Rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akifungua mafunzo ya siku mbili tarehe 22 – 23/11/2018 kwa Wajasiriamali Wadogo wa Usindikaji wa Vyakula mkoani Shinyanga, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mhe. Zainab R. Telack katika Ukumbi wa SIDO wa Mkoa wa Shinyanga. Kulia, ni Mkaguzi Mkuu wa Chakula wa TFDA, Lazaro Mwambole na kushoto ni Mwenyekiti wa mafunzo hayo Juma Nyankanga
Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula Justin Makisi akisisitiza jambo kwa washiriki wa mafunzo (hawapo pichani). Kushoto, ni Mgeni Rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Bi. Jasinta Mboneko na kulia ni Meneja wa TFDA Kanda ya Ziwa, Moses Mbambe
Sehemu ya wasindikaji wa vyakula wa mkoa wa Shinyanga wakifuatilia mada zilizotolewa na TFDA katika mafunzo hayo.
Sehemu ya picha ya pamoja baina ya Mgeni Rasmi, Watumishi wa Serikali na Wasindikaji wa chakula wa mkoa wa Shinyanga

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad