HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, 6 November 2018

Wachimbaji Wadogo watakiwa kuhakikisha leseni kutokuwa chanzo cha migogoro

Na Rhoda James – Bukombe 
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amewataka wachimbaji wadogo nchini kuhakikisha kuwa leseni za uchimbaji Madini zinazotolewa na Wizara kupitia Tume ya Madini ikiwemo mikataba ya ubia wanayongia na Kampuni mbalimbali kutokuwa chanzo cha migogoro nchini.
Naibu Waziri Biteko aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akisuluhisha mgogoro uliokuwepo kati ya Kampuni ya Pamoja Mining Ltd na Mkazi wa Nyarugusu Salum Othman ambaye aliilalamikia kampuni hiyo kwa kukiuka mkataba waliojiwekea kati yao.
Akizungumza katika kikao hicho cha usuluhishi, Naibu Waziri Biteko alisema kuwa, wachimbaji wadogo wanapoingia mikataba na kampuni yoyote ile yenye nia ya kuwa na ubia na Mzawa  ni lazima  wazingatie  na kukubaliana juu ya mikataba wanayoingia  kwa kuwa, pindi  taratibu zinapokiukwa zinaichafua nchi.
 “Mikataba hii mnayoingia mjue ya kuwa nyinyi mnakuwa ni taswira ya nchi sasa mkikiuka mnakuwa mnaichafua nchi yetu, lazima mzingatie makubaliano mnayojiwekea nyie wote, mwekezaji na mzawa,” alisema Biteko.
Aidha, aliainisha baadhi ya masuala ambayo yanatakiwa kuzingatiwa wakati wa kuingia mikataba na wabia  na kueleza kuwa ni pamoja na kuangalia uhai wa leseni zao, kusajili mikataba yao kwenye Tume ya Madini, kuhakikisha kuwa eneo au biashara wanayoingia haina migogoro, wazawa kujua kuwa wanatakiwa kuwa na asilimia angalau zisizopungua 25 na kuhakikisha kuwa kodi zote za serikali zinalipwa kwa wakati.
Vilevile, Naibu Waziri Biteko alimtaka, Othman ambaye ni mlalamikaji kuhusu ukiukwaji wa mkataba kati yake na Kampuni ya Pamoja Mining Ltd kuhakikisha kuwa wanazingatia sheria zote ili pande zote mbili ziweze kufanya kazi  kwa tija na bila kukwepa kodi za serikali. 
Pia, alitumia fursa hiyo kuzitaka Ofisi za Madini kote nchini kuhakikisha kuwa zinaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo ili matatizo kama hayo yanayojitokeza sasa yasiendele kujitokeza kwani ni wajibu wa Wizara kuhakikisha kuwa migogoro baina ya wachimbaji  na wawekezaji inakwisha.
Naye, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita, Daniel Mapunda alimshukuru Naibu Waziri Biteko kwa kusuluhisha mgogoro huo ambao umedumu kwa kipindi kirefu nakueleza kuwa, ofisi hiyo itaendelea kuzingatia na kutekeleza maagizo hayo kwa mujibu wa sheria.  
 Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia) akisikiliza mgogoro uliokuwepo kati ya Kampuni ya Pamoja Mining Ltd na Mkazi wa Nyarugusu Salum Othman (hawapo pichani) katika Ofisi ya Halmashauri ya Bukombe. Kushoto ni Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita, Daniel Mapunda.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa kwanza kulia mbele) akisikiliza mgogoro uliokuwepo kati ya Kampuni ya Pamoja Mining ltd na Mkazi wa Nyarugusu Salum katika Ofisi ya Halmashauri ya Bukombe. Wengine katika picha ni Wafanyakazi kutoka Ofisi ya Madini Geita na  kampuni ya Pamoja Mining Ltd.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad