HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 29, 2018

MEJA JENERALI JACOB AZITAKA IDARA YA HUDUMA ZA UANGALIZI, JESHI LA POLISI NA MAGEREZA KUSHIRIKIANA ILI KUONDOA MSONGAMANO WA WAFUNGWA MAGEREZANI

Na Mwandishi wetu, Morogoro
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja Jenerali Jacob Kingu, amewataka watendaji wa Idara ya Huduma za Uangalizi , Jeshi la Polisi na  Magereza kushirikiana kwa pamoja ili kupunguza msongamano wa wafungwa Magerezani. Meja Jenerali Kingu ameyasema hayo leo wakati akizungumza kwenye Mkutano wa Maafisa Wafawithi wa Mikoa waliokutana katika Ukumbi wa Magadu Officers Mess mjini Morogoro, kwa lengo la kutathmini utendaji kazi wao zikiwemo mafanikio pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao.

Meja Jenerali Kingu amesema kuwa, Idara ya Huduma za Uangalizi zamani ilikuwa ikiitwa Huduma kwa jamii ambayo ndio inayohusika na utoaji wa adhabu mbadala wa vifungo Magerezani, imeanzishwa ili kuhakikisha kuwa wafungwa wenye makosa madogo yasiyo hatarishi kwa jamii na taifa, wanatumikia adhabu zao kwenye jamii nje ya magereza. “ Kwa  kufanya hivyo kungesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msongamano  Magerezani hivyo kuipunguzia  Serikali  gharama za kuwahifadhi  wafungwa  Magerezani”. Amesema Meja Jenerali Jacob Kingu.

Meja Jenerali Kingu amewataka watendaji hao wa Idara ya Huduma za Uangalizi kubainisha changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao ili ziweze kutatuliwa kwa haraka, jambo litakalosaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi hivyo kupunguza msongamano wa wafungwa Magerezani. Akizungumzia suala la nidhamu kazini, Katibu Mkuu huyo amesema hatosita kumchukulia hatua mtumishi yeyote yule atakayebainika  kwenda kinyume  na maadili ya utumishi wa Umma na sheria za nchi.

Katibu Mkuu huyo amemuagiza Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Ungalizi Aloyce Musika kupeleka watendaji katika mikoa mitatu  Lindi, Katavi na Ruvuma ili wakazi wa mikoa hiyo waweze pia kupata huduma zinazotolewa na Idara hiyo, kwani kwa sasa Idara hiyo ina watendaji wawakilishi katika Mikoa 23 hapa Tanzania.
 Mwisho. 
   Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja Jenerali Jacob Kingu  wa kwanza kushoto akitoa maelekezo kwa baadhi ya Wakuu wa Idara wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakati wa Mkutano wa Maafisa Wafawithi wa Mikoa kilichofanyika Magadu Officers Mess Mjini Morogoro leo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja Jenerali Jacob Kingu  aliyevaa suti nyeusi akifurahia jambo na baadhi ya Wakuu wa Idara wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakati wa Mkutano wa Maafisa Wafawithi wa Mikoa kilichofanyika Magadu Officers Mess Mjini Morogoro leo.
  Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja Jenerali Jacob Kingu wa tatu kutoka kulia akiwa katika picha ya pamoja na Washiriki wa Mkutano wa Maafisa Wafawithi wa Mikoa kilichofanyika Magadu Officers Mess Mjini Morogoro wa pili kutoka kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Ungalizi Bw. Aloyce Musika.(Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad