HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 22, 2018

HAKUNA MGAO WA UMEME MWAKA HUU -DKT ALEXANDER KYARUZI

Na Francis Godwin,Iringa
MWENYEKITI  wa  bodi ya  shirika la  umeme Tanzania  (TANESCO )  Dkt   Alexander Kyaruzi amesema  kuwa  hali ya  uzalishaji  wa  umeme  nchini  ni  nzuri na  kuwa   watanzania  wasitegemee  kuwepo  kwa mgao   wa  umeme  kwa  mwaka  huu.

Akizungumza  jana wakati  wa   hafla ya  uwashaji  umeme  kijiji  cha  Ndolezi katika  Halmashauri ya  mji Mafinga  Dkt  Kyaruzi  alisema  kuwa  pamoja na  kuwa  kipindi cha  kiangazi  kinakwenda  kumalizika ila hali ya maji  katika  vituo  vya uzalishaji  umeme  vya Kidatu na Mtera  ni  nzuri  na kuwa maji hayo yataendelea  kuongezeka  zaidi kwani msimu wa masika  unakaribia.

Kuhusu   kasi ya  usogezaji wa  umeme  katika  vijiji  ,vitongoji  na  maeneo ya  visiwa alisema  kuwa  kasi  inaendelea   vizuri na  kuwa  hadi  mwaka 2021  maeneo  yote ya  nchi umeme  utakuwa  umefika na  hakutakuwa na kijiji  wala  kisiwa  ambacho  wananchi  watakuwa  hawana  umeme .

Pamoja na  umeme    huo  wa maji na  gesi  ambao  unatumika  kwa sasa bado  alisema  shirika  limeendelea  na uvumbuzi  wa  vyanzo  vingine  vya  umeme kama  umeme wa  joto ardhi  ambao tafiti  zinaonyesha  baadhi ya  mikoa kama  mkoa  wa Mbeya  kuwepo  kwa  umeme   huo .

"  Tunategemea  miaka  mitano mbele  kuwa na umeme  utakaozalishwa   kupitia  joto  ardhi   hivyo  bado  nchi  itaendelea  kuwa  na  uhakika  wa  umeme baada ya  kuwa na  vyanvyo  tofauti  tofauti "  alisema  Dkt  Kyaruzi

Alisema  kuwa maeneo    Ziwa  ngozi  mkoani  Mbeya  ni  eneo la kwanza  ambalo  wamefanikiwa  kufanya  utafiti na  kuonekana  lina weza  kuzalisha  umeme  wa  joto  ardhi na  tayari  wamempata  mkandarasi  wa kufanya  zoezi la  uchimbaji  wa eneo hilo .

Dkt  Kyaruzi  alisema  serikali ya  awamu ya  tano  chini ya  Rais  Dkt  John Magufuli imekuwa na makusudi mema kwa  watanzania  na  kuweka  mkakati  kabambe  wa  kuhakikisha ifikapo  mwaka 2021  kila mtanzania  kuweza  kupata   umeme  hivyo wao kama  watekelezaji wa mpango  huo  watahakikisha  wanatekeleza  kwa  nguvu  zote .

Awali  akizungumza na  wananchi  wa kijiji  cha Ndolezi  wakati wa hafla ya  uwashaji umeme kijijini hapo  mkuu wa  mkoa wa Iringa  Alli  Hapi  alisema  hatakubali  kuona ucheleweshwaji  wa  utekelezaji wa miradi ya  umeme katika  mkoa  huo .

Mkuu  huyo wa mkoa  alimtaka  mkandarasi  wa wakala wa Nishati Vijijini (REA) anayetekeleza  mradi  wa  umeme  katika kijiji  cha Ndolezi  kuhakikisha anakamilisha  zoezi  la  usambazaji  wa umeme katika kijiji  hicho  ndani ya  siku 21  .

Pia  mkuu  huyo wa mkoa  alisema mkandarasi lazima  kuhakikisha anapeleka umeme katika maeneo  yote  ya umma  kama  zahanati ,shule  na mengine kama  alivyoelekezwa na  kuacha  kupeleka  umeme  kipendeleo kwa  baadhi ya  watu .

Wakati  huo  huo mkuu  wa  mkoa  wa Iringa amepiga marufuku halmashauru zote za Mkoa  huo kuruhusu usafirishaji wa nguzo za umeme pasipo kulipia ushuru wa nguzo wa asilimia tano kwa mujibu wa sheria zilizopitishwa na bunge.

Asema wilaya ya Kilolo pekee kupitia kampuni ya New Foret amebaini ukwepati wa kodi wa shilingi bilioni 2.7 pesa ambazo walipaswa kulipa ushuru wa asilimia 5 kwa kila nguzo na wao wakawa wanalipa shilingi 5000 kinyume na sheria zilizotungwa na bunge.

Mkuu huyo wa mkoa ametoa agizo hilo kabla ya  kwenda kuwasha umeme  wakati akizungumza na wadau wa mazao ya Misitu pamoja na viongozi wa halmashauri za wilaya ya Mufindi katika ukumbi wa mikutano kabla ya kuanza ziara yake ya kikazi wilayani humo.

Alisema kuwa kitendawili cha umasikini wetu  mkoa wa Iringa kimeanza kuteguliwa baada ya kubaini mabilioni ya fedha yanayopotea katika kipengere kimoja pekee cha nguzo za umeme kutokana na halmashauri kufanya mazungumzo yasiyo rasmi ya kuchukua ushuru wa shilingi 5000 kwa kila nguzo badala ya kukusanya ushuru wa asilimia 5 kwa kila nguzo.

Hapi alisema kuwa katika kuona mkoa wa Iringa kwa mwaka ujao unaongoza kitaifa katika ukusanyaji wa mapato ni lazima kwa wakurugenzi wote kusimamia ukusanyaji wa mapato yatokanayo na mazao ya Misitu kwa kufuata sheria na sio makubaliano yaliyo nje ya sheria zilizopitishwa na bunge toka mwaka 2013 pamoja na kufanyiwa marekebisho mbali mbali.

"Sheria hii ipo wazi na hakuna namna zaidi ya kutekeleza kwa maslahi ya nchi na mkurugenzi atakayeshindwa kusimamia basi atakuwa ameamua kutofuata sheria na litakalo mkuta yeye kama mkuu wa mkoa atakuwa amenawa mikono" alisema  Hapi

Kuwa lazima mapato ya serikali kuweza kukusanywa kwa ufanisi na wakurugenzi na wakuu wa wilaya ni lazima kusimamia zoezi hilo kwa ufanisi .

Akitolea mfano alisema kwa wilaya ya Kilolo pekee kupitia kampuni moja ya New Foret company amebaini ukwepaji wa kodi wa shilingi zaidi ya bilioni 2 ambazo kampuni hiyo imeshindwa kulipa asilimia 5 za nguzo kwa muda wote na badala yake kampuni hiyo imekuwa ikilipa shilingi 5000 kwa kila nguzo kinyume na sheria zilizotungwa na bunge .

"Kwa pesa hizi pekee ambazo kampuni imeshindwa kulipa iwapo wilaya ya Kilolo ingeweza kukusanya ingeweza kujenga hospitali ya wilaya kwa pesa hizo ama kujenga shule zaidi ya tano au kupeleka maji kwa wananchi" alisema mkuu wa mkoa

Kuwa kwa upande wake yupo kwa ajili ya kusimamia sheria hivyo atahakikisha kodi iliyokwepwa kwa muda wote toka sheria ilipopitishwa inalipwa na namna ya kulipa watakubaliana na halmashauri jinsi pesa hizo zitakavyotolewa ila kuanzia sasa ni marufuku nguvu kusafirishwa bila kulipia asilimia 5 iliyopitishwa kisheria na bunge .

Alisema kuwa anatambua zipo nguzo za saizi mbali mbali kama saizi tatu tofauti na zipo zinazouzwa hadi milioni moja sasa kuchukua ushuru wa shilingi 5000 kwa nguzo ya milioni 1 ama nguzo ya shilingi 500,000 utaona ni kwa kiasi gani halmashauri zinavyopoteza mapato yake .

Mkuu huyo wa mkoa alisema kupitia eneo hilo pekee utaona ni kwa kiasi gani ukwepaji kodi huo ulivyokuwa na mnyororo mrefu kwani iwapo wataamua kufuatilia jambo hilo kwa kina wengi watakamatwa kwa kesi ya uhujumu uchumi .

"Ila tumesema kwa kuanzia sasa sheria isimamiwe kwa nguzo zote zinazotoka kulipia ushuru kwa asilimia 5 pili kuanzia makubaliano ya namna gani watalipa pesa wanazodaiwa na kama itashindikana basi watendaji wa umma watasema wanakusanya mapato kwa sheria gani  Kilolo wao wamekwisha fanya wamebaini wanadai shilingi bilioni 2.7 hivyo halmashauri nyingine fanyeni hivyo "

Hata hivyo alisema hatakubali kuona mapato ya serikali yanapotea na kama kampuni za nguzo zitashindwa kulipa watatumia taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa  nchini (TAKUKURU) na vyombo vingine kuona wahusika wote wahujumu uchumi kukamatwa.

Hivyo alitaka ndani ya wiki tatu apewe taarifa ya namna kamati zitakazoundwa na wakuu wa wilaya kukaa na kukubaliana namna ya pesa hizo zitakavyo lipwa ikishindikana ataleta vyombo vyake kuona wote waliohusika kuhujumu uchumi wanafikishwa mahakamani .

"Kuwa hakuna atakayekusaidia kukwepa mapato hata upige simu kwa waziri gani kwani haya ni maagizo ya mheshimiwa Rais hivyo jambo la muhimu ni kukubali kulipa kwa utaratibu uliopo na wale watakaokubali wataweka utaratibu ila watakao kataa na kutaka kwenda mahakamani tutawabana wao kabla.
 Mkuu  wa  mkoa  wa  Iringa Ali  Hapi mwenye  suti  nyeusi na mkurugenzi wa bodi ya Tanesco Dkt Alexander Kyarusi kulia  wakiwasha  umeme  kijiji cha Ndolezi Mafinga mkoani Iringa
 Mkuu wa  mkoa wa Iringa Alli Hapi  akisikiliza kero za  wananchi juu ya umeme wilayani Mufindi jana
 Mwenyekiti wa  bodi ya Tanesco Dkt Alexander Kyaruzi (kushoto) akifuatilia taarifa ya meneja wa Tanesco Mafinga  wakati wa uwashaji  umeme kijiji cha Ndolezi
Wananchi Mufindi wakitoa kero zao kwa  mkuu wa mkoa wa Iringa Alli Hapi  wakati wa  kuwasha umeme kijiji cha Ndolezi Mafinga

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad