HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 22 November 2018

BARAZA LA TIBA ASILI LATOA ELIMU KWA WAKUNGA WA JADI

 NA WAMJW- DAR ES SALAAM. 
BARAZA Tiba asili na Tiba mbadala nchini limetoa elimu kwa wakunga wa jadi  kuwa kazi yao kubwa ni kuhakikisha mama mjamzito anajifungua salama kwenye kituo cha afya kilichopo karibu ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Hayo yamesemwa na Msajili wa Baraza la Tiba asili na Tiba mbadala nchini Dkt. Ruth Suza wakati wa semina na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa tiba  asili na tiba mbadala nchini. 

Amesema kuwa wakunga  wa jadi nchini wanatakiwa kuwa kipaumbele katika kuhakikisha wamama wajawazito wanawahimiza kujifungulia katika vituo vya afya kwa usalama wa maisha ya mama na mtoto. 

"Tunapita kuwaelimisha Wakunga wa jadi kuwa kazi yao kubwa ni kuhakikisha mama mjamzito anajifungua salama kwenye kituo cha afya kilichopo karibu ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi" alisema Dkt. Suza. 

 Dkt Suza amesema jumla ya waganga wa tiba asili na tiba mbadala 19912 wamesajiliwa na Baraza la Tiba asili na Tiba mbadala nchini ili kuweza kutoa huduma hizo kwa kufuata sheria na taratibu. 

 "Pamoja na waganga wa tiba asili na tiba mbadala 19912 kusajiliwa pia tumesajili vituo vya tiba asili na tiba mbadala 19  kutoa huduma za afya nchini" alisema Dkt. Suza. 

 Dkt. Suza amewataka waganga wa tiba asili na tiba mbadala kupitisha dawa zao kwenye mamlaka husika kwa ajili ya vipimo pamoja na kusajiliwa kwa matumizi sahihi ya watanzania. 

Kwa upande wake Mratibu wa Taifa wa masuala ya Tiba asili na tiba mbadala Dkt. Liggyle Vumilia amesema kuwa watanzania wanatakiwa kujitokeza kwenye kilimo cha uzalishaji wa miti ya dawa za asili na mbadala ili kupiga hatua zaidi kwenye huduma hizo nchini. 

Naye Mfamasia kutoka Baraza la Tiba asili na Tiba mbadala  Ndahani Msigwa amesema kuwa waganga hawatakiwi kutoa matangazo ya dawa zao ambazo hazijasajiliwa pamoja na kujitangaza kama hawajasajiliwa. 

"Mganga wa tiba asili na tiba mbadala hatakiwi kutangaza dawa yake km hajasajili dawa hiyo na asijitangaze kama hana kibali maalum kutoka baraza hili iwe kwenye luninga, radio, magazeti hata mitandao ya kijamii", alisema Bw. Msigwa. 

Aidha Ndahani amesema kuwa waganga hawatakiwi kukata vimeo kwa watoto, kukeketa, kutoa meno ya plastiki pamoja na kupiga ramli kwani ni kinyume cha sheria na taratibu za baraza hilo. 

Bw. Ndahani amesema kuwa waganga wanatakiwa kuzingatia usiri pindi wanapowahudumia wateja wao na kuweka mazingira ya kutolea huduma zao kuwa na usafi pamoja na usalama wa wateja
 Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala , Dk.Edmond Kayombo akizungumza na wadau mbalimbali kuhusu taratibu na hatua za usajili wa waganga,dawa na vituo vyakutolea huduma leo jijini Dar es Salaam, (kushoto ni)Msajili Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Ruth Suza.(Picha na Emmanuel Massaka wa MMG)
 Mratibu wa Taifa tiba asili na tiba Mbadala Dkt.Liggyle Vumilia wa Wizara ya Afya akizungumza na waandishi habari na wadau mbalimbali juu hatua walizozichukua kwa watoaji huduma tiba asili na tiba mbadala leo jijini Dar es Salaam.(Picha na Emmanuel Massaka wa MMG)
 Mfamasia Baraza la  tiba asali na tiba  Mbadala wa Wizara ya Afya, Ndahani Msigwa akizungumza na wadau mbalimbali wa afya kuhusu sheria, kanuni na taratibu za utoaji huduma za tiba mbadala leo jijini Dar es Salaam.
 Sehemu wa wadau mbalimbali wakimsikiliza Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala , Dk. Edmond Kayombo.
Picha ya pamoja

1 comment:

Post Bottom Ad