HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, July 18, 2018

Tanzania yafurahishwa na UN katika kutekeleza mradi wa KJP

MKUU wa mkoa wa Kigoma Emmanuel Maganga  amesema serikali ya Tanzania inafurahishwa na namna Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanavyofanya kila linalowezekana kusaidia kuboresha maisha ya wananchi wa mkoa wa Kigoma ambao ndio wenyeji wa wenzao wanaokimbia matatizo nchi jirani.
Akizungumza katika mkutano wa kamati ya maandalizi ya utekelezaji wa programu ya pamoja ya kusaidia Kigoma (KJP), alisema kazi kubwa inayofanywa na mashirika hayo ikiwamo ya kupeleka ushawishi kwa wadau wa maendeleo ya kusaidia wananchi wa Kigoma wakiwemo wageni wakazi na wakimbizi.
Akiwa Mwenyekiti mwenza wa kamati hiyo, Maganga alisema pamoja na juhudi hizo bado mkoa una changamoto nyingi zinazotakiwa kushughulikiwa japo serikali imeendelea na juhudi za kuboresha mazingira ya miundombinu ya kuwezesha shughuli za kiuchumi.
Alisema toka mkutano wa mwisho mwaka jana, kumekuwa na maendeleo makubwa katika kampeni za serikali za kuufungua mkoa huo kiuchumi kwa kutengeneza miundombinu mbalimbali kuifanya Kigoma kuwa kitovu cha biashara.
Alisema serikali inaendeleza miradi ya kimkakati hasa ya barabara zinazounga mkoa huo na nchi za Rwanda, Burundi, Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo (DRC)  na mikoa mingine ya Tanzania ya Shinyanga, Mwanza, Kagera na Tabora.
Alisema mathalani kwa kujengwa kwa barabara ya Nyakanazi – Kigoma kwa kiwango cha lami kutafungua fursa za kiuchumi  za mkoa huo. Aidha alisema kwamba kumekuwepo na maboresho katika usafiri wa anga ambapo kwa sasa kuna safari sita za ndege kwa wiki.

Akizungumzia kuhusu umuhimu wa ushiriki wa wadau wote katika programu hiyo, alisema baada ya mkutano wa Aprili 27 mwaka huu anaona kuwiwa sana na Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha kwamba kila mdau anashiriki kuhakikisha utekelezaji wake.
Aliuomba Umoja wa Mataifa kuwapatia elimu wabunge ambao walikosekana katika mkutano huo wa kueleweshana kuhusu programu ili waweze kushiriki kikamilifu.Pia aliomba Umoja wa Mataifa kufanyia kazi hoja ya kutanuliwa kwa programu hiyo kufika katika wilaya zote za mkoa huo.
Mkuu huyo wa mkoa  pamoja na kumshukuru binafsi Mratibu wa mashirikia ya Umoja wa Mataifa nchini Alvaro Rodriguez na Umoja wa Mataifa alisema kwamba kutokana na umuhimu wa programu hiyo yeye binafsi atakuwa anaifuatilia na kuwataka watendaji katika mkoa kuhakikisha kwamba wanatekeleza wajibu wao kwa mujibu wa programu yenyewe.
Naye Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez Alvaro Rodriguez akizungumza katika kikao hicho alisema mradi wa utekelezaji wa pamoja wa Kigoma (KJP) ni ajenda muhimu katika utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania  UNDAP II, wenye lengo la kutoa msaada wa maendeleo kwa Tanzania ndani ya mpango wa maendeleo wa Tanzania wa miaka mitano.
Alisema mpango huo umelenga kuangalia changamoto za maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika mkoa wa Kigoma na hivyo kuwezesha maendeleo endelevu (SDGs) kuweza kufanikiwa. Mkoa wa Kigoma unaongoza kwa kuhifadhi wakimbizi kutoka Burundi, Rwanda na Kongo
Katika hotuba yake kwenye kikao hicho alishukuru mataifa ya Sweden, Norway na Korea Kusini kwa kuchangia fedha kwa ajili ya kufanikisha programu hiyo ya maendeleo. Mkuu huyo wa mashirika ya Umoja wa Mataifa pia alishukuru serikali ya Tanzania kwa kuteua mtu ambaye atakuwa anashughulika na mradi huo moja kwa moja. Aidha alishukuru wadau wengine wa mradi kwa kuliona hilo na wao kuteua watu mahususi ambao wataangalia utekelezaji wa miradi katika nafasi yao.
Mradi huo wa KJP unajumuisha shughuli za kitaifa zenye lengo la kuwa kwamua wananchi wa Kigoma na pia kuwawezesha kuhimili muingiliano wa tamaduni zingine kutokana na kupokea wakimbizi. Mambo yanayofanyika katika mradi huo ni kukabili ukatili wa kijinsia kuwawezesha kiuchumi wananchi wa Kigoma, Uendelezaji wa sekta ya kilimo (ASDP 2) na  mradi wa maendeleo ya maji  (WSDP).
Imeelezwa kuwa kufanikishwa kwa mambo hayo kutawezesha mkoa huo kusonga mbele na kukamilisha malengo ya maendeleo  endelevu ya dunia.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa katika mradi huo yenyewe yanatoa utaalamu wa kiufundi, fedha na msaada wa kitaasisi kuhakikisha kwamba kazi zilizokusudiwa katika mradi zinafanyika kwa kiwango kikubwa.
Alisema katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo wanawake  na vijana wamejitwalia nafasi ya kujifunza na pia kuwezeshwa katika elimu na kilimo.Kukamilika kwa kituo cha mafunzo kumewezesha vijana 270 kila mwaka kupata elimu ya ufundi kama tehama, useremala, utengenezaji wa sabuni na kadhalika hali ambayo inatarajiwa kusababisha mabadiliko makubwa ya kimaendeleo.
Pia mradi unashiriki katika ujenzi wa masoko yasiyo na mpaka katika maeneo ya Kakonko na Kibondo  na kuanzishwa kwa makundi 61 ya uwekaji akiba yaliyo na wanachama 1400.
Aidha watoto 513 waliokuwa wanaoishi katika mazingira magumu huku wakiwa wamefanyiwa ukatili wa kijinsia wamepatiwa nyenzo muhimu za kusoma na wengine 3,900 walitambuliwa ujuzi wao na kwamba mipango iko mbioni kuhakikisha kwamba wanashiriki katika uzalishaji mali.
Naye Kansela wa Ubalozi wa Norway nchini Britt Kjolas amesema kwamba amefurahishwa shughuli zinazoendelea katika mradi huo wa pamoja kuahidi nchi yake kuendelea kushirikiana na mashirika ya Umoja wa Mataifa na serikali ya Tanzania kuwezesha mabadiliko chanya katika mkoa wa Kigoma.
Alielezea kufurahishwa kwake na kujitokeza kwa wingi kwa wadau wa mradi na kusema mradi huo upo katika msingi mzuri wa mafanikio.
 Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (kulia) akibadilishana mawazo na wadau wa maendeleo mara baada ya kuwasili kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi za Umoja wa Mataifa kabla ya kuanza kwa mkutano wa kamati ya maandalizi ya utekelezaji wa programu ya pamoja ya kusaidia Kigoma (KJP) uliofanyika jana jijini Dar es Salaam. Wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga na Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa Kigoma, Evance Siangicha.
 Mchambuzi  Mratibu wa Umoja wa Mataifa (UN Coordination Analyst )nchini, Kanali Rankho akitoa maelekezo kwa Adrian Fitzgerald kutoka Irish AID wakati washiriki wa mkutano wa kamati ya maandalizi ya utekelezaji wa programu ya pamoja ya kusaidia Kigoma (KJP)walipokuwa wakiwasili katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam.
 Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akitoa neno la ukaribisho wakati wa mkutano wa kamati ya maandalizi ya utekelezaji wa programu ya pamoja ya kusaidia Kigoma (KJP) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga na kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Charles Pallangyo.
 Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga (wa pili kulia)akizungumza wakati akifungua mkutano wa kamati ya maandalizi ya utekelezaji wa programu ya pamoja ya kusaidia Kigoma (KJP) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Charles Pallangyo (kulia), Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (wa pili kushoto) pamoja na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) nchini, Michael Dunford (kushoto).
 Kansela wa Ubalozi wa Norway, Britt Kjolas akitoa salamu kwa niaba ya wadau wa maendeleo wakati wa mkutano wa kamati ya maandalizi ya utekelezaji wa programu ya pamoja ya kusaidia Kigoma (KJP) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam.
 Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Charles Pallangyo (kulia) akifafanua jambo wakati wa mkutano wa kamati ya maandalizi ya utekelezaji wa programu ya pamoja ya kusaidia Kigoma (KJP) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam.
 Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa Kigoma, Evance Siangicha akiwasilisha rasimu ya makubaliano ya utekelezaji wa Programu ya KJP wakati wa mkutano wa kamati ya maandalizi ya utekelezaji wa programu ya pamoja ya kusaidia Kigoma (KJP) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Mchambuzi  Mratibu wa Umoja wa Mataifa (UN Coordination Analyst )nchini, Kanali Rankho
 Mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani (UNICEF) nchini, Stephanie Shanler akiwasilisha hatua iliyofikiwa kwenye utekelezaji wa mradi wa KJP eneo la kuzuia ukatili kwa wanawake na watoto wakati wa mkutano wa kamati ya maandalizi ya utekelezaji wa programu ya pamoja ya kusaidia Kigoma (KJP) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam.

 Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Viola Kuhaisa akiwasilisha hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa eneo la elimu wakati wa mkutano wa kamati ya maandalizi ya utekelezaji wa programu ya pamoja ya kusaidia Kigoma (KJP) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam.
 Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mfuko wa Mitaji ya Maendeleo (UNCDF) nchini, Prisca Mgomberi akiwasilisha hatua iliyofikiwa katika uwezeshaji  kiuchumi kwa wanawake na vijana wakati wa mkutano wa kamati ya maandalizi ya utekelezaji wa programu ya pamoja ya kusaidia Kigoma (KJP) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam.
 Mwakilishi Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) nchini, Kajsa Nyerere akiwasilisha hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa program ya KJP katika eneo la kilimo wakati wa mkutano wa kamati ya maandalizi ya utekelezaji wa programu ya pamoja ya kusaidia Kigoma (KJP) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam.
 Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa Kigoma, Evance Siangicha akifafanua jambo wakati akiwasilisha hatua iliyofikiwa kwenye programu nzima ya KJP wakati wa mkutano wa kamati ya maandalizi ya utekelezaji wa programu ya pamoja ya kusaidia Kigoma (KJP) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam.
 Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akifafanua jambo wakati wa mkutano wa kamati ya maandalizi ya utekelezaji wa programu ya pamoja ya kusaidia Kigoma (KJP) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam.


 Pichani juu na chini ni washiriki wa mkutano wa kamati ya maandalizi ya utekelezaji wa programu ya pamoja ya kusaidia Kigoma (KJP) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam.
Picha ya pamoja ya washiriki wa mkutano wa kamati ya maandalizi ya utekelezaji wa programu ya pamoja ya kusaidia Kigoma (KJP) wakiwemo wadau wa maendeleo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad